Dar es Salaam. Bajeti inayotarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni bungeni Dodoma haitakuwa na manufaa yoyote kwa Watazania, iwapo Serikali haitakuwa tayari kupunguza nakisi inayotokana na matumizi makubwa yasiyokuwa ya lazima.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa Ripoti ya Ukuaji wa Kiuchumi kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara iliyotolewa na Repoa, Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Ibrahim Lipumba alisema tatizo lililopo kwa sasa ni matumizi makubwa ya Serikali kwa mambo yasiyo ya lazima, huku ikiwa na mapato madogo.
Profesa Lipumba ametoa maoni hayo siku moja baada ya Waziri wa Fedha, Saada Nkuya kuliambia gazeti hili kuwa masharti ya wahisani na utegemezi wa fedha ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanakwamisha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo nchini.
Pamoja na kukiri imekuwa vigumu kwa Tanzania kuridhia masharti mapya ya wahisani, pia alikiri kwamba matumizi ya Serikali yamekuwa makubwa kuliko mapato, hivyo kusababisha nakisi kubwa katika bajeti ya mwaka 2013/14.
Hata hivyo, Profesa Lipumba alifafanua chanzo cha tatizo hilo wakati wa uwasilishaji ripoti iliyoandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini (Repoa) kwa kushirikiana na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ikilenga kuangalia ukuaji wa kiuchumi kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa miongoni.
Alieleza kwamba matumizi hayo ni pamoja na ya zaidi ya Sh60 bilioni zilizotumika kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo hata baada ya kukamilisha kazi yake, Serikali imesimamia kutotumia mapendekezo ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa, hivyo kupoteza mabilioni ya shilingi za walipa kodi bila sababu.
“Pamoja na matumizi makubwa ya Tume, matumizi ya Bunge la Katiba bado thamani halisi ya fedha za walipa kodi haiwezi kulipwa kwa utaratibu ambao Serikali imeamua kuutumia. Hapa tunaona namna Serikali inavyokuwa na matumizi makubwa ambayo hayana tija kwa wananchi,” alisema.
Alisema ili kuondoa kasi ya ukuaji wa nakisi, Serikali pia inatakiwa kufuta kabisa misamaha holela ya kodi inayofikia Sh1 trilioni na bilioni 800 ambayo ni sawa na asilimia tano ya pato la taifa.
Alisema miongoni mwa maeneo mengine yanayosababisha tatizo hilo ni katika miradi inayosimamiwa na Serikali ambayo mingi imekuwa ya gharama kubwa kuliko uhalisia na gharama huongezwa kwa kati ya asilimia 30 hadi 50 zaidi ya gharama halisi.
Hata hivyo, akizungumzia ripoti hiyo ya Repoa iliyoangazia zaidi ukuaji wa kiuchumi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, alisema japokuwa uchumi huo unakua, haujaweza kuwasaidia wananchi wa kawaida katika nchi za Afrika.
Awali, mwakilishi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) nchini, Thomas Baunsgaard alisema japokuwa ukuaji wa uchumi umekuwa ukitia moyo na Tanzania inafikia asilimia 7.2, bado upunguzaji wa umaskini unakwenda kwa kasi sana.
Alisema kupungua uzalishaji kwenye sekta ya kilimo kumechangia ukuaji wa sekta ya utoaji huduma na Dar es Salaam idadi ya maskini imepungua.
Mwananchi
1 comment:
ahsante sana professa lipumba mungu akubarik kwa kutufahamisha kwa kina vipi magamba wavyofuda pesa za umma mungu akuweke professa wetu tunahitaji watu kama nyinyi katika nchi yetu lakini kwa vile tumeshazoe ufisadi ndo maana nchi yetu mpaka hii leo tunategemea misaada kutoka nje kuendesha bajeti yetu what a shame
dunia ya leo watu wakiwa hawatumii akill zao ndo watu wanaoonekana wa maana sana na ndo wanaotawala professa kama wewe mafisadi daima hawatokupenda kwa kusema ukweli wako wa kisomi na experience zako
Post a Comment