.jpg)
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amekata rufaa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupinga hatua ya kuvuliwa wadhifa wa Unaibu Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Aidha, aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk. Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, ambao walivuliwa nyadhifa zao pamoja na Zitto, waliwasilisha utetezi wao kwa maandishi jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa Mbunge huyo, Albert Msando, alisema Zitto amefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa utaratibu wa kumvua uongozi umekiukwa, ikiwa ni pamoja na sababu za kuchukuliwa hatua hizo kuwa siyo sahihi.
Msando alifafanua kuwa kwa mujibu wa katiba na kanuni za Chadema za uendeshaji kifungu namba 6.5.6, kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu, bila ya kwanza kupewa mashitaka yake kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kujibu mashitaka kwa maandishi.
“Pia tunapenda ijulikane kwamba kanuni ya uendeshaji 6.5.2 kifungu (a), (b), (c) kama ilivyorekebishwa Januari 2013 ambayo inasema kwa mujibu wa ibara ya 5.4.3 ya katiba, mwanachama yeyote hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa, ama kuachishwa ama kufukuzwa uanachama bila mambo kadhaa kufanyika."
Msando aliyaainisha mambo hayo kuwa ni kujulishwa makosa yake kwa maandishi na kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili, kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao kinachohusika na kujulishwa uamuzi wa kikao wiki mbili baada ya kusikilizwa.
"Vile vile, Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu (b), (c) hapo hapo juu kama itaona maslahi ya chama kwa ujumla yanaweza kuathiriwa, isipokuwa mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa atalazimika kuitwa kwenye kikao hicho," alisema.
Aidha Msando alifafanua kuwa uongozi wa Chadema ulifanya mkutano wake na waandishi wa habari Novemba 26, mwaka huu, kwa kusema kwamba marekebisho ya kanuni ndiyo yaliyofuatwa kuwavua madaraka.
Alisema kanuni hiyo hakuifahamu, hivyo alidanganywa kwa kufuata kanuni ya zamani huku ikiwa imeshabadilishwa na kwamba mabadiliko hayo yamefanywa katika kipengele (d), kuhusu hatua ya dharura iliyochukuliwa na kamati kuu ya Chadema.
Kwa mujibu wa Msando, Zitto hakupewa mashtaka yake bali aliyakuta ndani ya kikao baada ya kupewa taarifa kwa ujumbe wa simu na kwa uzito wa makosa hayo yaliyosababisha kuvuliwa uongozi na kwa kuangalia athari zake kwake yeye binafsi, na chama kwa ujumla kamati kuu ilitakiwa kujiridhisha kwamba kanuni na uendeshaji pamoja na katiba zinafuatwa.
"Hivyo, Zitto ametoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa chama kumweleza nia yake ya kukata rufaa kwa Baraza Kuu la chama kupinga hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu dhidi yake, kumvua nyadhifa zake ndani ya chama," alisema.
Wakati huo huo; Dk. Mkumbo na Mwigamba jana waliwasilisha utetezi wao kwa maandishi.
Msando, alisema Dk. Mkumbo na Mwigamba waliwasilisha utetezi wao baada ya kupokea barua za mashitaka, ambazo ziliwataka wajitetee kwa maandishi na wamefanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na kanuni za uendeshaji za chama.
Katika hatua nyingine; Mwigamba amewasilisha malalamiko yake kwa Msajili wa Vyama ili atoe mwongozo kuhusu mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya chama hicho, kufuatia kipengele cha katiba kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume cha utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kwenye katiba ya 2004 kipengele cha 5.3.2 kinasema kiongozi anayemaliza muda wa uongozi, ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena ilimradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja.
Mwigamba alifafanua kuwa hata hivyo katiba ya 2006 kipengele cha 6.3.2 (c) inayozungumzia muda wa uongozi, inasema kwamba kiongozi aliyemaliza muda wa kiongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena ilimradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.
“Sentensi kuhusu ukomo wa uongozi haipo, ni kweli kuwa marekebisho yalifanyika 2006, lakini hoja ya kubadili kipengele hicho haikuwepo kwenye muhtasari unaoonyesha wazi kuwa kulikuwa hakuna mjadala wa kipengele hicho au kuhusu suala zima la ukomo wa uongozi,” alisema Mwigamba.
Aliongeza kuwa siyo kweli kuwa Chadema haijawahi kuwa na katiba ambayo ina ukomo wa uongozi, pia alisema siyo kweli kwamba mwaka 2006 katiba iliandikwa bali marekebisho yalifanywa kwa baadhi ya vipengele na kipengele 5.3.2 (c) haikujadiliwa.
“Natumaini kuwa Msajili wa vyama ataweza kutupatia hekima zote na kutoa mwongozo ili suala hili lipatiwe suluhisho la kudumu ndani ya chama chetu,” alisema Mwigamba.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment