Saturday, May 31, 2014

Serikali yamtuhumu Balozi wa Uingereza

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Dianna Melrose. Picha na Maktaba

Dodoma. Serikali imetangaza rasmi mgogoro wa kidiplomasia kati yake na Balozi wa Uingereza nchini ikimtaka kujieleza kwa madai ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi.

Mgogoro huo ulitangazwa bungeni mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle aliyemtaka balozi huyo kufika Wizara ya Mambo ya Nje kujibu tuhuma hizo.

Kiini cha Serikali kumtuhumu balozi huyo ni hatua ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) kuihusisha Uingereza na urejeshwaji wa Sh76 bilioni za chenji ya Rada.

“Katika mchango wake (Kafulila), ameongea jambo moja nyeti sana na hili bora niliseme ili liwe fundisho kwa wengine… Hii ni nchi huru baada ya mwaka 1961,” alisema Naibu Waziri.

“Zimekuwapo ripoti kwamba Balozi wa Uingereza amekuwa akijihusisha kuratibu vikao mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam na Dodoma kinyume cha utaratibu na hadhi ya kidiplomasia.”

Huku akionyesha kuwa na hasira, Maselle aliongeza kusema: “Vikao hivyo vina malengo ya kuhujumu mipango na mikakati ya maendeleo, ushahidi huo upo na utakapohitajika utatolewa.”

“Inasikitisha na kuchukiza balozi wa taifa kama Uingereza akifanya vitendo kinyume cha maadili… Anahusishwa kushawishi marafiki wa maendeleo wasitishe misaada ya kibajeti kwa Tanzania,”alisema.

Balozi wa Uingereza

Hata hivyo, Mwananchi ilimtafuta Balozi wa Uingereza Dianna Melrose, azungumzie suala hilo, msemaji wake Tamsin Clayton ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Siasa, Miradi na Mahusiano alisema wameshtushwa na taarifa hizo, lakini kwa sasa hawawezi kusema chochote mpaka wafahamu chanzo cha tatizo.

Aidha Naibu waziri Maselle alisema kuwa hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), alikuja Tanzania na kwamba upo ushahidi kuwa Balozi huyo wa Uingereza, alitamka kuwa anafikiria kuishawishi Serikali yake isitoe fedha za Miradi ya Maendeleo ya Millenia (MCC2).

“Ni aibu kwa Serikali ya Waziri Mkuu, David Cameron kwa balozi wake kufanya uwakala wa Benki ya Standard Chartered, kuishawishi Serikali ya Tanzania ikope fedha ili kulipa kampuni binafsi,” alisema Maselle huku akipigiwa makofi na wabunge wengi wa CCM na kuongeza:

“Rais Kikwete amelikataa kwa nguvu zote…, Serikali haiwezi kubeba mzigo wa kampuni binafsi.”

Alisema chini ya mkataba wa Vienna, katika vifungu vya 41 na 42 Serikali wakati wowote bila kuhojiwa kuhusu uamuzi huo, inaweza kumtangaza mfanyakazi yeyote wa ubalozi au balozi kuwa hatakiwi na nchi yake.

Maselle alisema na ikitokea hivyo na balozi huyo asirudishwe kwao, basi atanyimwa haki zote za kibalozi na baadaye kushtakiwa.

“Kwa kuwa kinga ya kushtakiwa inawalinda wanadiplomasia wote, lakini mkataba huo wa Vienna unawataka mabalozi kuheshimu sheria za nchi na kanuni zake,” alisisitiza Maselle.

“Kinyume chake Serikali inaweza kumfukuza balozi anayefanya mipango ya kijasusi au kuhujumu Serikali na ustawi wa nchi ama uchochezi wa uvunjifu wa amani,” alisema Maselle.

Aliongeza: “Kama ilivyojitokeza hivi karibuni mkoani Mtwara, Serikali inamtaka Balozi wa Uingereza ajipime kama anafaa na anatosha kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania.”

“Tanzania ni nchi huru hatutakubali kuburuzwa wala kuingiliwa katika mambo yetu ya ndani yanayohusu ulinzi na usalama na maendeleo ya wananchi wake,” alisema.

Waziri Maselle ameitaka Serikali ya Uingereza ichunguze tuhuma dhidi ya balozi wake na kuchukua hatua zaidi ili kuepusha mgogoro wa kidiplomasia unaoweza kukuzwa na balozi huyo.

“Tunamtaka Balozi wa Uingereza afike Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kujibu tuhuma hizo… Kuna mambo mengi yanaendelea, nashukuru Kafulila leo ametufunilia,” alisema.

“Balozi anafanya mambo ambayo hayana hadhi ya ubalozi…. Deni la IPTL ni la kampuni binafsi, inakuwaje balozi atuambie tukope tulipe deni la kampuni binafsi?”Alihoji Maselle.

Itakumbukwa kuwa, wiki iliyopita kulisambazwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) ukimhusisha balozi huyo na njama za kukwamisha Bajeti ya Nishati na Madini.

Muhongo amjibu Mnyika

Akijibu hoja za wabunge jana jioni, Profesa Muhongo alisema aliifananisha taarifa ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya wizara hiyo mwaka 2014/15 ni kama stori tu, huku akifafanua mipango ya wizara hiyo.

“Bahati yao wametoka maana nilitaka niwape hesabu moja kuhusu Mnyika. Hesabu yenyewe ni hivi; Mnyika kipeo cha nne kujumlisha nne sawa sawa wa nne, Mnyika ni ngapi” alihoji na kuwafanya wabunge kushangilia huku wakisema “Mnyika ni sifuri”.

Profesa Muhongo alisema kuwa ana ushahidi kuwa baadhi ya wabunge wa Kambi ya Upinzani nao wamechota fedha za IPTL na kusisitiza anazo picha zao za video zikiwaonyesha wakiwa wanasaini nyaraka mbalimbali za fedha.

Watoka nje ya Bunge

Wakati haya yakiendelea jana, wabunge wa upinzani walitoka nje kuonyesha kupinga kutozingatiwa kwa hoja zao, walizodai za msingi kuhusu suala hilo wakisema hawapo tayari kuwa sehemu ya kulinajisi taifa.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliongoza wabunge hao kutoka nje baada ya kutoa mchango wake uliosisitiza kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza sakata la Esrow.

Awali, wabunge watatu waliwasilisha nyaraka za ushahidi kutaka Bunge liunde kamati teule iliyo huru kuchunguza suala hilo.

Katika mjadala wa hotuba ya makadirio na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, wabunge wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), walionekana kujipanga kutetea bajeti hiyo, lakini Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka aliungana na wabunge wa upinzani kuikataa akisema: “Sitaiunga mkono hoja hata kwa risasi.”

Akaunti ya Escrow ilifunguliwa wakati kukiwa na mgogoro wa kisheria baina ya wabia wa zamani wa Kampuni ya IPTL (VIP Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande mwingine.

Akaunti hiyo, iliyokuwa Benki Kuu (BoT), ilifunguliwa kwa masharti kwamba upande wowote usiguse fedha hizo, hadi mzozo huo utakapotatuliwa.

Ole Sendeka

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alienda mbali zaidi na kudai mmoja wa waliochota fedha hizo, alichukua Dola 5 milioni za Marekani kutoka Benki ya Stanbic akitumia mfuko wa sulphat kwa kurudia.

Mbunge huyo alisema kuwa watu wenye uhusiano na ‘wakubwa’ walichota Dola 200,000 mara tano kwa siku moja katika Benki ya Standard Chartered huku akihoji: “Kwa nini watu hao hawajakamatwa hadi sasa?”

Kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha Sh1,630 kwa Dola moja, Dola 5 milioni ni sawa na Sh8.15 bilioni, wakati Dola 200,000 mara tano ni sawa Dola milioni moja zilizo sawa na Sh1.6 bilioni.

Bunge lilikabidhiwa rundo la nyaraka za ushahidi, huku Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila akisema: “Kwa Bunge makini, hata kifo cha Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, kilipaswa kuchunguzwa.”

Hayo yalijitokeza jana, muda mfupi baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuwasilisha kitabu chenye maoni ya kambi hiyo chenye kurasa 119, kikianika ufisadi wa kutisha wa mabilioni serikalini.

Mnyika

Maoni hayo yaliwasilishwa na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika ambaye pamoja na kuwasilisha maoni hayo, aliwasilisha nyaraka mbalimbali kuhusu sakata la Escrow.

Kutokana na mhimili huo kuguswa ukielezwa kushindwa kuisimamia Serikali, Spika wa Bunge, alikuwa wa kwanza kujivua lawama kwa kueleza kuwa kama ni makosa basi ni ya wabunge wote.

“Suala kwamba Bunge halifanyi kazi yake ni kosa la Bunge lote pamoja na nyinyi (upinzani) kwa hiyo wa kwanza kulaumiwa ni nyinyi wabunge,”alisema Spika Makinda na kuongeza:

“Kwa sababu mimi nimeunda kamati zangu, kila kamati inasimamia wizara moja moja, kama nyinyi hamtekelezi wajibu wenu, mjilaumu wenyewe huko mliko.”

Kafulila ambaye ndiye aliyeibua kashfa hiyo ya Escrow, jana aliendelea kuwa mwiba kwa Serikali pale alipotoa begi zima bungeni, akisema limesheheni nyaraka za ushahidi kuhusu kashfa hiyo ya Escrow.

“Kama kweli Bunge hili ni la wawakilishi wa Watanzania wanaothamini utajiri wa mali yao, basi iundwe Kamati Teule ya Bunge. Kama wewe ni msafi, unaogopa nini kuchunguzwa?”alihoji Kafulila.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, aliwataka wabunge wa CCM kukumbuka kiapo chao cha utii walichokula cha kusema kweli daima, rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.

“Fikiria mtu anaingia benki anaondoka na Dola 5 milioni kwa mfuko wa Sulphate… Nataka Kamati Teule ya Bunge iundwe kuona ukweli huu,” alisema Ole Sendeka na kuongeza:

“Tunataka tuthibitishe juu ya watu wenye uhusiano na wakubwa wa nchi hii waliokwenda katika Benki ya Standard Chartered na kusafirisha Dola 200,000 mara tano.”

“Watu wanasafirisha Dola 2 milioni kinyume cha sheria ya kutakatisha fedha hawajakamatwa na wako mpaka leo... Nataka mtueleze Serikali ilikuwa wapi wakati ilipewa tahadhari na Kampuni ya VIP?”alihoji.

Hata hivyo, wakati Sendeka akiendelea kushusha makombora, kipaza sauti chake kilizimwa kuashiria muda umekwisha na yeye kulalamika kuwa muda wake ulikuwa haujaisha bali amechakachuliwa.

Awali Mnyika alilitaka Bunge kuunda tume kuchunguza kashfa hiyo ili kujua mbivu na mbichi dhidi ya sakata hilo.

Mnyika alisema inasadikiwa wezi wa fedha za Escrow wako ndani ya Bunge hilo na kwamba kamwe hawataunga mkono CAG na Takukuru kupewa jukumu la kuchunguza kashfa hiyo.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Fidelis Butahe na Habel Chidawali.

Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Misaada mnayoipata kutoka Western Countries inatokana na pesa za walipa kodi wa hizo nchi..nyinyi hamthamini walipa kodi wa Tanzania:( kwa uchafu huu usiokwisha kila uchao mnafikiri hawa mabalozi hawana macho na masikio? Rais wetu kila uchao yuko ughaibuni kuomba misaada ambayo inaishia kwenye matumbo ya wachache..Huyu balozi ni mkombozi wa wanyonge na mwiba kwa serikali..Mnafikiri kila mtu ni mjinga?