1 Wathesalonike 5:18
Tuna kila sababu ya kumshukuru
Mungu wetu, kama Mtume Paulo anavyotukusha katika barua yake kwa 1 Wathe 5: 18. Kwanza, hatuna budi ya kumshukuru Mungu kwa kutusaidia kuumaliza Mwaka 2013. Pili, tuna sababu nyingi za kumshukuru Mungu
kwa kutuingiza katika Mwaka Mpya, 2014.
Haya yote ni mapenzi ya Mungu kwetu.
Katika Mwaka 2013, tuliweza kuuona Mkono wa Bwana katika mambo mengi;
kwa mfano, Mungu alitusadia kutimiza umri wa miaka minne katika Ibada ya
Kiswahili Columbus. Pili, 2013 tuliweza kuuona Wema wa Mungu pale Ibada ya
Kiswahili Columbus ilipofanikiwa kupata utambulisho rasmi ndani ya KANISA la Kiinjili
la Kilutheri hapa Marekani, kuanzia ngazi ya Sinodi mpaka makao makuu yake pale
Chicago. Kwa hakika, tuna kila sababu ya
kumshukuru Mungu wetu kwa mafanikio makubwa ndani ya Umoja wetu.
Vilevile, katika Mwaka 2013 tuliweza kupata baraka ya
ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadhamini wetu, ambao ni kanisa la Gethsemane na kanisa la
Ascension. Kupitia kwa watumishi wa
Mungu, Mchungaji June Wilknis na Mchungaji Tim Miller, tulifanikiwa kupata
huduma mbalimahali; kwa mfano mahali pa
kuabudia, huduma ya mpiga kinanda, na huduma nyingine muhimu bila ya matatizo yoyote. Vilevile, tulifanikiwa kupata huduma za
kiroho, kimwili na kijamii pale tulipokuwa na mahitaji ndani ya Ibada ya
Kiswahili na ndani ya jumuiya yetu kwa ujumla.
Kwa hakika, tuliweza kuuona Mkono wa Mungu ukiwa katikati yetu. Mwaka 2013, ulizidi kuwa ni mwaka wa baraka
kwetu pale Mungu alipotupatia huduma za kiuchungaji kwa karibu zaidi kupitia mtushi wake,
Mchungaji Ipyana Mwakabonga. Tuliipotazama
NEEMA ya BWANA katika mambo haya yote, tuliweza kufungua vinywa vyetu na kumshukuru
Mungu wetu, “Pamoja na Kwa Umoja” tulisema
Mungu wetu ndiye EBENEZA ndani ya Umoja wetu.
Wapendwa katika Kristo, Mkono wa
Bwana umetusaidia kuuona Mwaka Mpya, 2014.
Pamoja na kuendelea kutoa shukrani zetu kwa Mungu wetu aliyetutoa mbali
na kutufikisha katika Mwaka 2014, tunamuomba kila mmoja wetu aendelee kuumbea
UMOJA wetu pamoja na huduma ya Ibada Ya Kiswahili Columbus. Karibuni tuitangaze Habari hii Njema ,“Pamoja
na kwa Umoja,” Habari Njema ambayo Mungu
ametutendea ndani ya JUMUIYA yetu. Habari
Njema iletayo furaha pale penye huzuni. Pamoja na kwa Umoja tuwe NURU ndani na nje ya
jumuiya yetu . Nuru iletayo Mwanga.
Mwanga wenye kuleta matumaini mema kwa watoto wa Mungu. Haya yote yatawezekana
kwa IMANI , kama tunavyokumbushwa na nabii Jeremia, “ … nitakuonyesha mambo
makubwa, magumu usiyoyajua.” Yer.33:3.
Mwisho, tunamuomba kila mmoja wetu
awe huru kutoa maoni au ushauri utakaoiboresha
huduma ya “Ibada Ya Kiswahili Columbus” katika Mwaka 2014. Karibuni sana ili tuweze kuujenga Mwili
Kristo, “Pamoja na kwa Umoja” kwa njia ya vipawa vyetu au karama zetu ambazo
Mungu amembariki kila mmoja wetu. Mtunzi wa Zaburi ya 133, anatukumbusha ujumbe
ufuatao: …..Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, na kwa
umoja. Wapendwa katika Kristo
Yesu, Mungu wetu anatupa mwaliko wa kuuanza Mwaka 2014 tukiwa “Pamoja na kwa
Umoja” na Mungu wetu. Mwaka 2014 na uwe
mwaka wetu “PAMOJA NA KWA UMOJA.” AMEN.
No comments:
Post a Comment