
Dar es Salaam. Uongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), umesema Yanga itake isitake AzamTV itarusha mechi zote na kama hawataki ni bora wakajitoa kwenye Ligi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmad Yahaya akijibu azimio lililofikiwa na viongozi na wanachama wa Yanga wa kugomea AzamTV kuonyesha mechi zake.
Yahaya alisema Yanga hawana haki ya Televisheni za Ligi Kuu mwenye haki hizo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Haki za Televisheni za Yanga wanazo wenyewe wala sisi hatujawaingilia, wanauamuzi wao kama watauza haki hizo kwenye mechi zao za kirafiki, mechi za kimataifa hilo ni jukumu lao wala sisi halituhusu.
“Lakini haki za Ligi Kuu ni za TFF, Ligi Kuu ni mali ya TFF ambayo Bodi inasimamia, na Yanga itaheshimu misingi, kanuni, na maelekezo yote yanayotolewa na TFF, Azam imeingia mkataba na TFF kupitia Bodi ya Ligi ambao ndio wasimamizi, Yanga hawana haki yoyote ya kukataa mechi zao zisionyeshwe na AzamTV.
“Wao Yanga kama hawataki AzamTV iwatangaze basi ijitoe kwenye ligi sisi hatutawatangaza, lakini madhali wapo kwenye ligi basi mechi zao zitaonyeshwa na huo ni msimamo wa Bodi na Serikali,” alisisitiza
Yahaya alisema kuwa fedha za Yanga Sh75 milioni ambazo wamezisusa bado zipo kwenye akaunti ya Ligi Kuu na iwapo muda wowote wakiziitaji watapatiwa fedha hizo.
Kauli ya Yahaya imekuja siku chache baada ya Yanga kuzungumzia suala la mkataba wa AzamTV kwenye mkutano wao mkuu na wanachama kuwataka viongozi wao kuwapeleka mahakamani Azam kwa kukiuka agizo la Yanga la kutaa mechi zao za Ligi kuonyeshwa live na kampuni hiyo.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusufu Manji alitoa mchanganuo wa udhamini huo kwa kusema “Azam wanataka kuonyesha mechi zetu kwa Sh100 milioni, kwa mechi 26 tunazocheza ligi nzima hiyo ni sawa na Sh3 milioni kwa kila mechi, kwa mechi yetu moja tunapata zaidi ya Sh3 milioni na ile inayotukutanisha na Simba tunaingiza zaidi ya Sh100 milioni na kuhoji wanachama wake udhamini huo ni halali au siyo halali ambapo kwa pamoja waliukataa kwa kile walichoeleza siyo halali na kutaka Azam wapelekwe mahakamani.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga akizungumzia suala hilo mara baada ya mkutano huo alisema, “Kuna kampuni ambayo tumeingia nayo mkataba SGM ya Kenya kwa ajili ya kuonyesha mechi yetu ya raundi ya kwanza dhidi ya Al Ahly ya Misri, kampuni hii kwa mechi moja tu inatupa Dola 55,000 (sawa na Sh90 milioni).
“Tulikubaliana na Azam TV wao wabaki na kipindi cha Yanga Soccer Show, sisi tuendelee na Haki zetu za Televisheni na Zuku, lakini yaliyotokea hapa katikati yanajulikana,” alisema.
“Wanachama wameamua tuwapeleke mahakamani AzamTV, lakini sisi kama viongozi tutakaa na uongozi mpya wa TFF, na wanasheria wetu kuangalia upya suala hili, milango bado ipo wazi kwa Azam kukaa meza moja na sisi.”alisema Sanga.
Naye Mwenyekiti wa AzamTV, ambaye ni Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Mohamed Said akizungumzia suala hilo alisema Azam haijaingia mkataba na Yanga, imeingia mkataba na TFF na hakuna makubaliano yoyote yaliyokuwepo kati ya Azam na Yanga. “Siku zile Serikali iliposema tukutane yeye Sanga alikuja na tukaongea naye, lakini alishindwa kutoa uamuzi na kusema mpaka Manji awepo na kikao kingine kilimhusisha Manji alikataa akasema hataki kusikia habari za AzamTV.”
Mwananchi
1 comment:
Huu ni ubabe wa wazi kwa timu zetu za Tanzania ukizingatia maamuzi yanatolewa bila wao kusikilizwa. Kuna conflict of interest kwa huyu makamu mwenyekiti wa bodi ya ligi ambaye pia ni mwenyekiti wa Azam. Haya ni mazingaombwe kwa watanzania wote wapenda michezo. Timu zote zionyeshe msimamo kwenye hili kwani kelele za mmoja hazitamzuia mlaji.....
Post a Comment