ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 12, 2014

Maelezo ya kina kuhusu Majambazi yalivyovamia kituo cha Polisi na kupora bunduki 5

Walikuwa na mapanga, waua Polisi na kujeruhi

Kamishina wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja

Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia Kituo kidogo cha Polisi cha Mkamba kilichoko katika Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani na kumuua askari polisi, kuwajeruhi wanamgambo wawili, kupora bunduki tano, mbili aina ya Sub Machine Gun (SMG) zenye risasi 60 na bunduki tatu aina ya shotgun zilizokuwa zimehifadhiwa ghalani.

Majambazi hao sita, walivamia kituo hicho wakiwa na mapanga waliyotumia kumuulia askari na kuwajeruhi wanamgambo hao usiku wa kuamkia jana.
Silaha walizopora majambazi hao, zilikuwa zikisubiri kupelekwa katika kituo kikubwa cha polisi chenye ghala kuu kwa ajili ya hifadhi.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishina wa Polisi wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7:00 usiku katika Kituo kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo kijiji cha Kimanzichana wilayani Mkuranga.

Kamanda Chagonja alifafanua kuwa bunduki mbili za SMG zilizoporwa na majambazi hao kila moja ilikuwa na risasi 30 kwenye magazini. Aidha, alimtaja askari polisi aliyeuawa kwa mapanga katika tukio hilo kuwa ni D 9887 Koplo Joseph Ngonyani.

Kamanda Chagonja alisema askari huyo alifariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga ambako alipelekwa kwa matibabu.
Kadhalika, aliwataja wanamgambo waliojeruhiwa katika uvamizi huo kuwa ni Venance Francis na Mariamu Mkamba.

Kamanda Chagonja alisema wanamgambo hao kwa sasa wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Jeshi la Polisi nchini limelaani vikali kitendo hicho na kuanzisha msako mkali dhidi ya majambazi hayo ili yafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Kamanda Chagonja aliongeza kuwa pia jeshi hilo litahakikisha kuwa silaha walizopora majambazi hayo zinapatikana haraka.
Aidha, Jeshi la Polisi nchini limetoa wito kwa wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki huku wakitoa ushirikiano ili kufanikisha kuwatia mbaroni majambazi hayo.

Pia limewaomba raia wema wenye taarifa za wahalifu kutoa taarifa kupitia namba ya simu 0754 785557 ama namba ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, 0715 009953 au katika kituo chochote cha polisi cha jirani.
 

CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

So sad!! Tunakwenda wapi watanzania?? Tumefikia hatua hiyo.mhhh