Dar es Salaam. Hatimaye Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limetoa taarifa ya wizi uliotokea katika Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni Aprili 15, mwaka huu, likisema tukio hilo lilipangwa ndani ya benki hiyo.
Katika taarifa yake jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema watu 13 akiwamo meneja wa tawi hilo na meneja wake wa uendeshaji wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za wizi huo wa zaidi jumla ya Sh500 milioni.
Kova alitoa mchanganuo wa fedha zilizoibwa kuwa ni Sh392 milioni za Tanzania, Dola 55,OOO za Marekani, Euro 2,150 na Paundi za Uingereza 50.
Kova aliwataja wanaoshikiliwa na polisi kwa tuhuma hizo kuwa ni Meneja wa tawi hilo, Alune Kasililika (28), Mkazi wa Kimara Bonyokwa na Meneja Uendeshaji, Neema Bandari.
Alisema katika wizi huo, robo tatu ya fedha zote zilizoibwa zilichukuliwa siku moja kabla ya tukio linalodaiwa kutengenezwa la wizi, kwa lengo la kuficha wizi huo na kwamba kulikuwa na vikao mbalimbali vya maandalizi ya kufanikisha wizi huo.
Alisema Aprili 15, mwaka huu siku ambayo wizi huo unatajwa kufanyika, kilichotokea ni tukio la kukamilisha njama hizo.
“Tukio hili lilileta utata tangu mwanzo tulipokwenda kukagua eneo la tukio, kwani siku moja kabla, yaani Aprili 14, gari la kubebea fedha kupeleka Benki Kuu lilifika katika tawi hilo kama ilivyo kawaida lakini fedha hazikutolewa kumbe ilikuwa ni mkakati uliowekwa kufanikisha wizi huo.”
Alisema wachunguzi wa polisi wamebaini kwamba fedha zilizoibwa katika benki hiyo zilichukuliwa siku moja kabla ya tukio la kutunga.
Alisema polisi wamefanikiwa kukamata gari moja aina ya Toyota Opa ambalo linashukiwa kutumika katika ujambazi huo na juhudi za kutafuta gari la pili zinaendelea.
Kova alisema baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa na kuhojiwa walikiri kuhusika na wizi huo na walipopekuliwa walikutwa na fedha kidogo ambazo ni sehemu ya mgawo.
“Tumegundua baadhi ya matukio ya wizi wa fedha katika benki mbalimbali yanafanywa na wafanyakazi wa benki hizo na matokeo yake Jeshi la Polisi linapata lawama kuwa halifanyi kazi yake kwa ufanisi,” alisema.
Watuhumiwa wengine
Kamanda Kova aliwataja watuhumiwa wengine wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Fredrick Lazaro (19) mkazi wa Manzese, Kakamiye Julius (31) mkazi wa Kinondoni, Idd Nguvu (32) mkazi wa Kinondoni, Sezary Masawe, Boniface Ndaro (29) mkazi wa Kijitonyama.
Wengine ni Erasmus Mroto (38) maarufu kwa jina la Menyee mkazi wa Magomeni, Deo Olomy (32) mkazi wa Manzese Darajani, Mohamed Athumani (31), mkazi wa Kimara Stopover, Joseph Mkoi (33) mkazi wa Kimara Stopover, Lucy Amos (30) mkazi wa Tabata na Grace Amon (39) mkazi wa Kibaha mkoani Pwani.
Taarifa za awali
Katika tukio la awali, ilielezwa kuwa majambazi hao walifika katika benki hiyo Aprili 15, mwaka huu, saa 3:00 wakiwa na magari mawili na bunduki aina ya SMG pamoja na bastola, kisha waliingia ndani ya benki hiyo na kupora fedha walizotoka nazo kwenye mfuko na kukimbia nazo kwa kutumia pikipiki
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment