ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 25, 2014

Wapinga milioni 15/- kutumika kwa mabango ya Ukimwi

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, wamepinga uongozi wa halmashauri hiyo kutengewa Sh.milioni 15 katika bajeti ya mwaka 2014/2015 kwa ajili ya kutengenezea mabango kupiga vita ugonjwa wa Ukimwi wilayani humo.

Madiwani hao wamefikia hatua hiyo baada ya Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Juma Abeid kusoma bajeti na kukuta Idara ya Ukimwi, imetengewa kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutengeneza mabango sita.

Diwani wa Kata ya Mkamba (CCM), Hassan Dunda, alisema mabango hayo gharama yake ni kubwa ikilinganishwa na fedha zilizotengwa.


"Yaani itumike milioni 15 kwa ajili ya kutengeneza mabango sita! Wakati huu ugonjwa upo kila eneo, kwa nini yasitengenezwe mabango mengi na kusambazwa kwenye vijiji vyote vya wilaya hii kwa gharama hiyo hiyo iliyotengwa kuliko hayo mabango sita, Je hayo mabango sita yanawekwa maeneo gani,'' alihoji.

Mratibu wa Ukimwi wa wilaya hiyo, Jully Swai, alisema mabango hayo yatawekwa katika maeneo ya Vikindu, Kisiju na Mkuranga mjini.

"Tunataka kutengeneza mabango ya kisasa kama ya Wakala wa Barabara (Tanroads) na siyo ya vitambaa kwani watu wengi wameathirika na Ukimwi na hasa kata ya Vikindu," alisema Swai na kuendelea:

"Tunatarajia kuweka mabango mawili, Kisiju nako kuna maambukizi ya Ukimwi nako tutaweka mabango mawili na Mkuranga mjini tutaweka mabango mawili."

Hata hivyo, baadhi ya madiwani walipinga kuwekwa mabango maeneo ya mjini pekee na kushindwa kuweka vijijini, kwa madai kwamba jamii inatakiwa kupewa elimu juu ya maambukizi ya Ukimwi ili waweze kuitumia kwa kujikinga.

Walisema Ukimwi upo maeneo mengi na siyo njia zenye lami tu, hivyo inatakiwa mabango yapelekwe mpaka vijijini na sio mjini tu na ikiwezekana hata mabango ya vitambaa yatumike ili wananchi wote waweze kujua elimu ya ukimwi, kwani ukimwi haupo mjini pekee.

Swai, alisema kuwa suala hilo wataliangalia na kwamba elimu ya Ukimwi itaendelea kutolewa kila eneo na sio kuwekwa mabango hayo tu.

Wakati huo huo, baraza hilo limepitisha bajeti ya halmashauri hiyo ya Sh.bilioni 29 kwa ajili ya kuboresha miradi ya maendeleo sambambana na mishahara.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: