ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 7, 2014

Kalenga ilivyozizima mazishi ya Mgimwa

Rais Jakaya Kikwete akiwa na mkewe Mama Salma, wakiweka shada la maua juu ya kaburi la aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, katika mazishi yaliyofanyika kijiji cha Magunga Kata ya Maboga eneo la Kalenga mkoani Iringa jana.

Simanzi ilitanda jana katika mji wa Kalenga wakati Rais Jakaya Kikwete, alipowasili katika kijiji cha Magunga, mkoani Iringa kwa ajili ya kuongoza umati wa waombolezaji waliojitokeza kuhitimisha safari ya mwisho duniani ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa.

Halikuwa jambo la kawaida kwa wananchi wa Iringa kukubali kifo cha Dk. Mgimwa na mara zote walisikika wakipaza sauti bila kujali hisia zao, wakieleza kuwa hakuna mbadala wa kiongozi huyo ambaye alikuwa akitumia fedha zake za mfukoni kuwanunulia chakula wananchi wake, kugawa bure mbolea kwa ajili ya kilimo na kutafuta ada za wanafunzi waliokosa uwezo jimbo zima pasipo ubaguzi.

Wakati wote, makundi ya wananchi hasa wakazi wa Kalenga, walijikusanya nje ya makaburi ya familia ya Waziri Mgimwa ambaye alikuwa Mbunge wa Kalenga wakitafakari hatma yao baada ya msiba huo wakiangua vilio kwa nyakati zote huku jamii ya kabila la Wahehe wakidai kifo hicho kwao ni sherehe kwa mpendwa wao aliyetangulia mbele ya haki.

“Huyu hakuwa mtu wa kujikweza wala kugombana na viongozi wenzake, kwa nini Mungu ametenda haya? Nani atakayeweza kubeba uchungu aliokuwa nao kwetu kwa sababu alituletea chakula, anatugawia mbolea bure na alitupa fedha zake za mfukoni kusomesha watoto wetu hapa jimboni...Kweli tumepoteza jembe letu na hatuwezi kumpata mtu wa aina ya Mgimwa,” alisema David Kisinini, Mchungaji wa Kanisa la Living Fire Gospel Assembly.

Ilipofika saa 3:30 asubuhi, Mshauri Makamu wa Askofu (Monsinyori) Julian Kangalawe aliyemwakilisha Askofu wa Jimbo la Iringa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Tarcius Ngalalekumtwa, alianza kuendesha ibada ya mazishi baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na viongozi wa serikali kuwasili makaburini akiwataka wanasiasa wa Tanzania waache kufanya madudu mbele ya umma huku wakijua kwamba waliapa kulitumikia taifa.

“Inashangaza kuwaona wanasiasa wetu hawa wanazozana, wanagombana na kuchukizana, lakini wakae wakijua kwamba hilo wanalolifanya halitabadili maisha na mtazamo wa Watanzania. Kama mtu ni mbadhirifu ataendelea kuwa mbadhirifu, lakini mpenda haki ataendelea kutenda haki...Kule bungeni wanaapa na tunawaona kwenye televisheni kwamba wataitumikia vyema nchi yao, lakini wakitoka hapo ni madudu,” alisema Kangalawe.

Aliongeza: “Watanzania siku hizi tunaogopana na tunaona ni utamaduni kwamba mwenye nacho aendelee kuwa nacho lakini maskini atabaki na umaskini wake, wanasiasa wetu hebu mtusaidie kukaa pamoja tena kwa ustaarabu na kuanza kuwapenda wengine na hasa kama alivyokuwa akifanya Dk. Mgimwa wakati wa uhai wake.”

PINDA AWATULIZA WANANCHI
Saa 7:30 Rais Jakaya Kikwete, akiwa ameongozana na Mama Salma, walifika katika makaburi ya familia ya mzee Augustao Mgimwa, na kuungana na waombolezaji huku Pinda akiwataka wakazi wa Kalenga na Mkoa wa Iringa kutambua kwamba kifo cha Dk. Mgimwa kimetokana na mapenzi ya Mungu.

“Natambua kwamba mna machungu mengi sana lakini la msingi ni kuelewa kwamba kuna maisha mengine baada ya haya. Sisi tulimpenda, lakini yuko aliyempenda zaidi.
Tunawaomba mpokee tukio hili kwa mikono miwili, lakini ukweli ni kwamba afya yake ilianza kutetereka tulipomtuma Marekani mwezi mmoja kabla ya kuugua na alipokuwa kule tulipokea taarifa zake na tukaamua akatibiwe Afrika ya Kusini (Kloof Medi-Clinic) hadi mauti yanamfika,” alisisitiza Pinda.

Alisema Rais Kikwete alipomteua kuwa Waziri mwenye dhamana, alijua kwamba Wizara ya Fedha itatulia na kwa kweli aliweza kuituliza kwa sababu alikuwa mtu stahiki na kwamba pengo lake linaonekana.

MSIGWA AIBUA VICHEKO
Baadaye, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa, ambaye alimwakilisha kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisimama mbele ya Rais Kikwete na kuibua sauti za waombolezaji waliopaza sauti kumshangilia baada ya kuwananga wanasiasa wenzake
akisema kuwa kuanzia sasa iwe ni aibu kufa kabla mtu hajatoa mchango wake kwa taifa na kwamba Dk. Mgimwa aliweza kutekeleza hilo katikati ya mawaziri wenzake kwa muda mfupi akiwa Waziri wa Fedha.

AZIKWA KICHIFU
Baada ya salamu hizo kutolewa, mwili wa Dk. Mgimwa ulikabidhiwa kwa machifu wa kabila la Wahehe kwa ajili ya kuendelea na taratibu za maziko ya kimila chini ya Chifu Abdul Sapi Adam Mkwawa, akisaidiwa na machifu wengine saba. Kwa mujibu wa taratibu za kabila la Wahehe, Dk. Mgimwa alipigiwa mizinga na kufanyiwa `range' ya jeshi la wazee wa mila baada ya kumaliza kuuhifadhi mwili wake kaburini na baadaye wazee kuhitimisha kazi yao kimila.

AACHA WOSIA MZITO
Mtoto wake wa mwisho wa kiume, Godfrey Mgimwa, alimweleza Rais Kikwete kwamba baba yake alimwagiza muda mfupi kabla ya kifo chake kwamba anaomba amsaidie kuwapigania wapiga kura wake ambao aliwaahidi kuwajengea mabweni ya wasichana na kuwapa bati 1,200. “Lakini pia aliniambia nikirudi Tanzania na nikifanikiwa kukutana na wewe, nikushukuru kwa kuniamini na kunipa uwaziri ambao umeipa heshima kubwa nchi yetu,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Kwanza mungu aiweke roho yake peponi.amin. hii inaonyesha kumbe kuna watu bado unaweza kuwamini kuwa viongozi.mwakyembe , nani mwingine watanzania wanaweza kujivunia.tafadhali waandike hapa iliwajue tuko nao.