
Kazi ya viongozi wa dini, mila au serikali ni kuwaunganisha tu. Kazi yao humalizikia hapo, sasa suala la furaha ya ndoa ni kazi yenu wenyewe kama wanandoa mkiwa ndani.
Ndugu zangu, hivi umeshawahi kujiuliza; kwa nini mwanandoa anatoka nje? Anafuata nini? Unajua unaweza kushangaa, ukiambiwa fulani anatoka na mwanamke mwingine nje, wakati mke wake ni mzuri wa umbo, sura na tabia.
Watu wakimwangalia wanamsumbua kila kukicha, wanaota ni lini watampata japo kwa muda mfupi tu! Lazima ujiulize swali hili. Lakini hata wewe ambaye labda umeshatoka nje au upo katika fikra hizo, lazima ujiulize, unatafuta nini nje?
Mume/mkeo ana kasoro gani? Nini tatizo? Nawe ambaye mwenzi wako ametoka nje na una hakika na jambo hilo, inakupasa pia ujiulize na upate majibu ya swali hilo. Kwa nini ametoka nje? Kuna nini huko nje ambacho wewe humpi?
Rafiki zangu, asikudanganye mtu, tatizo kubwa kabisa huanzia katika kupoteza hisia. Ukiwa na mwenzi wako, yakafanyika makosa na likatokea tatizo la kupotea kwa hisia za mapenzi, ndiyo chanzo cha yote hayo.
Hakuna kanuni za moja kwa moja za mapenzi ndugu zangu lakini yapo mambo ambayo kiukweli kama yakizingatiwa vizuri, msisimko wa mapenzi huongezeka na kujikuta ukizidi kumuona mwenzi wako mpya kila siku.
TATIZO HUANZIA HAPA
Wengi huwa hawapati muda wa kufikiri na kutafakari juu ya jambo hili, lakini furaha ya mtoto wa kwanza, wakati mwingine hugeuka kero na msumari katika ndoa.
Wote hufurahia mtoto wao mpya lakini mama asipokuwa makini ndiyo kipindi ambacho anaweza kujikuta akipoteza msisimko wa tendo kwa mumewe. Kwa kawaida, mwanamke akishajifungua na muda wa kukutana na mumewe ukifika, mshawasha wake huwa wa juu zaidi.
Ni kipindi ambacho mwanamke humhitaji mumewe kwa muda mrefu zaidi. Atapenda awahi kurudi nyumbani, wale pamoja na kulala mapema ili aweze kufurahi naye.
Tatizo linakuja katika utaratibu mpya wa maisha baada ya kujifungua. Baadhi ya wanawake hujisahau na kuanza kufanya mambo yanayopunguza msisimko bila kujua.
Bahati nzuri ni kwamba, wakielezwa huelewa haraka sana. Hebu twende tukaone zaidi...
MAPENZI KUHAMIA KWA MTOTO
Kwanza kabisa mwanamke akipata mtoto hujikuta akimpenda zaidi mwanaye kuliko mumewe. Si kwamba hampendi mume wake tena lakini mapenzi kwa asilimia kubwa kipindi hiki huhamia kwa mwanaye.
Mwanamke anaweza kukesha usiku mzima, mwanaye akiwa pembeni yake na kumwacha mumewe peke yake. Hili ni tatizo na husababisha kupunguza msisimko wa mapenzi. Ni jambo hatari ambalo linaweza kusababisha mume kufikiria kuwa na mwanamke mwingine wa nje.
Si ajabu kichwani anaamini hafanyi makosa bali anakuwa na mwanamke wa muda kwa ajili ya kumpisha mkewe amlee kwanza mtoto wao. Acha kujidanganya rafiki, hilo ni kosa kubwa sana. Kwenye ndoa, usaliti ni sumu!
Wiki tutamalizia mada yetu.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
1 comment:
joseph shaluwa nimesoma kwa makini hii issue yako na nimependa sana sema ilipofika uliposema kwamba mwanammke anahamisha mapenzi yake kwa mwanaye sana kuliko kwa mumeo ni kweli lakini huyo mume kwa nini asielewe mtoto mchanga anahitaji kulelewa na yeye pia mume anahitaji hilo lakini naona kama kuna ushindani ni kweli mwanamke atakuwa anakosea lakini ni mlezi mwanamke ndo maana anamlea huuyo mume pia baba jitu zima tukubaliane na hilo
in a way mwanamme ni kiumbe kilicho selfish tukubali tukatae ndo ilivyo ndo maana unaambiwa ukimpata mtoto wa kike ukamsomesha shule basi umeisomesha jamii nzima mwanamkee ni mtu wa kushare na ni mlezi mwanamme yeye anajali yake tuu ni ukweli halisia mara nyingi katika makaaala eti tu na onywa hivyo mwanamkke akiza sijui hivi na vile mbona hamuwaonyi kwa kuwa selfish hao wanaumeee???
na nimefurahi ulivyosema usaliti ni sumu ninzuri sana unajua uandishi wako kweli kwa kutuliza madaa hongera
Post a Comment