Na Hans Mloli
KIPINDI cha usajili ndiyo muda wa wachezaji pia kutafuta mahali pa kutokea kwa ajili ya msimu ujao ambapo hali imekuwa tete Yanga baada ya kupokea barua na maombi kibao kutoka kwa wachezaji wanaotaka kuwa ndani ya kikosi cha Yanga msimu ujao.
Chanzo makini kutoka Yanga kimeliambia Championi Jumatano kuwa, mpaka sasa uongozi wa Yanga umeshapokea barua lukuki kutoka kwa wachezaji wanaotokea sehemu mbalimbali lakini bado hawajajibiwa.
“Barua kibao za wachezaji zimeshatumwa Yanga wakiomba kuichezea timu hiyo msimu ujao lakini mpaka sasa bado hazijajibiwa kwa sababu Yanga haijapanga kutafuta mchezaji kwa njia kama hiyo.
“Kiukweli sidhani kama kuna hata mmoja ambaye atajibiwa kutokana na mipango iliyowekwa, wapo wengine wanakuja na watu wao kutoka mikoani wanawaleta ofisini pale kwa ajili ya usaili, yaani kwa kifupi ni wengi mno wanaoitaka Yanga,” kilisema chanzo.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, kulitolea ufafanuzi suala hili, alikiri kuwepo kwa hali hiyo lakini akasema si muda wake kwa sasa kulizungumzia.
“Barua za maombi kwa wachezaji wanaotaka kuichezea Yanga zimefika hapa lakini siwezi kukutajia idadi yake au kwamba mchakato upo vipi kwa sababu muda wake wa kulizungumzia hilo haujafika,” alisema Njovu.
No comments:
Post a Comment