Unyanyasaji huo uliibuliwa kwenye kikao cha uongozi wa shule ya Mchangani anakosoma mtoto huyo (jina linahifadhiwa), kilichohusisha asasi ya utetezi wa haki na usawa kijinsia (Gewe) pamoja na wazazi wake.
Mkutano huo ulifanyika shuleni hapo wiki hii na wazazi hao walikubaliana binti huyo mwanafunzi wa darasa la tatu, mwenye umri wa miaka nane aishi na baba yake.
Akiibua tuhuma, mwalimu wa binti huyo, Gaudensia Donatus, alisema alilazimika kumchukua na kuishi naye kwa siku nne baada ya Sabrina kutishia kumuua.
Aliwaambia wajumbe kuwa wiki iliyopita mtuhumiwa alifika shuleni hapo akiwa na mwanae akifoka kuwa anamtafuta Denis, mwanafunzi wa Mchangani aliyemtuhumu kuwa kila mara anachafua shati la binti yake kwa wino.
“Aliingia shuleni bila kufuata utaratibu akitoa maneno makali akiwa amempiga mwanae na kueleza kuwa anamtaka Denis amchape pia,” alisema mwalimu huyo na kuongeza kuwa alikataa kutii maelekezo huku akitishia kumuua mtoto wake.
Hata hivyo, alisema kutokana na hali hiyo, iliwalazimu kumnyang’anya mtoto ili kuokoa maisha yake na baadaye alipelekwa kwa shangazi yake mkazi wa Upanga na kumjulisha kilichotokea.
Alisema alipoelezwa kuhusu wifi yake, alidai amechoshwa na vitendo vya mama huyo kwani alishawahi kumchukua mtoto huyo na kuwafanyia vurugu nyumbani kwake.
Alisema madhumuni ya kumchukua mtoto huyo ni kuhakikisha anakuwa kwenye mazingira salama.
Mwakilishi wa Gewe, Asha Said alisema kuna haja ya mtoto huyo kuulizwa iwapo anataka kuishi na baba yake au anapendelea kuishi na mama.
Kwa upande wa baba mzazi Constant Saiboko, alikiambia kikao hicho kuwa yupo tayari kumchukua mtoto wake na kumtafutia shule nyingine ya bweni na hakubaliani na mateso yake.
Alieleza kuwa anafahamu anavyoteseka na aliwahi kumhamishia kwa shangazi yake lakini mama huyo alikwenda kumfanyia vurugu jambo ambalo hataki kuona likijitokea tena.
Sabrina alisema hayupo tayari kumtoa mwanae kwa kuwa anajua hatamuona tena katika maisha yake lakini akataka kulipwa Sh 500,000 ili amkabidhi kwa mzazi mwenzake.
“Endapo nitapatiwa 500,000 nipo tayari kumuachia mtoto huyo na fedha hizo zitakuwa ni kama fidia ya kumlea,”alisema na Saiboko aliahidi kuitoa fidia hiyo Julai mwaka huu kwani kwa sasa hana fedha hizo.
Mkuu wa shule ya Mchangani, Janester Emilly, alikubaliana na maamuzi yaliyofanywa na kuahidi kuwa atayasimamia ili kumuokoa mtoto huyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment