ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 23, 2014

Kikwete ametimiza wajibu, asipuuzwe

Juzi Rais Jakaya Kikwete alilihutubia Bunge Maalum la Katiba na kuzungumzia mambo kadha wa kadha yanayohusiana na katiba inayosubiriwa kwa hamu na Watanzania.

Ilikuwa hotuba ndefu, iliyosheheni mambo mengi ya msingi na ambayo kwa upande wetu, tunaamini kwamba yanapaswa kuwa moja ya mapitio katika hatua zilizobaki katika kuifikia Katiba Mpya.

Tutambua kwamba ipo mitazamo tofauti, zipo dhana na nadharia tofauti pale masuala ya Katiba Mpya yanapojadiliwa. Lakini tujue kuwa mwisho wa siku kinachoandaliwa ni kwa mustakabali wa taifa letu Tanzania.

Hatuna shaka kwamba hotuba ya Rais Kikwete, ilijengwa katika maeneo ambayo, kwanza, yalijikita katika uelimishaji jamii kuhusu umuhimu wake (Katiba Mpya) kwa nchi na watu wake.

Pili, ilielimisha kuhusu maeneo yanayojenga hisia ambayo kwamba, ikiwa hayataangaliwa kwa makini na mtizamo mpana kisha kupatiwa ufumbuzi, basi upatikanaji wa Katiba Mpya ni jambo lisilowezekana. Hayo ni mambo yanayojumuisha pia yaliyo maarufu kama ‘kero za Muungano’.

Na kwa namna ya tatu, tunaitafsiri hotuba ya Rais Kikwete kuwa kielelezo cha kauli za hekima na busara kuhusu ulipotokea Muungano, ulipo na unapopaswa kuwa, ili taifa liendelee kuwa moja, lenye watu wenye mtizamo mmoja kwa maslahi kwa wote.

Tunapoitathimini hotuba ya Rais Kikwete, jawabu linaloweza kujumuisha maeneo matatu, miongoni mwa aliyoyazungumza ni kwamba alijiweka katika uwazi na ukweli, ili wajumbe wa Bunge hilo na wananchi wakishindwa kuyaelewa, kuyatafakari na kuyafanyia uamuzi sahihi, lawana na zisielekezwe kwake.

Kwa muda mrefu sasa, mwenendo wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba unaonyesha kuwapo misimamo ya kitaasisi, mathalani vyama vya siasa, pasipo wenye kuiendeleza misimamo hiyo kutowasilisha sababu ama hoja za msingi zinazowaaminisha kuwa hivyo.

Hali hiyo imekuwa chanzo cha mgawanyiko hata katika kujadili masuala yanayolihusu taifa, yakiwa nje ya maslahi ya vyama ama taasisi zinazowakilishwa ndani ya Bunge hilo.

Ndio maana, tumeridhishwa na tunaiunga mkono hotuba ya Rais Kikwete, ambayo kimsingi, haikuishia tu katika kutahadharisha, kuonya ama kukaripia, bali ilienda mbele zaidi na kutoa mapendekezo na ushauri wa namna bora ya kuiwezesha Tanzania kuwa na Katiba Mpya yenye maslahi kwa umma.

Maslahi ya umma yaliyosisitizwa na Rais Kikwete ni pamoja na umuhimu kwa Katiba Mpya kupewa mianya ya kuruhusu mfumo wa Muungano usiokuwa na madhara ya sasa au baadaye kwa raia wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar zilizoungana Aprili 26, 1964.

Suala la muundo wa serikali tatu lililopendekezwa katika Rasimu ya Pili ya katiba, limekuwa mwiba katika nyoyo za wengi ijapokuwa katika hotuba ya Rais amelitolea ufafanuzi kwa kuainisha udhaifu wake ikiwa ni pamoja na kile alichosema Serikali ya Muungano inayopendekezwa haina vyanzo vya mapato vya kuiendesha kwa sababu hata ushuru wa bidhaa unaopendekezwa siyo wa uhakika.

Kwa mantiki hiyo yaweza kudumu kwa muda tu kisha kuporomoka kwa sababu itakuwa tegemezi kwa kuwa imekabidhiwa majeshi na hivyo kuwa hatarini kuangushwa na jeshi baada ya kushindwa kuwalipa mishahara.

Lingine alilotaja ni kwamba serikali hiyo ya muungano haina mamlaka kushurutisha nchi washirika na isitoshe takwimu za wanaotaka serikali tatu katika rasimu zina walakini.

Rais ametoa tahadhari mbalimbali katika hotuba hiyo ili kuwapa taswira wajumbe Bunge la Katiba kutafakari na kupima, kisha kujipanga vema katika kuichambua rasimu, hatimaye kupata katiba isiyo na madhara kwa taifa letu.

Inawezekana baadhi ya sehemu ya hotuba yake isikubalike kutokana na tofauti za kiitikadi kwa wawakilishi wa wajumbe wa Bunge hilo, lakini ni vizuri ikatiliwa mkazo kwamba katika mambo yenye manufaa kwa nchi na watu wake, wote wanapaswa ‘kutembea njia moja’ kwani kosa moja leo, linaweza kuwa madhara kwa vizazi vingi vijavyo. Ni wapi maji yaliyomwagika yakazoleka na kubaki ujazo ule ule?

Yawezekana kwa mtizamo wa wengine wakaona aliyoeleza Rais ni vitisho, lakini mwelewa atayatafakari mara mbili mbili na kisha kuuona ukweli ulioko nyuma ya pazia.
Hata hivyo, tunaamini penye wengi hapaharibiki neno.

Wajumbe wa Bunge la Katika ni watu makini walioteuliwa kwa kuaminiwa na Watanzania waiweke mezani rasimu hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Mstaafu, Sinde Warioba kwa umahiri mkubwa, ili ijadiliwe kipengele baada ya kipengele, lengo likiwa ni kupata katiba mpya iliyo bora kwa mustakabali wa nchi yetu. Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: