Advertisements

Monday, April 21, 2014

Bunge la Bajeti kuendeshwa ‘fasta fasta’

Dar es Salaam. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujadili Bajeti ya Serikali 2013/14 linatarajiwa kuanza Mei 6, mwaka huu huku likiwa limetengewa siku chache ambazo zitasababisha liendeshwe kwa kasi ili kukamilisha shughuli zake.
Utaratibu wa sasa unalilazimisha Bunge hilo kuwa limefanya uamuzi wake (kupitisha au kutokupitisha), Bajeti ya Serikali pamoja na Sheria za Fedha ifikapo mwishoni mwa Juni kila mwaka, ili kuruhusu utekelezaji wa bajeti husika kuanza Julai Mosi, siku ya kwanza ya mwaka mpya wa fedha.
Ratiba ya Bunge hilo ambayo tayari imepata idhini ya Kamati ya Uongozi iliyokutana Alhamisi iliyopita, inaonyesha kuwa Bunge la Bajeti litakutana kwa siku 52, zikiwa ni pungufu kwa siku 28 au wiki nne, ikilinganishwa na mkutano kama huo mwaka jana.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alikiri kupunguzwa kwa siku za Bunge la Bajeti akisema hali hiyo inatokana na uchache wa siku pamoja na utaratibu mpya wa kuhakikisha bajeti inapitishwa mapema ili ianze kutekelezwa Julai Mosi.
“Kamati ya Uongozi haikuwa na njia nyingine zaidi ya kuminya siku ili kukimbizana na muda uliopo, hivyo ni kweli siku zimepungua, lakini hatukuwa na jinsi maana tunatakiwa tumamalize shughuli za bajeti mwishoni mwa Juni,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Kama mnavyofahamu, siku nyingi zimetumika kwenye Bunge Maalumu la Katiba, kwa hiyo hizo zilizobaki ndizo tulizozipangia kazi nyingi zilizopo na hata ukiangalia wakati wa bajeti huwa kamati zinakutana kwa wiki tatu, lakini tumewapa wiki moja tu.”
Mkutano wa 11 wa Bunge ambao ulijadili Bajeti ya 2013/14, ulitumia siku 80, ukifanyika kuanzia Aprili 9 hadi Juni 28, 2013 lakini zamu hii Bunge la Bajeti hadi litakapoahirishwa Juni 27, litakuwa limekutana kwa siku 52.
Kuchelewa kuanza kwa Bunge la Bajeti kumesababishwa na Bunge Maalumu la Katiba ambalo linahitimisha ngwe yake ya kwanza Ijumaa wiki hii, likiwa limekutana kwa siku 67. Bunge la Katiba linawajumuisha wabunge wa Bunge la Jamhuri na wale wa Baraza la Wawakilishi.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema tayari Kamati ya Uongozi imepitisha ratiba husika na kwamba mkutano huo wa 15 utatanguliwa na Kamati za Bunge zitakazokutana Dar es Salaam kwa siku tano tu, kuanzia Aprili 28, mwaka huu kabla ya wabunge kusafiri kwenda Dodoma Mei 5.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema licha ya kuwapo kwa shughuli za Bunge Maalumu la Katiba, Serikali iko tayari kwa bajeti zote za wizara pamoja na Bajeti Kuu.
“Sisi serikalini kwa jumla tuko tayari maana wakati mawaziri wakiendelea na Bunge Maalumu, wataalamu walikuwa wakiendelea na maandalizi na kimsingi, kila kitu kiko kama kinavyotakiwa kuwa, kuanzia tutakapohitajika mbele ya kamati (za Bunge) hadi bungeni kwenyewe,” alisema Lukuvi.
Athari kwenye mijadala
Uchache wa siku hizo, umesababisha kupungua kwa siku 13 za mjadala katika wizara ambazo kutokana na umuhimu wake, mwaka jana zilitengewa siku zaidi ya moja kwa ajili ya kuwapa wabunge nafasi ya kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo ya marekebisho.
Miongoni mwake ni Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo chini yake zipo wizara za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sera, Uratibu na Bunge pamoja na Uwekezaji na Uwezeshaji ambazo kwa pamoja zitajadiliwa kwa siku tatu tu, badala ya tano zilizotengwa mwaka jana.
Wizara ya Maji ambayo mwaka jana ilipewa siku tatu, mwaka huu imetengewa siku moja, sawa na wizara nyingine 10 ambazo mwaka jana zilitengewa siku mbili.
Wizara hizo ni pamoja na Ofisi ya Rais, ambayo inasimamia Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Uhusiano na Uratibu na Makamu wa Rais inayosimamia Muungano na Mazingira.
Nyingine zilizoathiriwa na utaratibu huo ni Kilimo, Chakula na Ushirika, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani ya Nchi; Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ujenzi; Uchukuzi; Afya na Ustawi wa Jamii; Nishati na Madini; Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa, Dk Hamis Kigwangalla alisema: “Sisi tunalazimika kuomba siku za ziada ili tuweze kutekeleza wajibu wetu vizuri, fikiria kamati yangu inasimamia mikoa 25 kwa maana hiyo kwa siku tano tulizopewa ina maana siku moja tupitie bajeti za mikoa mitano.”
Aliongeza: “Katika hali hii ni ngumu sana, la sivyo tutakuwa rubber stamp (muhuri) kwenye mapendekezo, hivyo tumeomba tuanze mapema kabla ya kamati nyingine na tumekubaliana na wajumbe wangu ikiwezekana tufanye kazi hadi usiku wa manane ili tuweze kukamilisha kwa wakati.”
Alisema ugumu wa kazi katika kamati yake unatokana na kusimamia matumizi ya mikoa ambayo ni zaidi ya Sh4.3 trilioni, kiasi ambacho kinakaribia kufikia theluthi moja ya bajeti nzima ya Serikali.
“Tukirashiarashia tu kwa fedha nyingi namna hii, tunaweza kujikuta tumepitisha madudu mengi na kusababishia taifa hasara ya kiasi kikubwa cha fedha,” alisema.
Bajeti Kuu
Hata hivyo, siku za mjadala kwa ajili ya bajeti kuu zimebaki saba kama ilivyokuwa katika mkutano wa 11 mwaka jana. Dk Kashililah alisema Bajeti Kuu ya Serikali itawasilishwa bungeni Juni 12 saa 10:00 alasiri na itatanguliwa na taarifa ya hali ya uchumi itakayosomwa asubuhi.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mjadala wa bajeti utafanyika kati ya Juni 16 na 24 na kufuatiwa na upitishwaji wa miswada ya Sheria ya Fedha na ule wa matumizi.
Dk Kashililah alisema kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu, umetengwa muda wa ushauriano baina ya Serikali na Bunge kupitia Kamati ya Bajeti ili kuzingatia hoja zenye masilahi kwa taifa katika majumuisho ya bajeti husika.
Mwananchi

No comments: