ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 23, 2013

UHUSIKA WA WAZAZI HUSABABISHA MTOTO AWE GUMEGUME AU GUBEGUBE KATIKA MAPENZI -5


KUTOKA mwanzo wa makala haya mpaka hapa tulipofikia, sina shaka utakuwa umeshatambua namna ambavyo uhusika wa wazazi unavyoweza kuwafanya watoto wao kuwa ama magubegube au magumegume katika mapenzi.

Kutoka hapo, sasa tuhitimishe mambo machache kwa kupeana maelekezo ya kimsingi ambayo yanaweza kukusaidia katika maisha yako ya kimapenzi hata kama ulipata muongozo wa ovyo kutoka kwa wazazi wako. Haishindikani wewe kuwa bora hata kama msingi wako ni mbovu.

Binadamu si kama nyumba, kusema kama msingi wake siyo imara basi ndiyo haitawezekana ‘mjengo’ kuwa bora mpaka msingi usukwe upya. Kuna tofauti kubwa, kuna hitaji dogo la kuzingatiwa kumfanya mtu mwenye sura ya shetani kuonekana malaika.
Hitaji hilo dogo ni kujitambua. Kama mtu mwenye muonekano mbaya kijamii kama shetani akijitambua na kuamua kwa dhati kabisa kubadilika, basi anaweza kutoka alipo hadi kuonekana mzuri kama malaika. Hilo halijawahi kuwa gumu kwa yule mwenye nia ya dhati.

ANZA LEO
Umeshabaini kuwa uhusika wako katika mapenzi una kasoro. Pengine unakuwa na matendo ya hapa na pale ambayo yanamkera mwenzi wako, vivyo hivyo kuufanya uhusiano wenu usiwe na furaha inayotakiwa. Jukumu lako kuu ni kujifanyia masahihisho.

Njia ni hii; Umeshajitambua, kinachofuata ni kujikagua mahali ambapo unakosea. Yapitie makosa yako yote. Si kila kitu ambacho mwenzi wako anakulaumu lazima kiwe tatizo, badala yake unapaswa kuchuja kila jambo. Yote yanayohusika, yaweke kwenye kioo cha ukweli kisha changanua.

Hata kama ulipata malezi mabaya kiasi gani lakini haiwezekani ukawa mbaya kwa kila kitu. Kwa maana hiyo, baada ya kuchuja kupitia kioo cha ukweli, kinachofuata ni kuachana na yote mabaya ambayo yanakuchafua kisha anza mazoezi kabla ya kuzoea kutenda yaliyo mema ambayo yatakujengea sifa njema.

Njia za kufanikiwa katika hilo ni nyingi. Kwanza unaweza kujipa jukumu binafsi (self assignment) la kujitathmini. Huwezi kugundua kama una matatizo ikiwa huelewi watu safi wapoje. Soma uhusiano wa wengine, utaona wahusika wazuri na wabaya.
Soma vitabu vya hadithi na vile vya uhusiano wa kimapenzi. Peruzi makala zinazotoa mafundisho kuhusu uhusiano wa kimapenzi. Tazama tamthiliya na filamu zenye simulizi za mapenzi. Ukitekeleza hayo, bila shaka utaweza kubaini yupi mhusika mzuri na nani ni mbaya.

Katika maeneo unayoishi, fuatilia uhusiano wa walio karibu yako. Ukiwa mdadisi, utaweza kubaini wale wanaoishi vizuri na kwamba mapenzi yao ni mfano wa kuigwa. Kama ndivyo, basi unazo njia mbili za kukuwezesha kufanikiwa.

Mosi ni kuiga mema ya hao uliobaini wanaishi vizuri. Vaa viatu vyao halafu ukanyage pale wanapotoa miguu yao. Vilevile unaweza kuwafuata na kuomba ushauri wao. Wakueleze ni kwa jinsi gani wao wapo hivyo. Itumie elimu watakayokupa kujijenga na kuubadili uhusiano wako kutoka hapo ulipo.

Siku zijazo utakuja kujikuta unaitwa mtu bora wa mfano katika uhusiano wako. Unaweza kumfanya mwenzi wako aondoke alipo sasa ambapo anakulaumu kwa uhusika wako mbaya pia anajilaumu kuwa na wewe, hadi kukusifia na kujipongeza kwa kukupata.

MSISITIZO
Nisisitize kuwa suala la ugubegube na ugumegume ni matokeo ya malezi kwa maana kwamba inawezekana wazazi wakawa wazuri sana lakini wakashindwa kusimamia vizuri ukuaji wa watoto wao na matokeo yake kukabidhi jukumu la malezi kwa watu wengine.

GPL

No comments: