
Wakati mwingine wapo watu ambao wamejikuta wakiingia kwenye uhusiano kwa kujilazimisha tu; kuangalia matamanio ya kawaida ya kibinadamu ambayo kimsingi huongozwa na akili na utashi.
Hilo ni jambo baya ambalo, mwisho wake husababisha matatizo makubwa.
Wapo ambao huamua tu kujiingiza kwenye uhusiano wakiwa na lengo la kujifunza kupenda. Hilo ni kosa.
Hakuna kujifunza kwenye mapenzi. Pendo hukaa ndani ya moyo; huwezi kulazimisha au kusubiri mabadiliko ambayo hayapo. Kama umependa, umependa na kama hakuna pendo, basi hakuna tu!
TUJIFUNZE ZAIDI:
Wapo ambao wakitongozwa na wanaume ambao wanaona wazi kuwa (mmoja wao) hampendi, lakini akawa na mali au uwezo mkubwa kifedha, huamua kumkubali kwa lengo la kupata vitu vya mwanaume huyo.
Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajifunza kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo, jambo ambalo si sahihi na halijawahi kutokea.
Angalia mawazo ya baadhi ya wasichana: “Pesa anazo, magari anayo, hata kama simpendi nitajitahidi kumpenda taratibu. Maisha mazuri kwake nitapata, wasiwasi wa nini?”
Ndivyo wanavyowaza. Haya ni mawazo potofu. Baada ya wazo hili kuingia akilini, huwa hana muda wa kusubiri zaidi, anakubali na wakati mwingine huweza kuingia katika ndoa ya chapuchapu. Mwisho wa ndoa hiyo hauwezi kuwa mzuri hata kidogo.
ANGALIA MADHARA:
Yapo madhara mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi wako uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati ambalo ndiyo msingi wa maisha. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.
adhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katika uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati! Unajua kitakachotokea? Kama hutaleta magonjwa ndani basi siku moja utafumaniwa.
Siku hiyo lazima utafukuzwa nyumbani kwa mwanaume huyo, na kama ana hasira, anaweza kukuua.
Fikiria zaidi juu ya siku hiyo. Upo tayari kwa aibu au fedheha hiyo? Jibu lako litakupa mwanga wa kuendelea kusoma kipengele kinachofuata.
UNAUTENDEA HAKI MOYO WAKO?
Kamwe usijaribu kuingia katika mkumbo huu, mkumbo wa kujifunza kupenda ndani ya uhusiano. Ni jambo gumu ambalo huweza kuharibu maisha yako kabisa.
Jambo ambalo linaweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa. Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo.
Maisha yako wewe mwenyewe, lazima ujichagulie maisha mazuri, matamu, yenye furaha yasiyo na huzuni. Uamuzi upo mikononi mwako. Unataka maisha ya aina gani? Chagua mwenyewe.
Bila shaka kuna kitu kipya ulichojifunza na utachukua hatua kwa kuanza maisha mapya kifikra kutokea hapa.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
No comments:
Post a Comment