WALE wenzangu na mimi ambao tumewahi au bado tunaendelea kuishi katika nyumba za kupanga na tunapanga maeneo ya uswahilini wa chumba kimoja kimoja, bila shaka ninaposema chumba kirefu wananielewa vema nina maana gani halisi ninayoilenga.
Kwa kifupi unaweza kusema kuwa, chumba kirefu ni sehemu ya katikati ya nyumba (corridor) ambayo imetenganisha chumba kimoja na kingine na mara nyingi kwa nyumba zetu za uswahilini, sehemu hii huwa si pana sana.
Nyumba nyingi za kupanga sehemu hiyo hutumiwa na wapangaji kama sehemu ya kupikia na kuhifadhia baadhi ya vitu vyao, ni nadra kukuta sehemu kama hiyo ikitumiwa kama chumba cha kulala na yeyote kati ya wakazi wa nyumba hizo, labda kwa sababu maalumu, kama vile wakati wa sherehe, misiba n.k.
Kutokana na ufinyu wake hata kama ikitokea kuna ulazima wa mtu kulala katika chumba kirefu, basi ni lazima alale chini ama kwa kutumia mkeka au godoro dogo na si vinginevyo.
Pia inapotokea umelala hapo, usingizi lazima uwe ni wa mang’amung’amu kutokana na sehemu hiyo kutumiwa pia na wapangaji kama njia wakati wanapokwenda msalani na kurudi.
Katika hali ya kushangaza, jamaa mmoja hivi karibuni alijikuta analazimika kutoka katika chumba chake cha kuishi na kuhamishia malazi yake katika chumba kirefu! Kisa? Tamaa ya pombe na starehe nyingine kupita uwezo!
Jamaa huyu ambaye kazi yake ni ufundi wa magari katika gereji moja maeneo ya Mwenge, jijini Dar es Salaam, tangu utoto wake hadi utu uzima unampigia hodi alikuwa akiishi pamoja na wazazi na ndugu zake maeneo ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Kwa bahati nzuri nyumba hiyo waliyokuwa wakiishi ni mali ya wazazi wao ambao waliijenga kutokana na kuitumia vema pesa yao kidogo waliyoipata katika ujana wao tofauti na kijana wao afanyavyo hivi sasa.
Katika hali ambayo haikutegemewa na watu wengi ambao wanaifahamu vema familia hiyo, mara tu baada ya wazazi wa fundi huyo kufariki dunia, yeye pamoja na ndugu zake wakaamua kugawana nyumba hiyo kwa vyumba, kila mmoja akapata vyumba vyake ambavyo alikuwa na maamuzi ya kuvifanya vyovyote isipokuwa tu kuviuza.
Kutokana na fundi huyu kupenda sana kinywaji kuliko uwezo wa kipato chake kitokanacho na ufundi wake, muda mfupi baada ya kumilikishwa vyumba viwili vya nyumba hiyo, akaingiwa na tamaa na kuamua kupangisha chumba kimoja na kubakiwa na kingine ambacho alikitumia kwa malazi yake.
Baada tu ya kupata pesa yake ya kodi ya mwaka, jamaa huyu alijihisi kama vile kapata pesa ya EPA na kuamua kuhama kabisa viwanja vyake vya kila siku vya banana na mwamba na kuingilia anga za kunywa bia na konyagi! Kana kwamba na yeye ana pesa ndefu yenye uwezo wa kustahimili vishindo vya vinywaji hivyo kwa maisha yake yote yaliyobaki hapa duniani!
Kwa kuwa muonja asali huchonga mzinga, basi zilipomwishia tu zile za chumba kimoja, akaingiwa na tamaa zaidi na kuamua kupangisha tena hata kile chumba alichokuwa anaishi yeye mwenyewe na kuyarudia tena maeneo yale yale ya wenye pesa zao za kinywaji na kuendeleza matanuzi ya nguvu.
Kwa sasa pesa zote zimemwishia, vyumba vyote kapangisha, hivyo anachokimudu sana sana akipata vijipesa kidogo ni kunywa banana alizozisusia baada ya kupangisha vyumba na kuvizia usiku watu wote wakiwa wamelala na kuingia chumba kirefu na kuvuta mbavu zake hapo hapo kama mkimbizi aliyeomba hifadhi ya malazi ya siku moja akiwa mbioni kuelekea sehemu nyingine!
Maisha ambayo yanamlazimu kila siku yeye ndiye awe wa mwisho kulala na inapokaribia kucha ni lazima pia awe ndiye wa kwanza kuamka, kwa maana chumba kirefu ni mali ya wapangaji wote kwa kupita, kupikia na kuhifadhi baadhi ya vitu vyao.
Hayo si mambo hata kidogo, tamaa ya starehe zipi hizo hadi upangishe chumba chako mwenyewe cha kulala na kujikuta unaishia kuwa mkimbizi ndani ya nyumba yenu? Bila shaka huo ni uchizi na si tamaa ya kustarehe.
No comments:
Post a Comment