ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 6, 2013

HATA KAMA UNADHANI KUCHEPUKA NJE YA NDOA NDIYO DAWA?


NIMEKUWA nikipokea malalamiko mengi sana ya migogoro ya ndoa huku chanzo kikubwa kikitajwa kuwa usaliti! Nimejitahidi kutumia uwezo wangu wote katika kutatua migogoro hii, ndiyo maana leo nimelazimika kuiweka wazi makala hii.

Kwa utafiti nilioufanya kwa siku za hivi karibuni, nimebaini kuwa asilimia zaidi ya themanini ya ndoa zivunjikazo chanzo kikubwa huwa ni usaliti!

Swali kubwa ambalo nimekuwa nikijiuliza ni je, kuchepuka nje ya ndoa ndiyo dawa? Huko unakokimbilia kuko salama kiasi gani? Ni nani aliyekamilika? Ukigundua tatizo lingine kwa huyo wa nje unakimbilia wapi tena? Utaacha wangapi au utachepuka nje ya uhusiano mara ngapi? Haya ni maswali ambyo unatakiwa kujiuliza.

Wiki iliyopita nilitembelewa na dada mmoja ofisini kwetu, alikuja analia na kuhitaji msaada wa ushauri juu ya ndoa yake inayokaribia kuvunjika kutokana na usaliti mkubwa wa mumewe.

Nilizungumza mengi sana na dada yangu huyo, wakati wa mazungumzo ndipo nikabaini chanzo kikubwa cha wanandoa kwenda nje ya ndoa au kuwa na nyumba ndogo.
Mosi, tatizo kubwa linalochangia wanandoa wengi kuchepuka ni kutotimiziwa kwa usahihi waliyoyatarajia kutoka kwa wenzi wao.

Lakini pia, sababu kubwa zaidi ni kushindwa kuwa wakweli kwa wenzi wao na kutoa maelekezo stahiki palipo na upungufu.
Sababu nyingine ambayo kwa sasa inazidi kushamiri, ni uwezo mdogo wa kuzuia na kudhibiti tamaa. Wakati mwingine mkumbo wa marafiki! Hapa chini nitachambua kipengele kimoja baada kingine.

KUKOSA WALIYOYATARAJIA:
Kila mtu aingiapo kwenye uhusiano, kuna mambo ambayo huyatarajia kuyakuta ndani ya uhusiano huo. Huingia katika uhusiano kwa furaha kubwa akitarajia ubora wa hali ya juu kutoka kwa mwenzi wake.

Tatizo huanzia pale anapokutana na hali tofauti na jinsi alivyokuwa akitarajia! Hujikuta akikata tamaa na kuanza kufikiria njia mbadala ya kupata aliyoyatarajia na hapo ndipo neno usaliti huzaliwa ubongoni mwa mhusika. Hii ni hatari sana.

Mfano alitarajia kuona mwenzi wake akiwa katika hali ya usafi kila kipengele na sasa anakutana na kinyume chake. Au alitarajia heshima kubwa sana kutoka kwa mwenzie lakini anakutana na hali tofauti.

Pengine alijenga picha ya ufundi mkubwa wa kwenye uwanja wa sita kwa sita kutoka kwa mwenzie na sasa anakumbana na ugoigoi mkubwa, jibu la kwanza kuingia kichwani ni kuchepuka kwenda nje ya ndoa hata kama hapendi!

KUTOKUWA MKWELI!
Ukweli ninaouzungumzia hapa ni ule wa kumweleza wazi mwenzio bila kumficha wala kupepesa macho hata kidogo juu ya upungufu alionao.

Mathalani unakuta mtu kaolewa au kuoa mwanamke mwenye upungufu kwenye eneo la usafi wa mwilini au mavazi na sehemu nyinginezo lakini badala ya kukaa naye chini na kumweleza tatizo hilo, anabaki akiumia moyoni hatimaye kufikia hatua ya kutafuta faraja na furaha sehemu nyingine. Usaliti!

Mtu anadhani akimweleza mwenzie udhaifu wake kitandani atajisikia vibaya hivyo ni bora kunyamaza na kuangalia sehemu nyingine ambayo ataweza kujipatia furaha anayoikosa kwenye ndoa. Jambo baya sana.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: