ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 31, 2014

WALIMU WA KIKE RUANGWA, LINDI WAOGOPA KUTOA ADHABU KWA WANAFUNZI WA KIKE

Ruangwa, Lindi

Walimu wa kike wa shule za msingi wilayani Ruangwa mkoani Lindi, wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wa kike kutokana na wanafunzi hao kuwachukulia waume zao kama kulipiza kisasi kwa adhabu wanayopewa na walimu wao.

Kadhalika walimu wa kiume wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wakiume kwa hofu ya kuchomewa nyumba zao moto.

Mwalimu wa kike ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema aliwahi kutoa adhabu kwa mwanafunzi wa darasa la tano ambaye alimchukulia mumewe wa ndoa ili kumkomesha.

Alisema alimuonya mwanafunzi huyo bila mafanikio na kuamua kwenda kwa Afisa wa Ustawi wa Jamii ambaye alisaidia kunusuru ndoa yake.
Alisema kutokana na hali hiyo walimu wote wa kike wanaogopa kutoa adhabu kwa wanafunzi wa kike.

Utafiti wa kihabari uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kuhusu ukatili, unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto, katika Wilaya ya Ruangwa mkoa wa Lindi, umebaini kuwepo kwa hali hiyo.
Chama hicho kinafanya utafiti wa kihabari katika wilaya kumi za Tanzania Bara na Zanzibar.

Akiongea na NIPASHE, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkata kata ya Nandagala, Wilaya ya Ruangwa, Ismail Chikandanda, alisema kuna uadui mkubwa kati ya walimu na wazazi kutokana na kutokupenda watoto wao kupewa adhabu.

Chikandanda, alisema katika tukio moja wanafunzi walipigana, mwalimu alimchapa mtoto aliyeanzisha ugomvi lakini baada ya kipindi mwanafunzi alitoka darasani na kwenda kumuita bibi yake ambaye aliita wanakijiji wakiwa na silaha kumtafuta mwalimu aliyemwadhibu mwanafunzi huyo.

Mwalimu wa kiume ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema nyumba ilichomwa moto na wanakijiji baada ya kumwadhibu mwanafunzi wa kiume.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule ya Msingi Ruangwa, Sharifa Hassan, alisema kuwa tatizo kubwa linalowafanya wanafunzi kuwa na tabia mbaya ni kutokana na ngoma za jando na unyago wanazochezwa na kujiona wako sawa na wakubwa.

Afisa Elimu Kilimo na Ufugaji wa Wilaya ya Ruangwa Yussuf Chilumba, alisema tatizo kubwa ni wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu, kwani hata wazazi wao hawakusoma hali inayowafanya kushindwa kusimamia maendeleo yao ya elimu,
“Wazazi wanawaomba wanafunzi wao wasifanye mtihani vizuri ili wasifaulu kwani watawapa shida ya kuwasomesha,” alisema Diwani wa kata ya Nandagala, Wilaya ya Ruangwa, Adrew Chikongwe, alisema kuwa ugomvi kati ya wazazi na walimu ameumaliza na kuanzia wakati huu kutakuwa na amani na hali ya elimu itaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na kuwahimiza walimu kuwafundisha kwa bidii watoto.
CHANZO: NIPASHE

No comments: