ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 23, 2014

‘SOMETIMES’ UONGO UNAHITAJIKA KWENYE MAPENZI!-2

FUNGUA ubongo wako sasa, maana muda wa kujifunza kuhusu uhusiano na mapenzi umewadia. Huwezi kukwepa kujifunza, ukifanya hivyo utabaki na mawazo yaleyale kila siku.

Inawezekana kwa uelewa wako kuna mambo ambayo unayafahamu kuhusu mapenzi, lakini kwa kuwa mdau wa kona hii, unaongeza kitu kingine kipya kila siku.

Naam! Sasa nipo tayari kuendelea na mada yetu iliyoanza wiki iliyopita. Nazungumzia juu ya uongo wenye manufaa kwenye mapenzi. Rafiki zangu, nilipata wakati mgumu sana kwa kupokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wasomaji wangu baada ya sehemu ya kwanza ya mada hii wiki iliyopita.


Nilibadilishana mawazo na wengi kwa kadiri muda ulivyoruhusu, lakini mwisho wa yote niliwashauri kwamba wavute subira hadi leo katika mwendelezo wake ambapo nina majibu ya maswali yote.
Hebu sasa twende tukaone uongo ambao unakubalika na hauna madhara zaidi ya kujenga uhusiano. Rafiki zangu, kuna wakati ukweli unaweza kuharibu!

WENZI WALIOTANGULIA
Nani amewahi kuwa mkweli kwa mpenzi wake mpya kuhusu idadi ya mapatna aliowahi kutoka nao kimapenzi?

Hebu anza na wewe mwenyewe? Jiulize, tangu umeanza mapenzi umetoka faragha na wanaume/wanawake wangapi? Je, upo tayari kumtajia mpenzi wako?

Umewahi kufanya hivyo? Rafiki zangu, kati ya mambo ambayo yanaudhi sana katika mapenzi ni pale mpenzi anapogundua kwamba mwenzi wake ni jalala, yaani ametoka na wapenzi wengi kabla yake.
Wengi wanatamani sana kusikia kwamba wao ni wa pili au tatu, vinginevyo akutane na mwanamke ambaye bado hajaanza kabisa mambo ya mapenzi. Rafiki zangu, tuwe wakweli, kumwambia mpenzi wako kwamba umeshatoka kimapenzi na wanaume hamsini, ni sawa na kumtangazia kwamba wewe ni mhuni uliyeshindikana.

Hata kama ni kweli umetoka na idadi hiyo, akikuuliza ipunguze, mwambie yeye ni mwanaume wako wa nne! Wa kwanza, alikutoa usichana ukiwa mwanafunzi, baada ya hapo ukaachana naye kabisa na mapenzi.

Mwingine ulikutana naye chuo, ukamuacha baada ya kugundua kwamba alikuwa akipenda kukutumia tu, wa tatu ulifuma meseji ya mapenzi kwenye simu yake ukaamua kumuacha, yeye ni wa nne!
Mwanaume huyo atajisikia fahari sana kuwa na mwanamke mwenye namba ndogo ya wanaume aliotembea nao, ingawa moyoni mwako unaujua ukweli, lakini inabidi udanganye ili kulinda penzi lako. Tupo pamoja jamani?

UGOIGOI FARAGHA
Ukiwa na mpenzi wako, si ajabu katika mazungumzo yenu ya kawaida, akakuuliza kuhusu uwezo wako wa kucheza ‘ligwaride’ muwapo faragha. Kwa bahati mbaya kuna rafiki wenye matatizo ya hapa na pale faragha.

Baadhi ya wanawake husumbuliwa na tatizo la maumivu wakati wa tendo, kuchelewa kufika mshindo na hivyo kuachwa njiani au kupoteza hamu ya tendo.

Wanaume wao husumbuliwa na tatizo la kufika mshindo mapema, kushindwa kurudia tendo na kuchoka mapema wakati mwenzake akiwa bado angali anamuhitaji.

Kimsingi matatizo makubwa hapa husababishwa na utayari wa kisaikolojia, maandalizi duni n.k. Unapozungumza na mwenzako kuhusu hili, hutakiwi kumpa taarifa za kweli.

Zipo athari kadha wa kadha za kuwa mkweli juu ya matatizo uliyonayo katika eneo hili. Kubwa zaidi, unajiongezea tatizo, maana utakuwa unaingia uwanjani ukiwa unajua kabisa kwamba mpinzani wako anajua udhaifu wako hivyo ni rahisi kukushinda!

Matatizo ya aina hii hutibiwa zaidi na mtu mwenyewe, kugundua udhaifu wake na kuufanyia kazi. Kama umegundua kwamba unapata maumivu wakati wa tendo, ni wazi kwamba maandalizi si ya kutosha, dawa yake hapo ni kutumia muda mwingi katika maandalizi kabla ya kuanza kazi yenyewe.

Kueleza tatizo lako moja kwa moja, kutamfanya mwenzako awe na mawazo, akiamini kwamba ama hutaendana na kasi yake, hatakufurahisha au utamuacha njiani. Kwa mtazamo huo ni rahisi sana kufikiria kuachana na wewe ili akatafute anayeendana naye.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

GPL

No comments: