ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 13, 2014

BAJETI 2014/2015: Kodi ya mishahara yapungua kiduchu, mishahara juu


Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya akionyesha mkoba uliobeba Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Dodoma. Kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi nchini kutaka Kodi ya Mshahara (Paye), ipunguzwe hadi chini ya asilimia 10 kimekwama baada ya Serikali kupunguza kodi hiyo kwa asilimia moja.
Hata hivyo, Serikali katika bajeti yake ya 2014/15 iliyosomwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya imetangaza ongezeko la
kima cha chini cha mishahara ambacho kiwango chake hakikubainishwa.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jana, Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum alisema katika mwaka huo unaoanza Julai Mosi, mwaka huu Serikali inakusudia kufanya marekebisho katika mfumo wa ‘Paye’ kwa kupunguza kiwango cha kodi kutoka asilimia 13 hadi 12.
Iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa na Bunge, wafanyakazi watapata unafuu kiduchu wa kodi ambao ni sawa na Sh1, 900.
Kodi hiyo ya mishahara imekuwa kitanzi kwa wafanyakazi na Rais Jakaya Kikwete alipohutubia taifa katika sherehe za Mei Mosi, Mwaka huu aliahidi kuendelea kushughulikia kilio hicho kadri mapato ya Serikali yanavyoruhusu.
“Kumekuwepo pia na ombi la muda mrefu la kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi kuwa chini ya asilimia 10. Kama nilivyoahidi mwaka jana, hili tutaendelea kulishughulikia kadri uwezo wa Serikali utakaporuhusu.
“Tumeshafanya hivyo kabla na hatuna sababu ya kutofanya hivyo huko tuendako. Tayari tumepunguza kutoka asilimia 18.5 mwaka 2007 hadi asilimia 13 hivi sasa. Maombi yenu tumeyapokea, tuachieni, tuangalie nini tunachoweza kufanya kama miaka iliyopita.”
Rais Kikwete alisema kinachokwamisha punguzo hilo kufikia tarakimu moja ni uwezo mdogo wa mapato ya Serikali.
Kima cha chini
Katika hotuba hiyo ya bajeti, Waziri Mkuya alitangaza mpango wa Serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma lakini hakutaja ongezeko hilo litakuwa la kiwango gani.
Suala la ongezeko la mishahara pia lilielezwa na Rais Kikwete wakati wa Mei Mosi, alipobainisha uwezekano wa nyongeza ya mwaka huu kuwa kubwa kuliko ya mwaka jana.
“Najua kuwa nyongeza tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata mimi nisingependa iwe hivyo.”
Rais Kikwete alibainisha kuwa kwa nyongeza iliyofanywa mwaka jana, hivi sasa Serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti kulipa mishahara, sawa na asilimia 10 ya Pato la Taifa.
Mwaka jana Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 41 kutoka Sh170,000 hadi Sh240,000... mwaka huu nawaahidi tena kuwa tutaongeza,” alisema Rais Kikwete.
Akifafanua namna Serikali ilivyofikia uamuzi wa kuongeza mishahara hiyo, Rais Kikwete alisema kulikuwa na mjadala mkali baina ya wafadhili waliodai nyongeza ni kubwa mno.
“Ni kweli mapato yetu ni madogo lakini kwa kuwa mishahara ni midogo, lazima tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo lazima ukitoe ili uijenge ile nafuu, alisema bila kutaja kiwango kitakachoongezwa.
“Hata sasa kumekuwa na ubishi mkali kati ya Wizara ya Utumishi na Hazina kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi gani, nikaingilia kati nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa wanataka ipingue kidogo,” alisema.
Pensheni kwa wazee
Katika eneo la masilahi ya watumishi, Serikali pia inakusudia kuongeza pensheni za wastaafu ili kuhakikisha wanapata viwango ambavyo vinaendana na uhalisia.
Waziri Mkuya alisema wastaafu hao wako wa aina mbili; wale ambao hawakuchangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wanaolipwa Sh50,000 kwa mwezi na wale ambao pensheni zao zinategemea michango yao katika mfuko husika.
“Serikali inatambua kuwa viwango vinavyolipwa kwa sasa haviendani na uhalisia. Katika kutatua changamoto hii, Serikali inapitia viwango hivyo ili kuongeza viwango kutegemeana na mapato ya Serikali na kuhakikisha malipo yanafanyika kwa wakati,” alisema.
Vilevile, Waziri Mkuya alisema Serikali kwa kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendelea kuhuisha kanuni za ukokotoaji wa mafao ili kuweka ulinganifu wa mafao katika mifuko hiyo.

1 comment:

Anonymous said...

tumeshamtabua kitambo huyu msaka tonge mnafiki mzandik