ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 12, 2013

HATA KAMA... UNADHANI KUCHEPUKA NJE YA NDOA NDIYO DAWA?-2

NAMSHUKURU Mungu kwa mara nyingine tena kwa kunijaalia fursa hii ya kuzungumza nanyi wapenzi wasomaji wa safu hii. Jamani mambo vipi? Maandalizi ya sikukuu yanakwendaje? Natumaini mambo yanakwenda vizuri.

Haya karibuni tena kwenye mambo ya malavudave, si unajua bila mapenzi hakuna maisha! Huo ndio ukweli. Huwezi kuishi kama jiwe au mti, raha ya maisha ni kuwa na mwenzi atakayekupenda kwa dhati na kutokuwa tayari kukusaliti kwa namna yoyote ile.

Kwa wale walio katika ndoa zenye furaha watakubaliana na mimi kuwa mapenzi yenye amani na masikilizano ni kama ‘ka paradiso’ kadogo ndani ya ulimwengu huu!
Wakati mwingine unaweza hata kujikuta umeshiba bila kula, eti kwa sababu tu umemuona mwenza wako au kuwa naye karibu tu, yaani yeye kwako ndo’ mambo yote, yeye ndio kila kitu! Raha ilioje!

Mpenzi msomaji wangu, wiki iliyopita utakumbuka nilianza kuzungumzia mada yenye kichwa cha habari kilichopo hapo juu. Ni mada inayowagusa wanandoa kwa kiasi kikubwa.
Lengo kubwa ni kutaka kuonesha umuhimu wa wanandoa kutulia na kutokuwa macho juujuu kutaka kuzisaliti ndoa zao. Nikagusia pia mambo yanayochangia baadhi ya watu kutoka nje ya ndoa kama ambavyo naendelea hapa chini.

KUSHINDWA KUZUIA TAMAA!
Ni kama hulka fulani iliyojengeka kwa wengi wetu. Ni kweli kama binadamu uliyekamilika, unakula na kushiba lazima utakutana na hali ya uhitaji wa faragha hata kama uko mbali na mwenzi wako, lakini ni kweli kabisa unashindwa kuzuia tamaa hiyo?
Unakuta mwanamke au mwanaume anakutana na mtu na kumtamani kutokana na ubinadamu, lakini bila kujiuliza mara mbili anajikuta anaamua kuingia kwenye usaliti.

MKUMBO WA MARAFIKI
Wapo ambao hawakuwa na chembe yoyote ya usaliti kabla ya kukutana na marafiki wenye hulka na tabia hizo. Unakuta mtu yuko na marafiki ambao tabia zao si nzuri hivyo hujikuta akishawishika na kusaliti ndoa aliyoipenda kwa muda mrefu.

MUHIMU
Maisha yanahitaji umakini wa hali ya juu sana. Akili iliyokomaa inatakiwa kutumika kukabiliana na changamoto za maisha. Kama kuna eneo ambalo mwenzi wako anapwaya, ishu ya msingi ni kukaa naye na kumweleza kila kitu tena kwa upendo wa hali ya juu kuhusu udhaifu alionao.
Lakini pia usiishie kumweleza tu udhaifu alionao, badala yake unatakiwa kupiga hatua mbele zaidi kumweleza nini cha kufanya ili kuondokana na tatizo hilo.

Hapo unatakiwa kulichukulia tatizo lake kama la kwako kwani tayari ninyi ni mwili mmoja sasa. Hapa namaanisha kwa walio ndani ya ndoa!
Mwisho kabisa nataka kuweka kumbukumbu sawa kuwa, hakuna aliyekamilika chini ya jua. Kama binadamu ni lazima mtagombana tu lakini kuchepuka na kwenda kwa nyumba ndogo au ‘kidumu’ siyo dawa ya matatizo ya ndoa yako.

Huenda huko unakokimbilia ndiko kuna matatizo makubwa zaidi, unajikuta unaingia kwenye mtandao wa wapenzi wengi kwa kukosa jambo moja tu muhimu katika maisha, uvumilivu na uelekezaji kwa mwenzako!

Fikiria maisha, boresha ndoa na kumbuka waliotoka nje ya ndoa zao leo hii wengi wao wanajuta. Hakikisha huwi miongoni mwao.

GPL

No comments: