Waziri wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu.PICHA|MAKTABA
Dodoma. Waziri
wa zamani wa Uchukuzi, Omar Nundu jana aliikalia kooni Serikali kwa
kuwakumbatia wageni na kuibua madai kuwa baadhi ya vigogo wa Serikali
walipewa nyumba wakati wa kubinafsisha viwanda nchini.
Nundu ambaye
ni Mbunge wa Tanga Mjini (CCM), alitoa kauli hiyo jana jioni alipokuwa
akichangia bajeti ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda
kwa mwaka 2014/15. “Hizi tax holiday (kipindi maalumu cha kusamehewa
kodi) ziondolewe maana siyo tunasema maneno tu, umefika wakati sasa
maneno yakae kando vitendo vifanye kazi, watu wamechukua viwanda kwa
ajili ya kuvidhoofisha tu,” alisema.
“Mnapewa
vijijumba, watu wazima ovyoo, unapewa kijijumba halafu unadhalilisha
nchi hapa! Mmeyafanya! Twende viwanda virudi tufanye kazi,” alisema
Nundu bila kuwataja kwa majina waliopewa nyumba.
Nundu
alisema uchumi duniani kote unategemea viwanda na kwamba pamoja na
wizara kueleza mambo mengi ukweli ni kwamba hayatoshi na kuna mengi ya
kufanya.
Utajiri wa magadi
Awali,
akiwasilisha bajeti yake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah
Kigoda alisema uzalishaji wa magadi soda utaanza kuliingizia taifa Dola
320 milioni za Marekani (Sh520 bilioni) kwa mwaka kuanzia mwaka 2016/17.
Alisema
mradi huo unaoendeshwa na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC),
unatarajia kuzalisha tani milioni moja za madini hayo na bidhaa nyingine
za chumvi kwa mwaka. Alisema tafiti kuhusu wingi na ubora wa rasilimali
ya magadi soda zilikamilika mwaka 2013/14 na kiasi cha tani bilioni
4.68 za magadi ambazo huongezeka kwa mita za ujazo milioni 1.86
ziligunduliwa.
Dk Kigoda alisema kiasi hicho kiligunduliwa katika Bonde la Engaruka na jitihada za kumtafuta mtaalamu mshauri zimeanza.
CHANZO
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment