ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 23, 2014

Utega yatishia kumshtaki Makamba

Mbunge wa Bumbuli (CCM) January Makamba

Umoja wa Wakulima wa Chai Usambara (Utega) wa mkoani Tanga, umetishia kumburuza mahakamani Mbunge wa Bumbuli (CCM) January Makamba, kwa madai ya kufunga kiwanda cha kusindika chai cha Mponde.

Mwenyekiti wa umoja huo, William Shelukindo, katika taarifa kwa vyombo vya habari alisema, uamuzi huo wa kumshitaki umefikiwa na mkutano maalum wa UTEGA uliofanyika juzi mjini Bumbuli.

Makamba, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknelojia, anashitakiwa kwa madai ya kuitisha mkutano wa hadhara mwaka jana na kutoa maazimio ya kufungwa kwa kiwanda cha kusindika chai cha Mponde Tea Estates kinyume cha sheria.

Kwa upande wake Makamba alisisitiza kuwa ataendelea kutetea wakulima wa chai wa jimbo hilo kwasababu anaamini kwa muda mrefu wamekuwa hawanufaiki kuwepo kwa kiwanda hicho.

Shelukindo alisema kwa mwaka mmoja tangu kiwanda kifungwe, jitihada mbalimbali zimechukuliwa za kukinusuru zikiwamo kufanya kikao na kamati ya siasa ya CCCM mkoa wa Tanga lakini imeshindikana.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa walifanya kikao kingine kati ya uongozi wa Utegi , Msajili wa Hazina, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Mali za Serikali Zilizouzwa (CHC) Consolidated Holdings pia bila mafanikio.

Akifafanua, Shelukindo alisema kuwa kikao kilibainisha wazi kwamba suala la Mponde ni la kisheria kwa vile kiwanda pamoja na shamba la Sakare viliuzwa na serikali kwa Utegi na hakuna upande wowote wenye tatizo na umoja huo.

Katika mkutano huo,wajumbe kwa pamoja walitoa tamko la kulaani kitendo cha kufungwa kiwanda na kukisababishia hasara, gharama kubwa na malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi.

Waliiagiza kampuni ya chai ya Mponde iende mahakama kupata kibali cha kufungua kiwanda ili wakulima wasiendelee kuteseka.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: