MKAZI wa Kijiji cha Mpunguti, Kata ya Katumba, Songwe wilayani Kyela mkoani Mbeya, Agust Mwamkinge (36), aliyetorokea nchini Malawi baada ya kutuhumiwa kumbaka na kumsababishia maumivu makali mtoto wake kwa malengo ya kupata utajiri, amekamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa katika harakati za kujiandaa kurejea kijijini humo.
Mwamkinge anadaiwa kutenda kosa hilo miezi mitatu iliyopita na kisha kutorokea nchini Malawi hatua iliyoulazimu uongozi wa kijiji kuwataka wanakijiji kufanya msako wa kumtafuta mtuhumiwa huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mpunguti, Richard Mwakanyikisye, alisema kuwa uongozi wa kijiji hicho uliwatuma askari mgambo wawili kwenda kumsaka mtuhumiwa huyo, lakini walizuiliwa na chifu wa Kijiji cha Mwambande, Wilaya ya Kalonga nchini Malawi.
Alisema kuwa kutokana na kizuizi hicho, uongozi wa kijiji ulilazimika kutoa taarifa polisi ambapo walipewa namba ya jalada RB KYL/IR/1768/2013.
Kiongozi huyo alisema kuwa baada ya askari hao kupewa namba hiyo, walianza msako na kufanikiwa kumkamata juzi saa 4:00 usiku kisha kumpeleka katika kituo kikuu cha polisi wilayani humo.
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Lusajo Mwakipiso, aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano walioufanya na kufanikiwa kumfikisha katika vyombo vya sheria.
Alisema kitendo alichokifanya baba huyo ni cha kusikitisha jambo ambalo limemsababishia masononeko mtoto wake.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kyela limekiri kumpokea mtuhumiwa huyo na kudai kuwa watamfikisha mahakamani pindi taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Awali baba huyo kabla ya kufanya unyama huo inadawa kuwa alianzisha ugomvi na mkewe saa 3:00 usiku na kuamua kumfukuza na ilipofika saa 8:00 usiku alimuingilia kimwili mtoto wake ambaye alikimbilia kwa mwenyekiti wa kitongoji baada ya kupata upenyo.
Ilielezwa kuwa mwenyekiti huyo aliitisha kikao cha dharura na kuwajulisha wanakijiji kuhusu kubakwa kwa mtoto huyo na ndipo walipoamua kumsaka.
No comments:
Post a Comment