ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 25, 2014

MAZUNGUMZO NJIA PEKEE YA UPATIKANAJI WA AMANI YA KUDUMU DARFUR-GEN MELLA

. Jenerali Mella, Kamanda wa Jeshi la UNAMID akibadilisha mawazo na Balozi Mwinyi, ambapo pamoja na mambo mengine, amesema wanajeshi kutoka JWTZ ambao ni sehemu ya UNAMID wameendelea kuonesha weledi na kujituma kwa hali ya juu katika eneo la ulinzi wa amani, ulinzi wa raia na usimamiaji wa misaada ya kibinadamu. Akasema kutokana na mapingano ya kikabili yanajitokeza mara kwa mara, na kuwa sehemu kubwa ya mapigano hayo yamekuwa yakitokea katika maeneo zilipo kambi za wanajeshi kutoka Tanzania, wanajeshi wetu wamejikuta wakilazimika kutoa huduma mbalimbali zikiwamo za kuwazalisha wanawake waja wazito. Utoaji wa huduma hiyo ya uzazi salama nje ya mamlaka yao imewafanya wazazi waliojifungua kuwapatia majina ya kitanzania watoto wao, kama shukrani yao kwa madaktari hao wa kitanzania kwa kuokoa maisha yao na ya watoto wao. Kushoto kwa Jenerali Mella, ni Luteni Kanali, Wilbert Ibuge, Mwambata Jeshi katika Uwakilishi wa Kudumu
. Luteni Jenerali Paul Mella, Kamanda wa Jeshi la Mseto la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika Darfur ( UNAMID) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Balozi Ramadhan Mwinyi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ( hayupo pichani). Jenerali Mella alifika katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kufuatia ziara yake ya kikazi ya siku tatu katika Umoja wa Mataifa ambapo alikuwa na mazungumzo na Wakuu mbalimbali wa UN. Akielezea tathmini yake ya miezi nane kama Kamanda wa UNAMID Jenerali Mella anasema njia pekee ya kupatikana kwa amani ya kudumu katika jimbo la Darfur ni kwa pande zinazopingana kukaa katika meza ya mazungumzo na kumaliza tofauti zao
Na Mwandishi  Maalum


Kamanda wa  Jeshi la Mseto la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika Darfur ( UNAMID) Luteni Jenerali Paul  Mella, amesema,  mazungumzo yatakayozihusisha pande zote zinazopingana katika mgogoro  na machafuko yanayoendelea katika Jimbo la Darfur  ndiyo   suluhu pekee inayoweza kurejesha hali ya Amani,  usalama na utulivu katika jimbo hilo.
Jenerali Mella,  ameyasema hayo wakati alipokuwa  akibadilishana mawazo na Balozi Ramadhani  Mwinyi,   Naibu  Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wakati Jenerali Mella alipoutembelea   Uwakilishi wa Kudumu.
Kamanda wa  Jeshi la  UNAMID alikuwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu,  ambapo alikutana na  kufanya mazungumzo na  Viongozi    mbalimbali  wa Umoja wa Mataifa.
“Katika  kipindi changu za  miezi nane sasa  kama      kamanda wa UNAMID yapo mambo mengi ambayo  nimejifunza zikiwamo  pia  changamoto mbalimbali katika eneo zima la ulinzi wa Amani katika Jimbo la Darfur. Kubwa la msingi  ambalo nimejifunza, ni kwamba, Amani ya kudumu haiwezi kurejea katika  jimbo la Darfur kama pande zote zinazopingana  hazitaweza kukaa katika meza moja   na  kufanya mazungumzo” anasema Jenerali Mella.
Na kuongeza  “  kwa tathmini yangu , wanajeshi wanaounda  UNAMID wapo pale kulinda Amani, kutoa  ulinzi kwa wananchi na kusaidia usambazaji wa  misaada ya kibinadamu. Lakini kwa kweli, hakuna Amani  ya kulinda, kwa sababu moja kubwa,  nayo ni kwamba pande zinazopingana hazijafikia   makubaliano ya  kusitisha mapigano na kurejea katika meza ya mazungumzo.”
Akielezea  zaidi tathmini yake katika  kipindi hicho ya  miezi nane ambapo anaongoza zaidi ya  walinzi wa Amani (wanajeshi)14,379 wanaounda  UNAMID. Jenerali Mella, anaeleza kwamba,  tangu achukue uongozi huo,  kumekuwapo na  mabadiliko katika mwenendo mzima wa mapigano katika jimbo hilo.
“ Changamoto  kubwa niliyokumbana nayo ni kuwa katika miezi hiyo nane ya  uongozi wangu, mwenendo mzima wa machafuko au mapingano umebadilika na  kujikita zaidi katika mapigano ya  kikabila” anabainisha na  kuongeza.
“Mapigano hayo ya kikabili  na ambayo   chimbuko lake ni kugombea raslimali zikiwamo dhahabu  mafuta na malisho,  yamepelekea kuwapo kwa wimbi kubwa la wakimbizi wa ndani.
Jenerali Mella anasema,  sehemu kubwa ya mapingano hiyo baina ya  makabila yalikuwa yanatokea karibu  na maeneo zilipo kambi zetu kwa maana ya wanajeshi  kutoka  Jeshi la wananchi wa Tanzania ( JWTZ). Ninafarijika sana  kueleza kwamba wanajeshi wetu wameonyesha weledi na uhodari wa hali ya juu kwanza kwa kutoa ulinzi kwa raia waliokuwa wakikimbia machafuko na pili kuwapatia misaada ya kibinadamu zikiwamo huduma za afya”.
“Ni katika kipindi hicho cha mapigano ambapo licha ya utoaji wa  huduma za kibinadamu kwa wakimbizi hao,   walinzi wetu wa Amani ( JWTZ), walijikuta wakilazimika kutoa huduma za dharura   kwa akina mama wajawazito zaidi ya saba waliojifungua salama watoto wao katika kambi zetu”.
“ Huduma hii ya kuwasaidia akina mama  wajawazito kujifungua salama watoto wao,  kuliwafanya  wazazi wale kuwapa  watoto  wao majina ya kitanzania kama shukrani yao kwa msaada  na  huduma  nzuri  waliyopatiwa na madaktari wa kitanzania katika kipindi hicho kigumu. Kuna watoto wenye majina ya kitanzania” anasema Jenerali Mella kwa  furaha.
Kwa upande wake,  Balozi Mwinyi ameshukuru Kamanda wa  Jeshi la  UNAMID kwa kutenga muda wake na kufika Uwakilishi wa Kudumu. Akashukuru pia kwa maelezo yake ya  kina kuhusu hali ilivyo katika  jimbo hilo la Darfur  na mchango mzima wa  walinzi wa Amani.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  ina kikosi  UNAMID  kinacho kalia maeneo  matatu ambayo ni  Khor Abeche,  Menawashe na Shangil Tobaya.
Tanzania  inakuwa nchi ya tatu kongoza  UNAMID , nchi nyingine ambazo zimewahi kuongoza ni  Nigeria na  Rwanda.

1 comment:

Anonymous said...

Kwanini uwanja unajengwa sehemu hiyo hiyo, wa develop sehemu nyengine.