Saturday, May 31, 2014

KICHUPA CHA DIAMOND ALICHOFANYIA LONDON GHARAMA ZAKE AWEKA WAZI

Mteule huyo wa tuzo za BET ambaye amemshirikisha mwanamuziki Iyanya kutoka Nigeria katika wimbo huo, amesema video hiyo imemgharimu fedha nyingi, ambazo ameamua kuwekeza katika muziki huku akiamini atavuna fedha nyingi kupitia muziki wake.
KICHUPA (video) kipya cha mwanamuziki wa Tanzania Diamond Platnumz, alichorekodia London, Uingereza, kimemgharimu zaidi ya Sh70 milioni kutayarisha licha ya audio ya wimbo huo kutengenezewa Nigeria miezi miwili iliyopita.


Mteule huyo wa tuzo za BET ambaye amemshirikisha mwanamuziki Iyanya kutoka Nigeria katika wimbo huo, amesema video hiyo imemgharimu fedha nyingi, ambazo ameamua kuwekeza katika muziki huku akiamini atavuna fedha nyingi kupitia muziki wake.


Diamond anasema anaumia sana pindi anapokuwa akifanya kazi zake kwani huchukua kiasi kikubwa cha fedha na kuwekeza katika muziki ili kukuza bongofleva na kuutangaza muziki wa Tanzania.


“Si kwamba ninafanya hivi kama Diamond, la hasha! Bali ninafanya kwa mapenzi ya Tanzania. Lazima nihakikishe naendelea kuipeperusha bendera ya nchi yangu ili hata wageni wanaonijua sasa waone dogo sikubahatisha,” anasema Diamond.


Anasema alitumia Dola 25,000 pekee kumlipa prodyuza wa video hiyo, kwani alitakiwa amfuate London yalipo makazi yake.


“Kiukweli tunaumia kwa sababu kumlipa Moe Musa peke yake na kupata kila kitu kwenye hii video ya juzi tumemlipa Moe Dola 25,000 (Sh40 milioni) ambazo zilinitoka hapo bado mambo mengine sijafanya,” anasema na kuongeza:


“Hiyo ilikuwa ni fedha niliyomlipa prodyuza, hapo usisahau tumewatoa kina Iyanya Nigeria kwa hela yetu kuwapeleka London, kuwalipia nauli ya VIP katika ndege na kuwatafutia hoteli za kulala ambazo ni ghali, nyota tano si hoteli ambazo sisi tungeweza kufikia, ni gharama kubwa,” anasema Diamond.


Meneja anayesimamia kazi za Diamond kwa sasa, Babu Tale anasema kutokana na kupiga hatua kwa Diamond na kuingia kwenye levo za kimataifa, imebidi waanze kufanya video za kiwango hicho cha kimataifa lakini haimaanishi kwamba hatafanya tena video hapa nchini.


“Video tuliyofanya na Iyanya Uingereza ni kwa sababu tulikuwa tunamhitaji mtayarishaji Moe Musa ambaye anaishi na kufanya kazi zake Uingereza, ndiyo maana tukasafiri mpaka huko,” anasema.


Babu Tale anasisitiza kwamba Diamond pia ameshafanya kolabo kadhaa Nigeria, hivyo akishamaliza ziara yake Ghana, anatarajia kufanya video nyingine Nigeria na ikitokea wanatakiwa kufanya video Tanzania watafanya hivyo.


Wiki mbili zilizopita Diamond alikuwa Uingereza kwa ajili ya kufanya shoo pamoja na kufanya video ya wimbo wake aliofanya na Iyanya. Aliwasili nchini na baada ya siku mbili alikwea pipa kuelekea Marekani ambako huko amefanya shoo kadhaa.


Kabla ya kurejea nchini Diamond atatua Ghana kwa ajili ya kolabo nyingine na Davido itakayowahusisha pia Tiwa Savage wa Nigeria na Mafikizolo wa Afrika Kusini ikiwa ni kampeni ya kituo kimoja kikubwa cha TV Afrika. Awania tuzo za BET


Wakati maelfu ya Watanzania wakishangilia ushindi wa Diamond katika tuzo za nyumbani KTMA, msanii huyu aliteuliwa kuwania tuzo ya BET. Diamond amechaguliwa katika tuzo hizo wiki mbili baada ya kunyakua tuzo saba za Kilimanjaro Music Awards 2014. Hata hivyo bado anawania tuzo ya KORA NA MTV (MAMA) zinazotarajiwa kutolewa Afrika Kusini Juni 7 mwaka huu.


Tuzo hizo zinazoandaliwa na televisheni kubwa ya Marekani ya BET, Diamond yupo kwenye kipengele cha wanaogombea tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kimataifa-Afrika (Best International Act Africa).


Katika kipengele hicho Diamond anachuana na wanamuziki: Davido (Nigeria), Mafikizolo (South Africa), Sarkodie (Ghana), Tiwa Savage (Nigeria) na Toofan (Togo).


BET kupitia ukurasa wa Twitter waliandika kuthibitisha kuchaguliwa kwa Diamond na kumpongeza akiwa pia ni msanii pekee wa Afrika Mashariki kwenye tuzo hizi za mwaka huu.


Katika tuzo za mwaka 2013zikiwashirikisha Radio na Weasel wa Uganda, tuzo hii ilichukuliwa na msanii Ice Prince kutoka Nigeria akiwabwaga wasanii wengine kama 2Face Idibia, R2Bees kutoka Ghana na Toya Delazy na Donald wote wa Afrika Kusini.


BET ni nini?


Tuzo hizi zilianzishwa na Kituo cha Televisheni cha Mtandao wa Watu Weusi Duniani kwa lengo la kuwakutanisha wasanii weusi.


Wasanii wanaokutanishwa na tuzo hizo ni pamoja na wanamuziki, wacheza sinema, wanamichezo na wasanii wote wanaong’ara maeneo mbalimbali duniani. Kwa mwaka huu Diamond amefanikiwa kung’ara na kuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kushiriki tangu kuanzishwa kwake mwaka 2001.


Tuzo hizi hutolewa mara moja kila mwaka kwa makundi yote ya wasanii waliong’ara kwa mwaka uliopita ikiwa ni moja kati ya tuzo zinazovuta hisia za idadi kubwa ya mashabiki duniani wakati wa kutangazwa ‘laivu’ na televisheni hiyo ya BET.


Dau lake sasa ni Sh45 milioni


Wakati wasanii wengine wakiendelea kujiuliza na kulalamika, Diamond sasa anatangaza dau lake jipya ambapo bila hiyo fedha huwezi kumpata jukwaani. Licha ya fedha za dharura ambazo, promota anatakiwa kuziandaa kwa ajili ya kumkarimu na mahitaji yake hadi kumpandisha jukwaani si fedha za maandazi.


Kwanza bila kumwonyesha kuanzia Sh 45 milioni kwenda juu, utaishia kuongea naye kwenye simu tu, bila hata ya kuona sura yake. Mbali na hilo, kwanza kama umeshatenga hilo fungu na kufanikisha kumuita kwa ajili ya kusaini mkataba, inatakiwa umsafirishe kwa ndege na apate daraja la kwanza au ndege ya kukodi.


Pia anahitaji hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano pia uwe umashatenga vyumba maalumu vikubwa kwa ajili ya timu yake wakiwamo wacheza shoo, mpiga picha, Dj, mlinzi na msaidizi bila kumsahau meneja wake.

1 comment:

Anonymous said...

nampenda jamaa kwa kubarikiwa kuimba lakini masifa yamezidi kila kukicha na nadhani anajiharibia kama yeye anaona watu wanamfagilia basi ajiulize NGOMA IKIVUMA SANA MWISHOWE HUWA NINI? AJAZE MWENYEWE

lakini katika karne hii kuwa saka vi baby vyema tamaa tamaa watu ndo maana wanatangaza mali zao na kuvaa minyonyoro kifuani ili kuonyesha anauwezo wa fedha ambayo ni fedheha.

inasikitisha sana mtu ukipiga muziki wako ukaonyesha kipaji chako watu fan zako watakuwa na wewe daima lakini ukianza kuonyesha utajiri wako huu ndo ukosefu wa fani yako na wa kufikiri na mwishowe kuwa manganganya na kwenda kwa BABU WA LIONDO.

HAKUNA WANA MUZIKI TANZANIA WALIOPO AMBAO HAWASIKIKI TENA NDO WENYE TALENT ZAO SI HAWA HATA KIDOGO