CCM CALIFORNIA
YATOA MAELEZO YA KINA KUHUSU UMUHIMU WA
URAIA PACHA KATIKA HARAKATI ZA KULISUKUMA SUALA HILI LIPITISHWE KATIKA BUNGE LA
KATIBA
Kutokana
na juhudi za Chama chetu na serikali yetu kuona umuhimu wa kutusikiliza sisi
tunaoishi nje ya nchi, na pia tume ya katiba kusikiliza ombi la chama chetu
kulirudisha hili suala katika rasimu ya pili ya katiba; ni kwa njia hiyo basi
tumelazimika kulitolea ufafanuzi katika njia halali za kutoa ushawishi kwa waheshimiwa
wabunge wa katiba kulielewa hili suala lenye umuhimu sana katika nchi yetu na
watu wake katika nyanja mbalimbali.
Juu ya
hilo, pia tuko pamoja na Rais wetu ambaye pia ni mwenyekiti wetu wa chama cha Mapinduzi
taifa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye ameendelea kuonyesha wazi nia ya
kutuunga mkono katika hili, pamoja na waziri wetu wa mambo ya nje Mheshimiwa
Bernad Membe. Na vile Mheshimiwa Mwiguru Nchemba Mb, Naibu Katibu Mkuu w CCM
Bara, pia Naibu Waziri wa fedha,
amesisitizia suala la uraia pacha juzi tu kwenye sherehe za Muungano hapo
Washington DC kuwa lina manufaa kwetu tulio na uraia wa nchi za nje na kwamba
Serikali ya CCM imelirudisha kwenye rasimu ili lifanyiwe kazi. Hivyo tuungane
na juhudi za viongozi wakuu wetu hawa kufanikisha zoezi hili.
Tunaomba
wabunge wetu waCCM na wawakilishi wengine wote mtusikilize na mtuunge mkono kwa
niaba ya Watanzania wote waishio nje ya nchi na wenye uraia wanchi nyingine.
Tunayo
machache ya kuelezea nia yetu nzuri ya kudai uraia wanchi mbili, yako mengi mno
lakini tuyaeleze machache hapa ili mpate mwanga mzuri wa kuona tuliposimamia
katika kulidai hili. Tuna matumaini makubwa sana mtakubaliana na sisi na
kulipitisha hili pindi mjadala uhusuyo hili jambo utakapowadia. Na pia
mkisaidiana na mwakilishi wetu aliyeko huko Ndugu Kadari Singo katika kupata
maelezo zaidi ya suala hili.
- 1. Uzalendo:Kuna Watanzania wengi tunaoishi nje ya nchi ambao ni tegemeo kwa nchi yetu.
· Sisi
Watanzania hatujaikimbia nchi wala kuikana nchi yetu. Bali tulikuja kwa nia
nzuri kabisa na tunajivunia Utanzania wetu katika nyanja na nia ya
kujiendeleza. Hivyo tunaona ni haki yetu kubakia kuwa raia wa kuzaliwa wa nchi
yetu.
· Watanzania
hawa ni nguvu kazi na wenye mapenzi sana na nchi yao, wanajivunia nchi yao kwa
kuzaliwa. Suala la kuomba uraia katika nchi nyingine halikuja vichwani mwetu
kwa ajili ya kuukana Utanzania wetu, La hasha! Suala hili limetokana na mazingira ya nchi za ugenini.
Ambapo usipokuwa na uraia wanchi hizi ni ngumu kupata kazi, elimu yenye gharama
nafuu, na hata uwezo wa kwenda nyumbani Tanzania kusalimia familia na ndugu
zetu au kuwekeza na kurudi tena katika nchi husika.
·
Watanzania
tunataabika kupoteza uraia wa kuzaliwa
kwasababu tu tumebahatika kupata uraia wanchi nyingine ili kuweza kupata elimu
katika fani mbalimbali, mfano katika huduma za kiafya, serikalini, viwandani,
mashuleni na sehemu nyingine nyingi ikiwemo kazi za kijiajiri ili kufanya kazi
katika mataifa tunayoishi ili kujipatia kipato kizuri na kusaidia familia zatu,
ndugu na marafiki walioko huko nyumbani. Hakuna ubaya wowote wa kufanya hivyo.
Tunadhani ni harakati nzuri za
kujikomboa kutoka kwenye janga la umaskini kama tutasaidia ndugu zetu walioko
nyumbani lakini zaidi tukipewa haki yetu
ya kuzaliwa katika kutimiza hayo.
- 2 Uchumi: Tukiruhusiwa kupata uraia wa nchi mbili tutakuwa nguzo kubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo huko nyumbani kusaidiana na juhudi za serikali katika kutekeleza na kuhamasisha maendeleo kwa njia mbalimbali za kisasa zilizojaa sayansi na teknologia. Tujue wazi na tukubali kuwa kwa wale waliobahatika kupata elimu zao katika nyanja mbalimbali kutoka vyuo, shule na mashirika mbalimbali ya huku nje ni wazi kwamba utaona ufahamu wako unavyoweza kurutubisha chachu ya maendeleo.
Tunaomba
tusihukumiwe na maneno haya kwamba labda tunadharau elimu inayotolewa na nchi
yetu; la hasha ila ni ukweli usiopingika kwamba nchi tajiri zina faida zake
katika kutoa elimu inayoendana na wakati wa sasa. Nchi yetu bado maskini na
inahitaji mchanganyiko wa mawazo tofauti kutoka watu wenye taaluma mbalimbali
ukiunganisha na za hawa tulioko huku nje kuweza kuchangia na kufanya kazi katika sehemu mbalimbali
nchini kwetu. Kwamfano:
I)
Utaalamu
katika vitengo mbalimbali kama vile:
·
Afya:
Katika kitengo hiki
cha afya tunaongelea wauguzi, madaktari, wanaradiolojia, wataalamu wa maabara,
wachunguzi na mambo menginemengi katika kitengo hiki. Mojawapo ya faida kubwa
sana inayoweza kuletwa na Watanzania walioko nje na kuwa raia wa nchi za nje ni
kutumia utaalamu wao walioupata nje kuendeleza vituo vya afya zikiwemo zahanati
na hospitali kubwa. Tunafahamu kuwa mojawapo ya vitu vinavyoturudisha nyuma ni
suala la afya za wananchi. Mwananchi anafika hospitali anakosa huduma
inayomstahili aidha kwa sababu ya uchache wa watoa huduma, uchelewashaji
wahuduma,ukosefu wa madawa au ubora wahuduma. Suala la afya katika nchi hizi
zilizoendelea zimepewa kipaumbele sana na kwa wale Watanzania waliobahatika
kupata elimu naujuzi nakutumikia katika hospitali za nchi hizi wamepata upeo
mkubwa sana wa jinsi ya kuwahudumia wagonjwa. Ni masikitiko makubwa kukosa
nafasi ya kuja kuchangia katika nchizao katika nyanja hiyo. Ukitaka kufanya hivyo
inakuwa ni mkataba kama mtu asiye Mtanzania wakati unafanya kazi katika nchi
yako na unawahudumia watu wako wakiwemo ndugu zako. Katika akili ya kifikra
jambo hilo linatesa sana.
·
Teknologia
za kisasa:
Kuna wahandisi(
engineers) katika nyanja mbalimbali, kwenye computer, umeme na nishati, ujenzi, utengenezaji zana
mbalimbali na mengine mengi. Kuna Watanzania wengi wako nje ya nchi na
wamebobea katika fani hizo na wako tayari kurudi nyumbani kufanya kazi katika
nchi yao na kusaidia nchi yao katika kile walichokipata huku, lakini sharti
hili la kutunyima uraia linatuzuia kutumiza ndoto hiyo.
·
Elimu
dunia :
Masuala kama
kuheshimu utu wa mtu na kuujali,
heshima za kazi, haki za kila mtu bila kujali chochote, ustaarabu, na
mengine, wazungu wanaita customer service,
au upande wa hospitalini wanaita patient
care, haya ni mambo ambayo Mtanzania anayeishi nje amefanikiwa sana kuyajua
na ni masuala muhimu ambayo yanaweza kurekebisha hali iliyopo nchini kwetu
katika tatizo hili ambalo limedondosha uchumi wetu kwa asilimia kubwa kutokana
na wafanyakazi katika vitengo mbalimbali kutokuwa makini, heshima na ustaarabu
katika kazi zao, kitu ambacho kinasababisha vyanzo vya rushwa. Tuna imani
Mtanzania aliyesukwa katika mazingira mazuri ya ugenini huku, akipewa nafasi ya
uraia wake na kuwezeshwa basi hiyo hali itaimarika kwa kiasi kikubwa
·
Taaluma
ya Elimu:
Watanzania wengine
waishio nje na wenye uraia wa nje ni wajuzi wa katika suala la ufundishaji.
Wapo wengi sana na wenye ujuzi tofauti wenye vipaji na elimu ya kutosha katika suala la
kuelimisha jamii na watu wetu. Kuna wengi kuanzia ngazi mbalimbali za
ufundishaji, kuna walimu wa watoto (kindergarten) kuna walimu wazuri tu wa
shule za msingi na sekondari mpaka vyuo vya kati na vyuo vikuu wenye elimu ya
kutosha. Hawa wakipewa nafasi ya kutoa mchango wao wa taaluma ya ufundishaji
katika nchi yetu, itakuwa ni jambo la busara sana.
Katika kitengo cha
Elimu tutakuwa tumefanikiwa sana hasa kuhusishwa utaalamu wa Watanzania wengine
ambao wameupata kutoka huku. Wengine wako tayari kuanzisha hata mashule yao.
Tunaomba tuwatimizie ndoto zao hizi za kuliendeleza taifa letu, na wenye
kujiona wamechangia katika kuleta maendeleo katika nchi yetu.
II)
Mikopo:
Tunaona sasa hivi
mashirika ya kifedha yanavyowezesha kutoa mikopo mizuri tu kwa Watanzania na
kuweka mazingira mazuri ya kurudisha mikopo. Maendeleo ya walio wengi nchini
kwa sasa yanaletwa na sheria zilizowekwa kwa kuruhusu mabenki kukopesha watu
ili kuanzisha vyanzo vya mapato yao, kujenga nyumba za kuishi, kusomesha watoto
wao na mengine mengi. Watanzania tulioko nje tumenyimwa nafasi hizo kwani hatuwezi kuwezeshwa mikopo
wakati tuko katika nafasi nzuri ya kukopa na kurudisha kutokana na masharti ya
benki. Shida kubwa ni kwamba hatuko pale kimwili hivyo hata ukitaka kutimiza
matakwa ya kibenki inakuwa ngumu kwamba lazima uwe na mali isiyohamishika na
vile vile niwepo pale kimwili kama raia. Sasa nitayafanyaje hayo nikiwa sio
raia? Maana hata kujenga au kumiliki ardhi, ndio tunajenga, au tunamiliki
tukiwa huku kwa kutumia ndugu zetu lakini tukiingilia vipengele vingine vya
ndani na tukagundulika tumejenga na huku hatuko raia tunaogopa na nyumba hizo
tutanyang’anywa au biashara tutafungiwa au tutawekewa masharti magumu mfano
riba, tax na mambo mengine ambayo yanatuweka katika wakati mgumu kujitoa wazi
na mali zetu huko nyumbani ili tupate mikopo hiyo.
Tukifunguliwa
mlango wa uraia pacha hii haitakuwa shida tena, tutakuwa wa wazi, tutapata
uhuru wa kukopa na kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ikiwa ni kuwezesha na
ndugu zetu huko na familia zetu huko. Ni
ukweli usiopingika kuwa uwezekaji umepamba moto katika kuleta maendeleo ya
haraka. Mwekezaji mwenye uraia wa kuzaliwa wa Tanzania ana masharti nafuu
katika kuwekeza kwani ni Mtanzania, lakini Mtanzania aliye na uraia wa nje ya
nchi naye pia anauganishwa kama mtu mgeni anayetaka kuwekeza katika nchi yake
ya kuzaliwa. Si haki kabisa na hili suala limetunyima maendeleo. Kuna Watanzania
wengi waishio nje ya nchi ambao sasa wana uraia wa nchi za ugenini wenye nia nzuri ya kuwekeza nyumbani, na wana
uwezo wao mkubwa wa kuwekeza, na wengine wana uwezo wa kati wa kuwekeza lakini
katika hali hii tuliyomo ya kutokuwa na uraia pacha, inatiwa wasiwasi kuwekeza
pesa zao nchini kwetu, wanazifungia mabenki tu na kufanya biashara ndongondogo
za nchi wanazoishi.
Hizi nchi za huku zimeishaendelea, sasakwa nini sisi Watanzania tuendelee kuwekekeza huku
na kuziendeleza hizi nchi wakati huko kwetu tunahitajika na uwezo tunao,
wakuwekeza huko kwetu kama Watanzania wa kuzaliwa? Tunaomba tuwekeeni mazingira
nafuu kwa kutupatia uraia pacha ili
ndoto hizi zitimilike.
III)
Mipakani
na viwanja vya ndege.
Kuna mengi hapa ya
kuorodhesha, lakini machache haya kuanzia yanaweza kutupa mwanga halisi,
machache tu ya ziada ni mihamgaiko ya njia za kuingia nchini mwetu, viwanja vya
ndege, bandari, mipakani, gharama kubwa anazolipishwa mgeni ambaye si raia wa
Tanzania. Sasa hata sisi Watanzania wa kuzaliwa ambaotumechukua uraia wa
ugenini hizi gharama zinatusulubu; Tunadhani huu ni unyanyasaji na uzalilishaji
wa hali ya juu ukizingatia haki ya mzawa.
IV)
Suala
jingine ni kuhusu vizazi vijavyo.
Watanzania wenye
uraia wanchi nyingine wana watoto waliozaliwa nje ya nchi. Hii nayo kwa
utaratibu wa sasa ni kwamba watoto hawa hawawezi kuwa raia wa Tanzania kwa
misingi hiyo hiyo kwamba wazazi wao si raia wa Tanzania, ingawa ni wazawa wa
Tanzania, lakini sheria zinakataa kuwapa uraia.
Tuna mategemeo
makubwa sana kwa watoto wetu kujua historia zao, vyanzo vya familia zao, upendo
wa nchi yao ambayo wazazi wao wamezaliwa. Hili ni tegemeo kubwa la mbeleni
pindi wanapofika umri wa kutambua na kujitegemea, daima hawataiona Tanzania kama
nchi ya kigeni, bali wataiona Tanzania kama nchi yao.
Sasa hivi tunapata
vigugumizi na aibu kuwaeleza watoto wetu kwetu ni wapi tulikozaliwa, maana
tunawaambia sisi ni sio raia wa Tanzania lakini tulizaliwa kule, ila sisi ni
raia wa hapa lakini hatukuzaliwa hapa. Watoto wanatuona sisi wazazi kama vile
wakimbizi tuliokimbia nchi yetu.
Watoto ndio vijana
wa kesho na ndio wazee wetu wa kesho pia. Tunawahitaji katika kuijua misingi ya
nchi yetu, na katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu huko baadae.
Hali ilivyo sasa
hivi ni kama wanabaguliwa kwa dhambi ile ile ya wazazi kuwa raia wananchi
nyingine hivyo kuondolewa sifa ya uzawa ndani ya nchi yao ya Tanzania.
Tunarudia kusema na
kuomba sana wajumbe wote waheshimiwa wabunge wa bunge la katiba, mlione hili suala kama suala la
kitaifa na si la kisiasa. Tunasikia mengi pia kutoka kwa wachache kuwa nia yetu
ni kuja kuchukua nafasi zao za kazi sio kuendeleza nchi. Tunataka kuliweka wazi
kabisa kwamba nia yetu ni njema. Sisi ni wazawa tunataka kushiriki katika
maendeleo ya nchi kama wazawa wengine. Ikitokea tukasidia sehemu fulani na
juhudi zetu zikatambuliwa na kuonekana, je hili swali kwamba tunakataka
kuchukua nafasi za wengine bado litaulizwa?. Tuna imani pia kuwa wale wenye
woga wa kuturuhusu basi hawaitendei mema
serikali yetu, maana wanainyima nafasi kubwa ya kuwezesha mchakato wa maendeleo
ambao uko wazi na hauna gharama.
Tuna hakika pia
kuwa wapo wengi miongoni mwa wabunge ambao wanaona hili suala kuwa na umuhimu.
Wengine wameishi nchi za nje, wengine wamesomea nchi za nje, wengine wametembea
nchi za nje na kukutana na Watanzania wengi wenye moyo na nchi yao. Wengine
wana familia zao nje, Wengine wana madaktari wao nje, na wengine wako Tanzania
hapo lakini wana ufahamu mkubwa sana wa mapenzi walionao Watanzania waishio
nje. Tukirudi nyumbani katika likizo zetu za kila mara tunaona wazi upendo
walionao kwetu, na kuwa na sisi ni tegemezi kwa taifa letu.
Mara nyingi
viongozi wakubwa wakitutembelea huku nje, katika nasaha zao huwa
wanatuhamasisha kutosahau nyumbani, kuisaidia serikali kuleta maendeleo,
kujenga nyumbani ili tuwe na mazingira mazuri ya kufikia na hata kuzikwa
tukifa, kuitangaza nchi yetu kwa mazuri mengi iliyonayo.
Haya yote
tunayafanya, lakini nusu nusu, tunayaweza kuyafanya kamili kama tukiwezeshwa
uraia pacha.
Asanteni sana
KIDUMU CHAMA CHA
MAPINDUZI
CCM-TAWI LA
CALIFORNIA
KAMATI YA SIASA YA
TAWI
Josephine
Masabala-Mwenyekiti
Erick Byorwango-Katibu
2 comments:
This is the best ever argument ya uraia pacha.... hii inapita zote nilizo wahi kuzisoma. Hakikisheni mnampa kiongozi huyo nakala ya huu ujumbe
Wasalaam - Mdau
CCM maana yake ni suppot Creativity, Concor and Move on- miaka 50 sasa. Hili swala la uraia pacha limeshapitishwa na chama tawala cha CCM. Tatizo liko kwa wale watu ambao wanajiita ni Wasomi, wabunge ambao wamejipanga kupinga swala la Uraia pacha, na chama cha Wafanya Kazi- (Tanzania worker Union Union) na wenigineo wachache wanapinga kila kitu. Kwa upande wa wasomi ( Intellectuals from different Universties in Tanznaia) tuanawaomba wakutane na wasomi wa Ugaibuin ili tuchambue swala hili- Peer Review and discussion. Tukutane uso kwa uso na kutumia curent scienfic research and evidence kuonyesha kwamba dunia ya sasa inakwenda wapi na sio kutumia mambo yaliyondikwa kwenye vitabu miaka arobaini na saba iliopita. Watanzania wanaoishi ugaibuni wanapenda sana kuiboresha nchi yao kama huko wanakoishi- kujivuna kidogo kama nchi nyingine kwa mafano tuna mlima kilimajaro- Serengeti Zanzbari na utamaduni wetu. Kama Brazil wanajivunia kwamba wana wanawake wazuri, hello- Tanzania tuna wanawake wzuri zaidi. Watu wenye ujuzi wa kuonyesha competition ni watazania wa ugaibuni. CCM, Chadema, CUF na wengine- wote juu, Juu zaidi
Temba
Post a Comment