Saturday, May 31, 2014

MAXIMO AMBAKIZA MANJI YANGA DAIMA

Lakini Yanga kupitia kwa kocha wake msaidizi,Boniface Mkwasa imetoa sifa tatu za wachezaji wa kigeni watakaosajiliwa Jangwani.

YANGA imempiga chini rasmi, Kocha Mnigeria ambaye alikuwa pendekezo la Mholanzi Hans Pluijm aliyeondoka na sasa ina jina moja tu la Mbrazil, aliyeipa heshima Taifa Stars, Marcio Maximo.

Lakini Yanga kupitia kwa kocha wake msaidizi,Boniface Mkwasa imetoa sifa tatu za wachezaji wa kigeni watakaosajiliwa Jangwani.

Mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga na aliyedhamiria kugombea moja kati ya nafasi mbili kubwa za juu kwenye uchaguzi ujao, aliisisitiza Mwanaspoti jana Ijumaa jijini Dar es Salaam kwamba wamemshawishi Yusuf Manji abaki Yanga kwa vile hata Maximo anapenda hivyo.

Kiongozi huyo amesema kwamba kocha huyo amezungumza na uongozi kwa muda mrefu na kuwaambia kwamba yuko tayari kutua Yanga kwa vile mkataba wake na Klabu ya Francana ya Brazil umebaki mwezi mmoja.

“Ametuambia anataka kuja Yanga na amekuwa anatupigia simu mara nyingi na viongozi wengi wameonekana kumkubali sana, ingawa hili suala la uchaguzi ndio linachelewesha,”alisisitiza kigogo huyo.

“Tunataka Manji agombee tena uenyekiti ili iwe rahisi kumlipa Maximo, lakini isitoshe hata Maximo mwenyewe anataka Manji aendelee kuwepo Yanga kwa vile anadhani ndio itakuwa rahisi kwake kulipwa tofauti na akiingia mwenyekiti mwingine,”aliongeza.

Lakini suala la Manji kugombea litafahamika kesho Jumapili kwenye mkutano mkuu wa Yanga jijini Dar es Salaam ambao tajiri huyo amesisitiza kutoa msimamo wake. Mwanaspoti linajua kwamba Manji ameshawishika kuendelea kugombea Yanga sambamba na makamu wake, Clement Sanga baada ya kushawishiwa na wanachama wazito.

Maximo aliinoa Taifa Stars tangu 2006-10 na kufanikiwa kubadili mambo mbalimbali ikiwemo nidhamu za wachezaji, kutoa nafasi kwa vijana pamoja na kutengeneza mfumo unaoeleweka ambao ulisaidia wachezaji wengi wa Tanzania kujitambua. Kocha huyo amekuwa akisifika kutokana na misimamo yake ya kiuweledi ambayo ilishuhudia wachezaji kadhaa waliokuwa na majina makubwa nchini kama kipa Juma Kaseja,Athumani Idd’Chuji’ na Haruna Moshi ‘Boban’ wakisugua benchi na wakati mwingine hawakuitwa kabisa Stars.

Katika hatua nyingine, Mkwasa ambaye anamsubiri bosi wake Yanga alisema wachezaji wa kigeni kwenye usajili mpya wanahitajika katika nafasi tatu pekee.

“Tunataka wachezaji ambao watakuwa na uwezo tofauti kuzidi hawa tulionao, wachezaji hao lazima wazichezee timu za mataifa yao na nchi zao ziwe kwenye viwango vya juu Afrika tofauti na Tanzania, tutaangalia katika nafasi tatu za kiungo, winga mmoja na ile ya ushambuliaji, yeyote tutakayempata katika hao tutamsajili. Nafasi zilizosalia tutazitoa kwa wazalendo,”alisema Mkwasa. Yanga ina wachezaji wa kigeni wenye mikataba ambao ni Haruna Niyonzima, Emanuel Okwi, Hamis Kiiza na Mbuyu Twite.
CREDIT MWANASPOTI

No comments: