ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 17, 2014

JK KUWALETEA USHER RAYMOND NA TREY SONGZ HABARI NDIYO HIYO

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete amesema atawaleta nchini wasanii nyota wa muziki kutoka Marekani kwa ajili ya kuja kutoa burudani na kuzungumza na wasanii wa muziki na filamu nchini Julai mwaka huu.

Kikwete maarufu kama JK, aliyasema hayo wakati akihutubia wasanii, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa pamoja na maelfu ya wananchi waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa usiku wa kuamkia jana.
Alisema ziara yake iliyopita nchini Marekani, ambayo alikutana na msanii aliyezoa tuzo saba za Kilimanjaro Music mwaka huu, Nassib Abdul 'Diamond Platnumz', ilikuwa na mafanikio makubwa.

"Hivi karibuni nilikuwa Marekani, tulianzia Canada kwenye mkutano wa jitihada za kimataifa za kuzuia vifo vya kinamama wajawazito, watoto wachanga na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Nilipitia New York nikamkuta Diamond anatumbuiza," alisema Kikwete na kuongeza:

"Nikamkaribisha hotelini, tukala wote chakula. Akanieleza kwamba amepata 'nomination' (uteuzi) mbili. Amepata 'nomination' ya MTV Africa Music Awards lakini pia amepata 'nomination' ya Black Entertainment Television (BET) ya Marekani.

"Ile 'nomination' ya MTV Africa Music Awards amekwenda kule hakuibuka mshindi lakini alitumbuiza pale na sisi tulikuwa tunaangalia tumemuona amefanya kazi kubwa, nzuri na watu walisisimka sana. Amelitangaza jina la Tanzania.

"Nadhani Julai 27 ndiyo wanafanya zile tuzo za Black Entertainment za kila mwaka. Diamond amewekwa kwenye kundi la kufikiriwa kupewa tuzo, hii yenyewe ni mafanikio. Diamond unatutoa kimasomaso bwana, tunakushukuru sana," alisema zaidi JK.

Aliendelea kueleza kuwa kutokana na kufahamiana kwake na wasanii wakubwa duniani, alimuunganisha Diamond na wasanii wakubwa na 'vigogo' waliowalea na kuwakuza wasanii wakubwa kama Jay Z wa Marekani.

"Siku moja nikamwambia Diamond nitakusaidia kukutambulisha kwa wakubwa wa hii sanaa hii ya muziki duniani. Yupo jamaa aliyewalea kuwainua baadhi ya wasanii wakubwa wa Marekani kina Jay Z," alisema.

Alisema magwiji hao wa muziki duniani kutoka Marekani wanatarajiwa kutua nchini Julai 11 mwaka huu kwa ajili ya shughuli hiyo waliyokubaliana ikiwamo kuwapa mwongozo wasanii wa hapa wa namna ya kupambana kuelekea kwenye mafanikio.

JK aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa video hiyo iliyoshirikisha wasanii kibao wa Tanzania, alisema anawapenda sana wasanii huku akiwakaribisha kwa mazungumzo na chakula Ikulu.

Alisema amependezwa na wazo la kutunga wimbo huo huku akiwataka Watanzania kutimiza wajibu wa kulinda nchi yao kwa kuwa inafitinishwa na kuchukiwa na wengi.

"Tulizaliwa Watanzania, tunaishi Watanzania, tutakufa Watanzania na tutazikwa Watanzania. Ni wajibu wetu wa kwanza kuipenda nchi yetu, kuithamini nchi yetu na kuwa tayari kujitolea kwa maendeleo, ustawi na usalama wake," alisema JK.

"Asilimia 91 ya Watanzania waliopo sasa walizaliwa baada ya Aprili 26, 1964. Lakini zaidi ya asilimia 78.6 ni Watanzania walio chini ya miaka 35. Hamkuwapo wakati TANU na ASP zinazawaliwa lakini kama Watanzania mnao wajibu wa kutetea na kulinda maslahi ya nchi," alisema.

MASLAHI WASANII
JK, ambaye aliweka wazi kwamba enzi za ujana wake alikuwa mpenzi mkubwa wa muziki wa dansi, alisema Serikali imeanza kuboresha taratibu za mauzo ya kazi za wasanii ili kuzuia hujuma zinazoikumba tasnia hiyo.

"Ninatambua mnafanya kazi kubwa na nzuri lakini haijawanufaisha vya kutosha. Nilitumia Sh.milioni 20 kumtafuta mtaalam mwelekezi kutoka chuo kikuu kutengeneza taratibu za kusambaza kazi zenu ili mpate malipo ya haki kwa jasho lenu.

Tumeshirikisha na TRA (Mamala ya Mapato Tanzania), tumeshirikisha Posta na tumeanza kuweka stika kwenye kazi zenu," alisema JK.

Alisema tayari Serikali imewajenga studio mpya kwa zaidi ya Sh.milioni 40 kwa lengo la kusaidia wasanii nchini.

Katika uzinduzi wa video ya wimbo huo alikuwa amefuatana na viongozi wengine wa Serikali wakiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinga, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, Mwenyekiti wa Kambi Rasmi Bungeni, Freeman Mbowe, Spika wa Bunge, Anne Makinda na mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere.

Awali akizungumzia uzinduzi wa video hiyo kwa niaba ya wasanii, rapa wa kundi la Weusi, Nicki wa Pili, mwenye shahada ya uzamili, alisema wamelenga kutembea nchi nzima kuhamasisha uzalendo.

1 comment:

Anonymous said...

KUMBUKA MZEE MZIMA AHADI NI DENI... BADO TUNAWASUBIRI BARCELONA