Advertisements

Friday, April 18, 2014

MKUU WA WILAYA YA KITETO AVUNJA NDOA YA MTU


MKUU wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbulla, amefanikiwa kumuondoa katika ndoa mwanafunzi aliyekatishwa masomo na kulazimishwa kuolewa.
Mkuu huyo wa Wilaya (DC) amefikia hatua hiyo baada ya aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Uloki Moshi, Ngaya Baraka (17) aliyeolewa mwezi mmoja uliopita kumpigia simu na kumuomba kumsaidia kwa kuwa bado anahitaji kusoma.
Akielezea mkasa huo huo jana, Ngaya, alisema hakutaka kuolewa na badala yake aendelee na masomo, lakini baba yake alimlazimisha.
Alisema kutokana na msimamo wa baba yake alilazimika kuwatafuta viongozi mbalimbali kwa ajili ya kujiami, lakini hakufanikiwa na wakati huo alikuwa akimtafuta mkuu wa wilaya bila mafanikio.
“Siku moja nilipokuwa natoka shule nilimkuta baba ameshamwandaa kijana wa kiume ambaye alinipakia kwenye pikipiki na kunipeleka vijiji vya porini. Nilikaa na mwanaume huyo kwa uchungu huku akipata mateso ya kuchunga mifugo. 
Alinipora simu ili nisiwasiliane na mtu yoyote,” alisema.
Alieleza alifanikiwa kupata mawasiliano na kumpigia simu mkuu huyo wa wilaya ambaye aliwatuma viongozi mbalimbali  na kufanikiwa kumtoa kwa mume huyo ambaye kwa sasa amekimbia.
Kutokana na hali hiyo, mkuu huyo wa wilaya ametangaza hali ya hatari kwa jamii ya wafugaji wenye tabia ya kuwaozesha watoto wao wakiwa na umri mdogo.
Alisema mapambano hayo yataenda sambamba na kuwachukulia hatua kali wazazi ambao wanakatisha masomo watoto wao.
Alisema kitendo kilichofanywa na familia ya binti huyo ni kitendo cha udhalilishaji na unyanyasaji kutokana na kumkatisha masomo na kumlazimisha kuolewa na mfugaji kwa lengo la kulipwa mahari ya ng’ombe 20.
 Chanzo;Tanzania Daima

No comments: