ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 15, 2014

Maelfu ya abiria wakwama Ubungo

Mabasi yaendayo Dar es Salaam yakiwa yamezuiliwa katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu, Morogoro baada ya eneo la Ruvu mkoani Pwani kujaa maji. Picha na Juma Mtanda

Dar es Salaam. Uharibifu wa barabara uliotokana na mvua zinazoendelea kunyesha, umeendelea kuwatesa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa mbalimbali nchini hasa baada ya mabasi ya mikoani kuzuiwa kufanya safari zake jana.
Amri ya kuzuia mabasi hayo ilitolewa jana ikiagiza mabasi yote yasiondoke katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo hadi itakapotangazwa vinginevyo, kutokana na uharibifu wa Barabara za Kilwa, Morogoro na Bagamoyo ambako madaraja yamevunjika.
Dereva wa Basi la Adventure liendalo Kigoma, Joseph Luciano alisema walitangaziwa na Sumatra na trafiki kuwa wasubiri mpaka hapo watakapojulishwa kuondoka.
“Hatuwezi kuondoka mpaka Serikali itakapotangaza ili kuepuka faini ambayo wenzetu, wale wanaopakia nje, wametozwa,” aliongeza huku ikielezwa kuwa baadhi ya mabasi yalitozwa faini kwa kukiuka amri hiyo.
Abiria anayesafiri kwenda Kibondo, Kigoma, Lydia Lutakinikwa alisema: “Nilikuja kuchukua mzigo wa duka langu tangu Ijumaa na nimekuwa nikilala gesti. Nimeishiwa hela hivyo nalazimika kuendelea kuwapo kwenye hili basi kwa kuwa sina tena pesa ya kwenda kulipia malazi.”
Kondakta wa Basi la Taqwa liendalo Nairobi, Yahaya Maulid alisema wameruhusu kubadilishwa tiketi za abiria wao, kama walivyoelekezwa na mamlaka husika ili kutoa nafasi kwao kujipanga upya.
Mkuu wa Usalama Barabarani Ubungo, Inspekta wa Polisi, Yusuf Kamutta alisema zaidi ya mabasi 400 yameathiriwa na uamuzi huo... “Tumezuia mawakala wasitoe tiketi mpya kwa sababu abiria wa leo (jana) ndiyo wanaotarajiwa kusafiri kesho, hivyo wanaweza kuuza tiketi za kuanzia keshokutwa.”
Msururu wa magari Pwani
Kutokana na kuharibika kwa baadhi ya madaraja katika Mkoa wa Pwani, magari yaliyokuwa yakisafiri kutoka maeneo mbalimbali yalikwama katika maeneo tofauti. Baadhi yalikwama Visiga na mengine Mlandizi jirani na Kituo cha Polisi katika misururu mirefu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei aliwataka wamiliki wa magari makubwa ya mizigo wanaotumia barabara hiyo kusitisha safari zao kwa kipindi hiki hadi hapo hali itakapotengamaa.
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Pwani na uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ililazimika kuweka kambi kwa siku nzima eneo la Mlandizi jirani na daraja la Ruvu kusimamia shughuli ya ukarabati wa daraja dogo lililokuwa na hitilafu.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Tumaini Sarakikya alisema hadi jana mchana magari yalikuwa yameanza kupita upande mmoja, lakini baadaye jioni yangeanza kupita bila wasiwasi.
Waliokufa Dar wafikia 13
Mafuriko yaliyotokana na mvua hizo yamesababisha vifo vya watu 13 mkoani Dar es Salaam hadi jana, huku Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pekee ikipokea maiti tisa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema maiti mbili zilipatikana Wilaya ya Temeke na nyingine moja ilikutwa eneo la Jangwani, Ilala na miili hiyo imehifadhiwa MNH na Hospitali ya Temeke.
Alisema jitihada zinaendelea kubaini iwapo kuna miili zaidi katika mito na mabonde ambayo yalikumbwa na mafuriko hayo na ameomba mwananchi kutoa ushirikiano.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema hadi jana hospitali hiyo ilikuwa imepokea maiti tisa zote zikiwa za wanaume na kati ya hizo, mbili zimetambuliwa na ndugu zao.
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mark Njela alisema maiti moja ya mwanamume ilikutwa jana kwenye Mto wa Mabibo nyuma ya Kampuni ya Ami.
Imeandikwa na Sanjito Msafiri (Pwani), Pamela Chilongola, Ibrahim Yamola, Joseph Zablon (Dar).
Mwananchi

No comments: