Advertisements

Saturday, April 19, 2014

Ndugu wanaokula maiti za watu wakamatwa tena Pakistan


Mohammad Arif Ali  na mdogo wake Mohammad Farman Ali  wakiwa chini ya ulinzi baada ya kichwa cha mtoto kupatikana katika nyumba yao. Picha na Mtandao 
Kwa ufupi
  • Waliachiwa huru baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo mwaka jana.

Pakistan. Watu wawili wanaotuhumiwa kula nyama za binadamu wamekamatwa baada ya kichwa cha mtoto wa miaka mitatu, kukutwa katika nyumba wanayoishi nchini Pakistan.
Polisi waligundua tukio hilo la kutisha na
kuwakamata watuhumiwa Mohammad Arif Ali (35) na mdogo wake Mohammad Farman Ali mwenye miaka 30.
Kwa mujibu wa gazeti la mtandaoni la Dailymail, wanandugu hao wanaotoka katika mji mdogo wa Darya Khan wamewahi kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kula nyama za binadamu. Waliachiwa huru baada ya kumaliza kutumikia adhabu hiyo mwaka jana.
Arif na Farman walikamatwa na kuswekwa rumande wakati uchunguzi ukiendelea, baada ya tukio hilo lililowavuta wengi na kutikisa tena eneo hilo.
Miaka mitatu iliyopita ndugu hao walifukua zaidi ya miili 100 ya maiti katika makaburi yaliyopo karibu na kijiji chao kisha kuzitumia maiti hizo kama asusa.
Mkuu wa Polisi katika eneo hilo, Ameer Abdullah alisema maofisa wake wa polisi waliamua kuvamia na kufanya upekuzi katika eneo hilo, baada ya majirani kulalamika kwamba kuna harufu mbaya ambayo imekuwa ikitoka katika nyumba waliyokuwa wakiishi.
“Wakazi hao waliifahamisha polisi baada ya kusikia harufu mbaya ikitokea katika nyumba waliyokuwa wakiishi watu hawa,” alisema Abdullah.
Abdullah alisema: “Tulifika katika nyumba hiyo siku ya Jumatatu asubuhi na kufanya upekuzi kabla ya kukiona kichwa cha mtoto wa miaka mitatu.
“Baada ya kugundua kitu hicho kinachotisha, tulimkamata mmoja wa ndugu hawa Mohammad Arif na alitupatia ushirikiano hadi tulipomweka kizuizini ndugu yake,” alisema Abdullah.
Alisema jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi ili kung’amua iwapo kuna makaburi mengine yamechimbwa na watu hao kijijini hapo au katika vijiji vya jirani.
Baada ya kuulizwa maswali mengi na polisi, ndugu hao walikiri kula nyama za watu na kueleza ukweli namna walivyokuwa wakitengeneza mlo huo. Kwa kuwa Pakistan haina sheria zinazohusu ukatili wa maiti, huenda haitakuwa rahisi kwa wawili hao kufungwa jela maisha.
Wafungwa jela miaka miwili                                                                            
Wawili hao awali walifungwa  baada ya polisi kugundua kwamba maiti ya mwanamke mwenye umri wa miaka 24 ilitoweka katika kaburi alilokuwa amezikwa mwaka 2011.
Uchunguzi zaidi uliofanywa na jeshi la polisi katika nyumba ya ndugu hao, iligundulika kuwapo na sufuria iliyopikiwa nyama inayosadikiwa kuwa ya binadamu, pamoja na baadhi ya nyama zilizokuwa zimesalia.
Ofisa Upelelezi aliyechunguza kesi hiyo, Abdi Bhatti alisema: “Jeshi la polisi bado lilichunguza na kugundua mabaki ya viungo vya binadamu pamoja na sufuria lililokuwa na nyama. Pembeni kulikuwa na kuni za kupikia, shoka lililotumika kukatia nyama na kisu kikubwa. Mafuta mengi yalionekana kuganda kwenye shoka hilo.
Pia kulikuwa na mchwa wengi waliojenga kutoka jikoni mpaka chini ya kitanda. Tulifuatilia mchwa hao ambapo tulikwenda kugundua uwapo wa viungo vya binadamu na sehemu ya mwili wa mwanamke,” alisema ofisa huyo.
Inspekta Bhatti alisema: “Ilinipa kazi ngumu kwani mwili huo ulikuwa umeondolewa mguu mmoja kwenye kiuno na mwingine ulikuwa umekatwa chini ya goti. Tunaamini kwamba sehemu hiyo iliyokatwa ndiyo tuliyoikuta kwenye sufuria.”
Kwa pamoja walikuwa wameoa na wana watoto, lakini wake zao walithibitisha kwamba waliamua kuachana na waume hao, baada ya kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufukua na kula maiti.
Kifungo chao kiliisha Mei mwaka jana. Kutolewa kwao jela, kulisababisha maandamano ya umma kupinga uamuzi wa mahakama katika Mji wa Darya Khan.
Tangu kumaliza kutumikia kifungo hicho, ndugu hao wamekuwa wakiishi kama digidigi kutokana na kukwepwa  macho ya umma.
Imeandaliwa na Herieth Makwetta

No comments: