ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 12, 2014

TANZANIA YASISITIZA UWEZESHWAJI WA NCHI MASKINI

 Dr. Lorah Madete akimpongeza mmoja wa Mwenyekiti- Mwenza  wa Kikundi   Kazi Mwakilishi wa Hungary Balozi Csaba Korosi mwishoni wa  mkutano wa 11 wa kikundi kazi hicho.  Pembeni anaonekana Mwakilishi wa Kenya, Balozi Macharia  Kamau ambaye  pia ni Mwenye Kiti- Mwenza wa kikundi hicho
 Balozi Tuvako Manongi,  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  akijiandaa kuwasilisha mchango na maoni ya Tanzania  wakati wa  Mkutano wa kumi na Moja wa Kikundi  Kazi cha Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa. Kikundi  Kazi hicho ambacho Tanzania ni  mjumbe kilikutana wa wiki moja  ambapo kilipitia na kuboresha rasimu ya malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015. Walio  kaa nyuma wa Balozi ni  Dr. Lorah Madete, Afisa Mkuu kutoka  Ofisi ya Rais-Tume ya  Mipango na Bw. Noel Kangada Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu

Na Mwandishi Maalum
 Kikundi kazi cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichopewa  jukumu la kupendekeza Malengo Mapya  ya Maendeleo Endelevu baada ya  2015 ( SDGs) kimemaliza mkutano wake wa  kumi na moja kwa kupitisha maazimio mbalimbali.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 30 zinazounda kikundi kazi hicho na imeendelea kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba, matakwa ya nchi maskini na zinazoendelea yanazingatiwa ipasavyo katika maandalizi  ya malengo hayo mapya ambayo yatachukua nafasi ya  Malengo ya Maendeleo ya  Millenia ( MDGs).

Wajumbe wa  Kikundi kazi hicho  walikutana kwa wiki moja hapa Makao  Makuu ya Umoja wa Mataifa,  na kazi kubwa iliyofanyika katika wiki hiyo moja, ilikuwa ni  kupitia na kuboresha rasimu ya malengo   mapya ya maendeleo  iliyokuwa imeandaliwa na   Wawakilishi wa Kudumu wa Kenya na Hungary ambao ni Wenyeviti -Wenza wa  Kikundi Kazi hicho.
Rasimu hiyo ilijumuisha maeneo muhimu  yaliyomo kwenye Malengo ya Millenia  na ambayo yanahitaji msisitizo na msukumo zaidi katika mpango mpya wa maendeleo baada ya 2015. Maeneo hayo ni pamoja na kuondoa umaskni, kuhakikisha upatikanaji wa chakula, afya, elimu  na uwezeshaji wa wanawake.
Aidha maeneo mapya yanayojumuishwa ni pamoja na  upatikanaji wa maji safi na salama,  nishati, miundombinu, utunzaji wa mazingira  yakiwamo ya  baharini, kuhakikisha usawa miongoni na baina ya nchi, na ujenzi wa jamii zenye amani, zinazotingatia utawala bora na utawala wa sheria
Akichangia majadiliano ya  uboreshaji wa rasimi hiyo,  Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa  Mataifa, na  ambaye aliongoza ujumbe wa Tanzania katika  mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa uwezeshaji  makini wa nchi maskini  na zinazoendelea.
Balozi Manongi alieleza kuwa nchi maskini na zinazoendelea  zinapashwa kuwezeshwa ili  kupitia uwezeshwaji huo  basi ziweze kuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza malengo mapya ya maendeleo  kama  ili vyokubalika katika Mkutano wa  Kimataifa wa Maendeleo Endelevu uliofanyika  Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2012.
Aliyataja maeneo ambayo nchi maskini na zinazoendelea zinahitaji uwezeshwaji makini kuwa ni  pamoja  na , masuala ya  biashara ambapo nchi zilizoendelea  zinatakiwa  kupunguza vikwazo vinavyozinyima nchi zinazoendelea  kufaidi fursa za biashara ya kimataifa.

Vile vile Tanzania  imezitaka nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi maskini kujenga uwezo wa kuendesha  sekta muhimu kama vile kilimo, uchukuzi, viwanda, elimu na afya, sekta ambazo  Tanzania  inaamini   ni muhimu kwa maendeleo.
Katika mkutano huo wa  kumi na moja na ambao pia  Asasi zisizo  za Kiserikali zilipata pia fursa ya kuwasilisha mapendekezo yao. Tanzania pia imezitaka nchi   zilizoendelea na zinazoibukia kiuchumi kuzipatia nchi maskini teknolojia salama na uelewa utakazoziwezesha kuongeza kasi ya maendeleo nchi zao.
Balozi Manongi akiwasilisha  maoni ya Tanzania, pia  alisisitiza  suala  la upatikanaji wa fedha  za  ndani mathlani kupitia ukusanyaji wa mapato. Pamoja na  misaada na uwekezaji  kutoka nje katika kufanikisha utekelezaji wa malengo hayo.
Kikundi  kazi kinatarajiwa kuhitimisha shughuli zake Julai 2014 kwa kuwasilisha taarifa yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye naye ataiwasilisha taarifa hiyo  kwenye Kikao cha 69 cha Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba  2014.
Taarifa hiyo pamoja na  taarifa za michakato mingine kuhusu agenda ya maendeleo baada ya  2015, itakuwa ndio msingi wa majadiliano ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa  yatakayohitimishwa mwezi Septembea 2015 katika  Mkutano wa Wakuu wa  Nchi na Serikali  ambapo wanatatarajiwa kupitsha agenda hiyo na malengo  ya maendeleo endelevu ambayo ndiyo mrithi wa Malengo ya  sasa ya Millenia.

No comments: