ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 17, 2014

Rais Kikwete amwaga mamilioni Simba


Na Hans Mloli wa GPL
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amemkabidhi hundi ya Sh milioni 30 mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage kama mchango wake kwenye harakati za ujenzi wa uwanja mpya wa klabu hiyo uliopo Bunju, Dar.

Rage aliweka bayana mchango wa rais huyo mbele ya waandishi wa habari jana Jumapili mara baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Katiba wa Simba uliofanyika kwenye Ukumbi wa Maofisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar.

Aidha, Rage alisema kwamba Kikwete aliamua kutoa mchango wake huo baada ya kumtaarifu kuwa bado wanahangaikia hati ya uwanja wao wa Bunju ambao utagharimu takribani Sh milioni 150.
“Kabla sijafika kwenye mkutano, leo asubuhi nilionana na Rais Kikwete nikazungumza naye kuhusu harakati zetu za kupata hati ya uwanja wa Bunju kutoka wizarani na kwamba inahitajika milioni 150 kwa ajili ya kufanikisha hilo.

“Akanikabidhi hundi ya shilingi milioni 30 kama mchango wake kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo na kuahidi kusimamia mpaka tunapata hiyo hati kutoka wizarani, kwa kweli kutokana na hiki alichokionyesha rais kwetu Simba inadhihirisha kabisa kwamba rais ni mpenzi wa timu zote hapa nchini na si wa timu moja kama watu wanavyosema,” alisema Rage.

Wakati huohuo, Rage pia alitangaza kuingia mkataba wa milioni 150 na Benki ya Posta ikiwa ni moja ya njia ya kupata fedha kwa ajili ya hati ya uwanja.

Alisema kwamba benki hiyo itatoa kadi maalum kwa wanachama wa Simba na wateja wa Benki ya Posta zitakazojulikana kwa jina la Simba Fan ikiwa na faida ya kutumika kama ATM kadi na itauzwa kwa shilingi 5,000.

“Wanachama wataweza kuchangia moja kwa moja klabu yao kwa kujiunga na kadi za Simba Fan kutoka Benki ya Posta ambapo hiyo kadi pia itatumika kama ATM kadi yako.
“Kadi inapatikana kwa shilingi 5,000 na katika kiasi hicho shilingi 3,000 itakwenda moja kwa moja kwenye mchango wa Simba, tayari kiongozi wa Posta yupo Ulaya anashughulikia upatikanaji wa kadi hizo,” alisema Rage.

No comments: