
Salum Barwany, Waziri Kivuli wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsi na Watoto
Waziri Kivuli wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsi na Watoto , Salum Barwany, amesema maujai ya albino Munghu Lugata (40) na wengine yanasababishwa na serikali kushindwa kuwalinda watu wenye ulemavu.
Lugata mkazi wa kijiji cha Gasuma mkoani Simiyu aliuawa kisha kucha, kidole gumba na mkono wake kuchukuliwa na wauaji, saa sita usiku mwanzoni mwa wiki hii.
Akiwasilisha hotuba ya kambi ya upinzani bungeni jana Barwany,alisema inasikitisha kuwa mpaka sasa serikali imeshindwa kupambana na matukio hayo,
Alisema kuuawa kwa Lugata kumeacha hisia na uchungu kwa albino wengine waliopata mikasa hiyo kutokana na kuhusishwa na imani za kishirikina huku waganga wa jadi wakituhumiwa kuhusika .
Msemaji huyo alisema matukio 140 ya kushambuliwa albino yameripotiwa ambapo 73 yamesababisha vifo na na 67 ni mashambulio ya kujeruhi sehemu mbalimbali za kama kukatwa viungo kama mkono na miguu.
Alisema hali ya kusikitisha zaidi matukio hayo waliofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi asilimia 75 yamekuwa yakihusisha wanawake na watoto hali ambayo imekuwa ikileta uchungu zaidi kwa walemavu hao.
Aliitaja mikoa inayoongozwa kwa vitendo vya ukatili dhidi ya albino ni Simiyu, Tabora, Shinyanga, Rukwa, Mara na Kagera na kuitaka serikali ifanye kila jitihada kukomesha jambo hilo.
Alisema katika siku ya walemavu wa ngozi Tanzania iliyofanyika mkoani Iringa, mwaka 2010 Waziri Mkuu Mkuu Mizengo Pinda alisema serikali itahakikisha inashinda vita hiyo, lakini imeonekana vita hiyo imeshindikana.
“ Napenda kuwaonya watu wote wanaojihusisha na vitendo vya viovu vya ukataji wa viungo na wauaji wa walemavu wa ngozi popote walipo kuwa siku zao zinahesabika ,ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi nawakikishia serikali itashinda vita hii na mtaishi kwa uhuru ndani ya nchi yenu,” alimnukuu .
Alisema kuwa pamoja na kauli hiyo Waziri Mkuu hakuna kilichofanyika kudhibiti ukatili huo.
Akichangia hotuba ya wizara hiyo, Mbunge wa Viti Maalum CCM, Mchungaji Getrude Rwakatare,alitaka serikali kuhakikisha inawalinda watu wenye ulemavu wa ngozi na kuwasaka wanaofanya vitendo vya kikatili dhidi yao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment