Advertisements

Wednesday, April 16, 2014

ELIMU, MAFANIKIO KIKWAZO KUPATA MKE SAHIHI -2


BILA shaka wapenzi wasomaji wangu mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida. Kama una mushkeli kidogo, usijali, mambo yatakuwa sawa.

Rafiki zangu, naandika mada hii nikiwa hapa Singida. Bado tunaendelea na somo letu ambalo lazima nikiri kuwa lina changamoto nyingi sana katika kuelewa.

Ndugu zangu, najua ni somo gumu kidogo kueleweka lakini tutaenda sawa. Subiri hapohapo. Wiki iliyopita nilifafanua suala la elimu na mafanikio ya kimaisha.

Nikasema, mwanaume akipata vitu hivyo viwili kabla ya kufanya chaguo la kuoa, anaweza kupata wakati mgumu kumtambua mwanamke mwenye mapenzi ya dhati kwake.

MWANAMKE ANAVUTIKA NA NINI KWA MWANAUME?
Tukianzia hapa tunaweza kupata majibu sahihi zaidi ya maswali yetu. Lazima tujue mwanamke anavutika na nini kwa mwanaume? Anapenda nini kutoka kwa mwanaume? Kuna watu wanafikiri labda mwanamke anapenda mwanaume mwenye nguvu, mwonekano mzuri, mwenye fedha pekee.

Kuna vitu zaidi ambavyo mwanamke anapenda kwa mwanaume. Vitu hivyo vimejificha ndani ya vitu viwili; jinsia (kiasili) na uanaume (mafanikio). Hebu tuendelee kujifunza.

JINSIA (KIASILI)
Hapa ndipo kwenye mzizi wa pendo la dhati kutoka kwa mwanamke. Kwa kawaida, upendo huanzia hapa. Yaani kwa namna ulivyo mwanaume – basi. Mwanamke anampenda mwanaume kwa maana ya uanaume wake wa kijinsia.

Kwamba, amekupenda kwa sababu wewe ni mwanaume unayevutia kwake. Hana kingine anachotaka kwako zaidi ya ulivyo. Amekupenda kiasili kwa sababu una vitu muhimu kimuonekano anavyopenda kutoka kwa mwanaume wake.

Hapa fedha si kigezo. Elimu si kipimo. Kinachoangaliwa ni mapenzi ya dhati tu. Ni hivyo tu.

UANAUME (KIMAFANIKIO)
Ukiachana na jinsi ya kiasili, mwanamke anapenda kukutana na mwanaume ambaye anautumia uanaume wake sawasawa.

Uanaume ni pamoja na mafanikio. Mwanamke akikutana na mwanaume mwenye elimu nzuri, mali, fedha, mwenye kujiamini, anayemlinda, uwezo wa kuongoza nk, anavutika naye.
Mwanaume kiasili ni kiongozi – uongozi wake huanzia nyumbani.

Mfano, mwanamke atafurahi zaidi kuwa mke wa meneja au mkurugenzi wa taasisi fulani.
Atajisikia mwenye fahari zaidi akiwa na mwanaume mwenye kichwa kinachofanya kazi – anayehangaika kuhusu kupata mafanikio, mwenye mbinu za kusaka pesa na mwenye kujiamini.

Mwanaume hatakiwi kuwa legelege. Anapaswa kuwa na nguvu ya ushawishi na mwenye kukubalika na watu wanaomzunguka. Kupoteza sifa hizo ni kupoteza sifa ya kukutana na mwanamke mwenye kujitambua.

ZINGATIA
Vipengele hivyo viwili havitegemeani. Mwanamke sahihi ni yule mwenye upendo wa asili kwanza. Mwenye kukupenda bila kuangalia mafanikio yako ya kimaisha.

Hii inamaanisha kwamba, ikiwa umekutana na mwanamke ambaye hafahamu kuhusu mafanikio yako, umaarufu wako, elimu yako, uwezo wako kazini, uongozi wako na akakupenda, kipengele cha mafanikio kitakuwa cha ziada tu.

Suala la mafanikio ni chachu ya maisha. Maana kama ni mwanamke sahihi, kwa kuwa yeye atakuwa msaidizi wako, bila shaka mafanikio yenu yataongezeka.

Tatizo ni pale utakapokutana na mwanamke ambaye atakuwa amevutika na mafanikio yako tu kabla ya kukupenda kwa dhati. Wanawake wa aina hii wapo wengi sana siku hizi.

Ni hodari wa kuigiza mapenzi. Anaweza kuonyesha hisia kali kiasi akamshinda hata yule mwenye upendo wa dhati. Kwa sababu yeye anachoangalia kwako ni maisha, si mapenzi, hataona shida kutafuta mbinu za kukupumbaza ili umuone ni mwanamke sahihi.

Kwa taarifa yako, ukikutana na fundi sawasawa, atakulaghai na wala hutajua kuwa unaingizwa mjini. Harakaharaka mwanaume utaharakisha ndoa, kumbe umeingizwa chaka!
Ndoa yako itakuwa yenye vilio kila siku.
Wiki ijayo nitakuwa hapa katika sehemu ya mwisho ya mada hii ambapo nitafafanua vipengele vingine vitakavyotoa suluhisho,

USIKOSE! Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

No comments: