Waziri wa Mambo ya Nje akiwa katika Picha ya pamoja na viongozi na wadu mbalimbali wa michezo.
Picha na Habari na Reginald Philip
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe (Mb) Leo amewataka wanamichezo wa kitanzania kujituma na kuweka bidii katika michezo ili kufanikiwa kunyakua medali za dhahabu na kuiletea sifa Tanzania.
Mhe. Membe ameyasema hayo leo tarehe 29 Aprili, 2014 wakati akikabidhi Bendera ya Taifa kwa wamichezo wapatao 50 wanaokwenda Nje ya Nchi kwa ajili ya Maandalizi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scotland mwezi Julai, 2014.
Wanamichezo hao ambao watakwenda katika nchi za China, Uturuki, New Zealand na Ethiopia wanashiriki michezo mbalimbali ikiwemo riadha, judo, kuogelea , mpira wa mezani, ngumi za ridhaa na mieleka.
Wakati wa mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Idara ya Michezo katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Leonard Thadeo, Waziri Membe alisema kuwa anaamini kwamba endapo vijana hao watajituma kwenye mazoezi na michezo wataweza kupata medali na kuiletea sifa Tanzania.
“Mtakapokuwa huko mnatakiwa kujituma kwa bidii sana, na kuweza kufanikiwa kunyakua medali za dhahabu, nawapeni changamoto ya kufanya vizuri katika michezo hiyo, kwa maana kwa kufanya vizuri mtaitangaza nchi yetu na kutuletea wafadhili wengi katika michezo”, alisisitiza Mhe. Membe.
Aidha, aliwaambia kwamba mbali ya kujitangaza, pia kwa kushinda kwao kutailetea heshima nchi yetu ambapo alitoa mfano wa Mkimbiaji wa riadha wa zamani wa Tanzania, Bw. Philibert Bayi, ambaye kwa kufanya kwake vizuri kumeifanya nchi ya Tanzania kujulikana hadi sasa.
Mhe. Membe alitumia fursa hiyo kuwaasa vijana hao kujiepusha na vitendo viovu watakapo kuwa kwenye mafunzo hayo, aliwasisitiza na kuwaambia “Hakuna kisicho wezekana”.
Waziri Membe aliwaambia wanamichezo hao kwamba endapo atapata nafasi atajumuika nao wakati wa kuelekea kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola Glasgow, Scotland hapo mwezi Julai, 2014.
Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Rais wa Chama cha Riadha Tanzania, Bw. Anthony Mataka aliipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia mpango wake wa Diplomasia ya Michezo ambayo imewawezesha wanamichezo hao kupata nafasi za kwenda kujifua tayari kwa kushiriki michezo ya Madola. “Nachukua nafasi hii na kwa namna ya pekee kumshukuru Mhe.Membe na Wizara yake kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha michezo nchini inafanikiwa kupitia Diplomasia ya Michezo,” alisema Bw. Mataka.
|
1 comment:
Maandalizi ya mashindano makubwa ni miaka sio miezi...kama kweli tuna nia njema pale tu tunapokwenda na kurudi mikono mitupu ndio tufanye maandalizi sio miezi miwili kabala.
Post a Comment