ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 16, 2013

UHUSIKA WA WAZAZI HUSABABISHA MTOTO AWE GUMEGUME AU GUBEGUBE KATIKA MAPENZI -4


KWANZA tuwe tumeshakubaliana na ukweli kwamba mzazi ni kichocheo cha mtoto kuwa mhusika bora katika mapenzi, baada ya hapo tutakuwa na mawazo yanayoshabihiana kwamba gubegube au gumegume mara nyingi ni matokeo ya malezi mabaya.

Tuendelee kutoka hapohapo, sasa ni muongozo kwako kuwa haina maana kuwa unaweza kusamehewa na kuachwa kama ulivyo eti kisa ndivyo ulivyolelewa. Nani atakukubali kama wewe ni mzigo usiobebeka? Tafakari kisha chukua hatua.

Haitawezekana kupata msamaha kwa uhusika wako mbaya kwenye mapenzi kwa kujitetea eti hicho ambacho unakionesha ndicho ulichojifunza kutoka kwa wazazi wako. Utaulizwa, akili yako inafanya kazi gani mpaka ushindwe kujitambua na kujibadilisha?

Chochote utakachokuwa unakishuhudia kutoka kwa wazazi wako. Picha ambayo utaipata kwa baba na mama, iwe mbaya au nzuri ni vizuri ikakujenga katika misingi iliyo bora. Hakuna msamaha endapo utakuwa na sifa yoyote mbaya kwenye mapenzi.

Ukiwa katili, kiburi, jeuri, mwenye dharau, mbinafsi na sifa nyingine mbaya zinazofanana na hizo, lawama hazipaswi kuwa za mzazi tena, hasa unapokuwa na umri juu ya miaka 18. Umepewa akili hebu changanua kwa ufasaha.

Maisha ya kimapenzi ni vile ulivyo. Chukua mfano huu; nenda kwenye kioo kisha jitazame. Anza kutabasamu, bila shaka taswira utakayoiona ni tabasamu lako. Ukinuna utajiona umenuna. Vivyo hivyo, ukiyachekea maisha, nayo yatakuchekea. Ukiyakunjia ndita, nayo yatakukunjia.

Sasa basi, kwa vile umepewa akili, na unawaona watu wengi jinsi wanavyohusika kwenye mapenzi yao. Unapomuona mtu anayeishi vizuri na mwenzi wake unamjua, basi muige. Usijifanye hujui, wanauliza; kusoma hujui, na picha huoni?

UNAWEZA KUBADILIKA
Niongezee kwa msisitizo kwamba ni kweli bila shaka kuwa suala la ugubegube na ugumegume ni matokeo ya malezi kwa maana kwamba inawezekana wazazi wakawa wazuri sana lakini wakashindwa kusimamia vizuri ukuaji wa watoto wao.

Hili jambo ni muhimu pia liwekwe kwenye mzani wake kwamba wazazi wengine hukimbia majukumu ya kulea, matokeo yake akina dada wa kazi au ndugu ndiyo wanaohusika. Baba na mama wanaweza kuwa familia ya mfano lakini watoto wakawa ovyo.

Ni hapo sasa inalazimu mzazi kuwa karibu na mwanaye kila siku. Awe anaona vitabia vya ajabuajabu kutoka kwa mtoto wake na kuvishughulikia ipasavyo na kwa haraka sana. Ni kosa kubwa kwa mzazi kumuacha mtoto akue vibaya.

Nifafanue hapa; mzazi anakosea sana kumuacha mtoto wake akue vibaya, yaani bila misingi imara ya kimaadili na namna ya kujumuika na jamii yake. Anayejua kujumuika na jamii yake, hakuna shaka kwamba atakuwa mhusika mzuri wa kimapenzi.

Hata hivyo, ufafanuzi baada ya kipengele hicho ni kwamba mtoto anapofikisha umri wa miaka 18, hatakuwa na wa kumlaumu kuwa alimnyima fursa ya kumjenga kimaadili. Ana akili timamu, anapaswa kujiongoza mwenyewe.

Hata katika sheria za nchi inatamkwa kwamba kutokujua sheria hakukupi nafasi ya kuvunja sheria. Ukishakuwa mtu mzima inakubidi uwe mjanja na unayejiongoza kila siku. Kuna walionyimwa fursa ya kusoma kutoka kwa wazazi wao lakini walijisimamia wakiwa wakubwa, wakajisomesha mpaka kupata shahada za vyuo vikuu.

Acha tabia ya kulaumu, maana wapo watu mpaka leo, mtu anafikisha umri wa miaka 50 lakini bado anamlaumu mzazi wake kuwa hakumsomesha. Kila siku unatakiwa ujichanganue unataka kuwa nani kisha ujitengenezee mazingira ya kufika unapopataka.

Soma vitabu, soma makala za mapenzi, peruzi hadithi, tazama tamthiliya na filamu zenye historia za mapenzi (love stories), hizo zikujenge kutambua kuwa mume au mke bora anatakuwa aweje kwenye uhusiano, kwa hiyo nawe ujitengeneza kuenenda katika taswira hiyo.

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: