ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 25, 2013

Sheikh Amri Abeid hali bado tete

HALI bado ni mbaya uwanja mkongwe wa Sheikh Amri Abeid jijini licha ya kufungiwa na Bodi ya Ligi kuchezewa michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara hadi ukarabatiwe.

Toka kufungiwa kwa uwanja huo, Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), kimefanya juhudi za kuhakikisha kinashirikiana na wamiliki kurekebisha eneo la kuchezea bila mafanikio.

Akizungumza na Tanzania Daima, Katibu Mkuu wa ARFA, Adamu Brown, alisema jitihada za chama hicho kutaka kushirikiana na wamiliki wa uwanja ambao ni Chama cha
Mapinduzi (CCM), zimegonga mwamba.

“Nimejitahidi kukutana na viongozi wa chama kuhusiana na kufungiwa kwa uwanja huu lakini nimekwama licha ya kuonana na Katibu Msaidizi wa CCM Mkoa, lakini majibu yake yanaonyesha ni ngumu kufikia malengo tuliyokusudia kama chama,” alisema Brown.

Awali, licha ya kufungiwa kwa uwanja, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitaka kuingilia kati kusaidia ukarabati huo ili kuiwezesha timu ya taifa kuweka kambi jijini hapa, lakini baadaye waliamua kambi ibakie Dar es Salaam.

Kama hali ya uwanja itabaki kama ilivyo sasa, ambapo eneo la kuchezea lina mashimo yanayosababishwa na mchwa hivyo kuleta miinuko ya vichuguu, huenda timu ya Oljoro JKT inayoshiriki Ligi Kuu kulazimika kuuhama kumalizia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Meneja wa uwanja huo ambaye ameteuliwa hivi karibuni, hakutaka kuzungumzia hiyo kwa madai ya kutoruhusiwa na waajiri wake, lakini alidai baadhi ya shughuli mbalimbali za michezo zitaendelea katika uwanja huo.

No comments: