ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 25, 2014

MWENZI WAKO ANAKULIZA, UNAMLIZA?

MAUMIVU ya mapenzi yanatesa, yanaumiza na kutoa machozi. Kwa hakika mapenzi yanaliza! Ili maisha yako ya kiuhusiano yawe mazuri, unatakiwa kuhakikisha unakuwa makini na kukaa mbali na maudhi.
Wengi ninaokutana nao kwa ajili ya ushauri ofisini kwetu, huwa wanazungumzia zaidi namna wanavyonyanyaswa na wenzi wao. Hata wale wanaonitumia meseji, wanalilia mateso ya moyo.

Ndugu zangu, inawezekana umeumizwa sana na mapenzi; huenda mpenzi wako haeleweki na maneno yake yanakera sana, yanakutesa na kukupa picha mbaya ya uhusiano wenu.

Hata kwa upande wa wanandoa, wapo walio kwenye mateso makubwa. Ni vilio na machozi kila kukicha. Labda umeolewa, mumeo ana maudhi ya kila siku. Anachelewa kurudi nyumbani, amekuwa mlevi kupindukia, hakupi kipaumbele na mara nyingi anakuwa zaidi na kampani yake kuliko kukufikiria wewe.

Kuna vitu vingi sana ambavyo huchangia mateso katika mapenzi. Hata hivyo kuwa kwenye kipindi hicho, hakukupi fursa ya kulia muda wote. Machozi yako hayatakuwa na maana ikiwa hujajua kitu cha kufanya ili kurudisha furaha iliyopotea.

Rafiki zangu, juhudi za kusaka amani katika uhusiano isiwe upande mmoja tu. Usingoje mpaka mwenzako aamue kubadilika mwenyewe. Lazima ujiulize, kwa nini amebadilika na utafanyaje kumrudisha kwenye mstari?

WEWE UNAISHIJE?
Usikubali kuyaacha mambo yajiendee yenyewe. Tafuta suluhu haraka. Kuwaambia rafiki zako juu ya udhaifu wa mwenzako hakutakusaidia sana; kutoa siri zenu za ndani na kuwasimulia ndugu zako hakuna maana yoyote.

Wengine watakucheka na si ajabu watakuwa wanafurahi ndoa/uhusiano wako kuharibika. Maisha ni yako wewe na mwenzako. Huwezi jua kilichomo ndani ya mtu.

Si ajabu mwingine anamvizia mpenzi wako muda mrefu, kueleza udhaifu au matatizo yaliyopo kwenye uhusiano wenu ni kumpa mbinu za kujipanga namna ya kumchukua kwa urahisi zaidi.

Hapa chini tutajifunza zaidi, lakini jambo la msingi zaidi kwako unalotakiwa kufanya ni kwamba, usikubali kukaa na matatizo kwenye uhusiano wako. Usibaki kusubiri muujiza utokee bila juhudi zako. Lazima usugue ubongo ili kuhakikisha amani inarudi.

JICHUNGUZE!
Hebu jichunguze, maisha yako yanampendeza mwenzi wako? Angalia nyendo zako. Unaishi na mwenzako kimapenzi au unamburuza mradi siku zinakwenda? Inawezekana una mpenzi mwingine nje ya mwenzako na unaamini huko unapata furaha zaidi, unajidanganya!

Hakuna cha maana huko nje rafiki yangu. Ikiwa utafanya sarakasi zako zote halafu mwisho wake unarudi nyumba ambapo hakuna amani, kuna faida gani?

Acha kumliza mwenzako, maisha yanahitaji uvumilivu, kupendana na kuchukuliana matatizo. Inawezekana leo unamuona ana kasoro nyingi, zamani zilikwenda wapi? Hakuna mkamilifu duniani.
Wiki ijayo nitakuwa hapa kuhitimisha mada yetu, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: