ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 23, 2014

Kiwanda cha ‘Kichina’ chabainika Dar

Dar es Salaam. Raia mmoja wa China anadaiwa kumiliki kiwanda bubu cha samani na vifaa vingine vya ujenzi katika eneo la Tabata-Segerea, Mtaa wa Migombani, Dar es Salaam.
Kiwanda hicho kinachoitwa L&J Engineering kilichopo katikati ya makazi ya watu, kinaendesha shughuli zake kwa usiri, bila kutoa stakabadhi na hata baadhi ya wakazi wa eneo hilo wanadhani nyumba inayohusika ni makazi tu ya Wachina.
Mwandishi wetu alinunua mito miwili iliyotengenezwa kwa pamba, kila mmoja ukiuzwa kwa Sh7,000 lakini alipodai risiti aliambiwa kwamba hawatoi risiti kwa bidhaa ndogondogo.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kiwanda hicho kimeliingizia hasara ya Sh30.4 milioni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutokana na wizi wa umeme.
Kaimu Meneja wa Tanesco Mkoa wa Ilala, Ahmed Mmingwa alisema baada ya kufanya tathmini katika mita ya nyumba kilipo kiwanda hicho, walibaini kuwa imechezewa.
“Tumepata hasara ya Sh30,388,853.42 kutoka katika kiwanda hicho pekee. Sasa tutawapelekea barua ili walipe deni hilo,” alisema.
Ofisa Usalama wa Tanesco Mkoa wa Ilala, John Chirare aliyegundua kuchezewa huko, alisema baada ya kufuatilia usajili, walibaini kuwa mita hiyo imesajiliwa kwa jina la Dk Kwayo kama nyumba ya kuishi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Masoko wa L&J Engineering, Meshack Lakati alisema walipanga katika nyumba hiyo siku nyingi na mita haikuwahi kubadilishwa.
Alisema inawezekana mita ndiyo yenye tatizo na kwamba wao hawajafanya hila zozote za kutumia umeme huo kwa shughuli zao. Alisema bidhaa zinazotengenezwa kiwandani hapo hazitumii umeme mkubwa kwa sababu ni za kawaida ambazo hutengenezwa pia katika maeneo mengine.
“Kampuni yetu inalipa ankara ya umeme kila mwezi, hatujawahi kuchezea mita. Lakini kwa kuwa Tanesco wamebaini kuwa mita haiko sawa, basi itakuwa na tatizo kwa vile imetumika muda mrefu bila kubadilishwa,” alisema.
Licha ya tatizo hilo la mita, kiwanda hicho kinadaiwa kuendeshwa kinyemela bila ya kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela). Mwandishi wetu alipitia usajili wa kampuni hiyo Brela ili kujua imesajiliwa kwa shughuli zipi, lakini haikuonekana.
Hata hivyo, Lakati alipinga madai ya kutokusajiliwa akisema kiwanda hicho hakiwezi kufanya biashara zao bila ya kuwa na usajili kutoka Brela. Hata hivyo, alipotakiwa kutaja namba ya usajili alisema hahusiki na hilo kwa kuwa lipo katika mamlaka nyingine.
Katika kiwanda hicho, shughuli kubwa zinazofanyika ni utengenezaji wa vitanda na magodoro ya ‘spring’, makabati ya kisasa, meza za ofisini kwa mbao kutoka nje, sofa, mito ya pamba, madirisha ya aluminiamu na mashuka.
Mbali na shughuli hizo, kampuni hiyo pia inajishughulisha na uchimbaji wa visima virefu.
Mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo (jina limehifadhiwa), alisema malighafi za bidhaa zao huagizwa kutoka China na wanatengeneza wenyewe na kuuza kwa watu binafsi au kwa kampuni mbalimbali.
Alisema wanapokea ‘oda’ kutoka kwa wateja wao na kuwatengenezea bidhaa wanazozitaka. Bei ya bidhaa hizo zinakuwa chini kiwandani hapo ukilinganisha na pale bidhaa hizo zinapopelekwa sokoni.
“Hii mito tunatengeneza hapahapa. Tunaagiza pamba kutoka China, lakini mambo mengine yanafanyika hapa,” alisema mfanyakazi huyo wakati akiuza mito hiyo.
Ilidaiwa kuwa malighafi hizo huingizwa usiku au alfajiri ili kukwepa kujulikana kwa kiwanda hicho na kazi kubwa hufanyika usiku na mchana wanafanya kazi za kawaida.
Soko la bidhaa
Kiwanda hicho kinazalisha bidhaa kwa oda maalumu kutoka katika hoteli kubwa, ofisi mbalimbali na maduka makubwa ya samani ndani na nje ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja ndani ya kiwanda hicho, seti moja ya sofa inauzwa kuanzia Sh1.5 milioni kiwandani hapo, lakini inapofika sokoni huuzwa kwa kuanzia Sh3 milioni na kuendelea.
Vitanda vya ‘spring’ vinavyotengenezwa katika kiwanda hicho vyenye ukubwa wa futi 5x6, vinauzwa kwa Sh480,000 na godoro lake la ‘spring’ likiuzwa kwa Sh400,000.
Hoteli mbalimbali zinazofunguliwa Dar es Salaam na mikoani zimekuwa zikinunua samani kutoka katika kiwanda hicho.
MWANANCHI

No comments: