ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 1, 2014

MKURUGENZI WA HABARI ATOA UFAFANUZI TUZO YA JAJI WARIOBA

Mkurugenzi Idara ya Habari Assah Mwambene akitoa ufafanuzi mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya tuzo aliyopewa Jaji Joseph Sinde Warioba wakati wa Sherehe za Muungano, ufafanuzi huo umetolewa leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Idara ya Habari Assah Mwambene (kushoto) akijibu maswali mbalimbali wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya tuzo aliyopewa Jaji Joseph Sinde Warioba wakati wa Sherehe za Muungano. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Vicent Tiganya. Mkutano huo umefanyika leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Waandishi wa Habari waliohudhuria Mkutano wakisikiliza na kufatilia kwa makini maelezo toka kwa Mkurugenzi Idara ya Habari juu ya tuzo aliyopewa Jaji Joseph Sinde Warioba wakati wa Sherehe za Muungano, ufafanuzi huo umetolewa leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo jijini Dar es Salaam.Picha zote na Benedict Liwenga
Na Magreth Kinabo

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Assah Mwambene amesema Jaji Joseph Warioba alitunukiwa tuzo ya muungano iliyotukuka kwa kuwa alistahili kupewa kama viongozi wengine na kuwa kitendo si kumkejeli kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti hivi karibuni.
Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu suala hilo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa MAELEZO jijini Dares Salaam.
“Kumekuwa kuna taarifa katika baadhi ya magazeti kuwa Serikali kumpa tuzo Jaji Warioba ni kumkejeli, Ninapenda kuwataarifu kuwa kitendo cha Serikali kumpa tuzo Jaji Warioba haikumkejeli wala kumtukana. Jaji Warioba anastahili kupewa tuzo kama mawaziri wakuu wengine kwa kuwa mchango wake katika muungano unajulikana,” alisema Mwambene. 
Tuzo hiyo aliyoipewa Jaji Warioba, wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tangayika na Zanzibar.
Mwambene aliongeza kuwa tuzo hiyo haihusiani na mjadala wa Rasimu ya Katiba.

Alifafanua kuwa katika mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba uliokuwa ukifanyika katika Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, baadhi ya wajumbe walikuwa wanatoa mawazo yao na si kwamba wanapingana na Jaji Warioba 

“ Mjumbe anatoa mawazo yake wakati wa kujadili kwa kuwa hiyo bado ni rasimu, hivyo hapingani na Jaji Warioba,” alisisitiza huku akisema rasimu huwa inafanyiwa marekebisho

Katika hatua nyingine,Mkurugenzi huyo , alisema bado Ofisi yake inaendelea na hatua ya pili kuhusu gazeti la MAWIO kutoa maelezo ya kuchapisha habari yenye kichwa cha habari ‘Hati Muungano Utata’.


Mwambene alifafanua kuwa ofisi hiyo inaendelea na suala hilo kwa hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa viongozi husika wa gazeti kutoa maelezo baada ya hapo awali kupeleka barua ya kutaka maelezo hayo kwenye Ofisi za gazeti la ‘MAWIO’ na kukuta zimefungwa.

Aidha alisema kuwa hata majirani wa ofisi hizo walikataa kupokea barua hiyo, kwa maelezo kuwa kama ni masuala ya habari wahusika ndio wanapaswa kuipokea.

Aliongeza kwamba ofisi yake itafanya maamuzi sahihi ikiwa haitapata maelezo hayo, hivyo isijeikalaumiwa.

Mwambene aliwataka waandishi wa habari kuwa na kitambulisho cha uandishi wa habari (Press Card) na ametoa muda wa wiki moja kuanzia leo kwa mwandishi ambaye hana ili kuweza kukamilisha taratibu za kukipata.

Pia amewataka waandishi wa habari kuwa na heshima katika utendaji kazi wa taaluma hiyo na kuzingatia mavazi yanayostahili kwani wao ni kioo cha jamii.
CRIDET:MATUKIO NA VIJANA.

No comments: