ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 15, 2014

Tano kali za utata, Mbeya City na Azam

JUZI Jumapili Mbeya City ilicheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya katika mechi ya Ligi Kuu Bara na Azam kushinda kwa mabao 2-1. Yafuatayo ni matukio matano yaliyotokea katika mchezo huo.
1. Mbeya City ilitinga uwanjani na njiwa huku wachezaji wake wakipitia mlango wa VIP na wengine kuingia na basi, mmoja wao alibeba njiwa wawili na kuwarusha angani. Mashabiki walipiga kelele kushangilia huku wengine wakikerwa na kitendo hicho kilichoonekana ni cha kishirikina.
2. Muda wote wa dakika 90 za mchezo huo mvua kubwa ilikuwa ikinyesha hali iliyosababisha wachezaji kuchafuka kwa matope na kuteleza mara kwa mara walipokuwa wanacheza.
3. Wachezaji wa Mbeya City walikuwa wakimvaa mwamuzi Nathan Lazaro kutoka Kilimanjaro kupinga baadhi ya uamuzi wake kwao na kufanya mchezo kusimama mara kwa mara. Straika Paul Nonga alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90 kwa kosa la kumzonga mwamuzi.
4. Machozi yalitawala kwa mashabiki na wachezaji wa Mbeya City baada ya mwamuzi kupuliza kipyenga cha mwisho, walilia kwa kwikwi na hasira za kufungwa na Azam kwenye uwanja wao. Ikumbukwe kuwa, Mbeya City haijawahi kufungwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.
5. Waamuzi walilazimika kubaki uwanjani kwa saa nne baada ya mchezo huo kwa kuhofia usalama wao kwani mashabiki walikuwa wakiwasubiri nje wakiwa na mawe na chupa ili wawaadhibu baada ya kutoridhika na jinsi walivyochezesha mechi hiyo. Baadaye wenyeji wa waamuzi hao ilibidi wawahamishe hoteli waliyofikia kwa usalama wao.

No comments: