ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 6, 2013

UNAONGOZWA NA TAMAA AU UNAUSIKILIZA MOYO WAKO?

KARIBUNI tena katika safu yetu nzuri ya kubadilishana mawazo juu ya uhusiano na mapenzi. Ni imani yangu kuwa mtakuwa wazima wa afya njema. Rafiki zangu, maisha ya uhusiano bila furaha ni kazi bure. Amani katika mapenzi ndiyo dira.

Hivi ni kweli kwamba unautendea haki moyo wako? Mpenzi uliyenaye unampenda au unajilazimisha tu kuwa naye? Majibu ya maswali hayo ndiyo mwongozo wa mada yetu ya leo.

Somo la leo litakupa mwanga wa kujua haki ya moyo na tamaa za mwili wako ni kipi sahihi kutendewa haki. Elewa kuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi.


Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mapenzi hayo, hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, wewe ni mtumwa wa mapenzi!

Kama ndivyo, kwa nini uwe mtumwa? Unadhani hakuna mwingine anayeweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi!
Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako! Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe!

Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda? Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi!

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria! Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu!

Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla. Hii inamaana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana, lazima utamkaribisha!

ACHA KUBAHATISHA
Baadhi ya wasichana, wakitongozwa na wanaume ambao wanaona wazi kuwa hawana mapenzi nao, lakini wakawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kuwakubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume hao. Hufanya hivyo wakijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo.

Fikra zake huhama kwenye mapenzi na kufikiria kuhusu pesa na mali. Hutamani maisha mazuri bila kujali moyo wake. Hili ni tatizo. Fahamu kwamba kwa kufanya hivyo, mateso katika maisha yako yapo njiani yanakuja.

MADHARA
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa uhusiano wenu. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.

Ikiwa kinyume chake ni mateso tu ambayo kumbe uliyagundua mapema na ulikuwa na nafasi ya kujiweka pembeni kwenye matatizo ambayo siyo ya lazima.
Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katia uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa. Unajua kitakachotokea baada ya hapo? Ni kuachika tu.

Ni bora iishie hapo, uachwe salama lakini kama mwaname mweyewe ana hasira na mwenye kuchukua uamuzi wa haraka, anaweza kusababisha madhara yoyote.

CHUKUA HII
Kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda, ni jambo gumu ambalo huweza likaharibu maisha yako kabisa. Jambo ambalo linaweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa.

Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: