ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 29, 2014

CCM wamtua zigo Spika Kificho

Mvutano kati ya Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho (pichani), na wanachama kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kumshutumu kuwa aliwasilisha maoni katika tume ya Jaji Warioba na kupendekeza muundo wa Muungano wa serikali tatu, umemalizika.

Mvutano huo umemalizika baada wa Spika Kificho kuweka wazi msimamo wake kwamba ni wa serikali mbili.

Alieleza msimamo wake Ijumaa iliyopita alipopewa nafasi ya kujadili Sura ya Kwanza nay a Sita ya Rasimu ya Katiba na kusema kwamba amezushiwa maneno mengi Zanzibar kwamba aliwasilisha maoni kwa tume kwamba Baraza la Wawakilishi linataka serikali tatu na kwamba ieleweke kuwa maoni yake ni serikali mbili.

Spika Kificho alisema alinukuliwa vibaya na tume ya Warioba.

Baadhi ya wanachama na viongozi wa CCM wakiwamo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walilalamika kuwa Kificho alikuwa amewasilisha maoni ambayo ni kinyume cha matakwa yao ya serikali mbili na kwamba ilikuwa ni kinyume cha kanuni.

Wakitoa maoni yao kuhusiana na msimamo wa Kificho, baadhi ya wana-CCM mjini Zanzibar walisema sasa wameridhishwa na kauli ya Kificho kukanusha waraka uliomhusisha kuunga mkono serikali tatu.

“Tunamuunga mkono Kificho hasa kutokana na kazi nzuri alioifanya katika Bunge Maalum la Katiba kwa kutetea muundo wa serikli mbili,” alisema Hafidh Ali.

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae, Muhammed Said Muhammed, alisema alihoji kwamba Tume ya Warioba ilipata wapi maoni kwamba Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanataka serikali tatu iliyapata wapi.

“Mimi ninachofahamu tume ya Jaji Warioba ilipokuja Baraza la Wawakilishi kupokea maoni yetu Wawakilishi kutoka CCM tulisema serikali mbili na wawakilishi kutoka CUF walisema wanataka Muungano wa Mkataba, sasa hizo serikali tatu zinatoka wapi?” alisema Muhammed.

Alisema anashangazwa na wajumbe wa CUF kudandia gari la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) la serikali tatu wakati wao (CUF) waliondoka Zanzibar wakiwa na msimamo wao wa serikali ya Mkataba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: