Emmanuel Mbasha, ambaye ni mume wa
mwimbaji nguli wa nyimbo za Injili, Flora
Mbasha amejitokeza hadharani na kusema
kwamba atakwenda polisi mwenyewe
kujibu tuhuma dhidi yake za kumbaka
Faili la tuhuma dhidi ya
Mbasha lilifunguliwa Jumatatu iliyopita
katika Kituo cha Polisi Tabata (Tabata Shule)
wakati shemejiye huyo (jina tunalihifadhi),
alipotaarifu kuwa Mbasha alimbaka mara
tatu kwa siku mbili tofauti. Kesi hiyo ilipewa
namba TBT/RB/3191/2014 na TBT/
IR/1865/2014.
Tangu siku hiyo, polisi imekuwa ikieleza
kuwa inamsaka Mbasha bila ya mafanikio
lakini mwishoni mwa wiki mtuhumiwa
huyo aliongea na gazeti hili na kuelezea
upande wake wa tukio hilo na kwamba
yuko tayari kujisalimisha ili ukweli ubainike.
"Tuhuma dhidi yangu ni za kutengeneza,"
alisema Mbasha na kufafanua kuwa yote
hayo yanatokana na mgogoro wa kifamilia
baina yake na Flora na familia yake ambao
alisema umedumu kwa siku kadhaa.
"Mimi sijabaka na sijawahi kubaka;
sijatenda dhambi yoyote; sijafanya kitu
chochote na kibaya haya mambo yote ni ya
kusingiziwa tu. Mungu wangu ni shahidi.
Na kwa kuwa sijafanya hiyo dhambi kama
wanavyodai, basi Mungu wangu
atanitetea," alisema Mbasha ambaye
anaonekana zaidi kwenye video ya wimbo
wa Maisha ya Ndoa alioshirikiana na
mkewe Flora.
"Si wamesema wananitafuta, nitakwenda
mwenyewe polisi. Nitawasikiliza na nitatoa
maelezo yangu. Kama wakinipeleka
mahakamani basi ukweli utajulikana… ipo
siku kila kitu kitakuwa wazi."
Kabla ya kufunguliwa kwa faili la tuhuma
hizo, msichana huyo alipelekwa Hospitali ya
Rufaa ya Wilaya ya Ilala (Amana) ambako
alifunguliwa faili la matibabu namba 667.
Matokeo ya vipimo ambavyo vilifanywa na
daktari kung'amua kama binti huyo
aliingiliwa vinaonyesha kuwa kulikuwa na
mbegu utokaji wa mbegu usio wa kawaida
(HVD).
Kadhalika binti huyo alifanyiwa vipimo
kuona kama ameambukizwa virusi vya
Ukimwi (VVU), pia kupata ujauzito, lakini
matokeo ya awali yalionyesha kuwa yupo
salama.
Akiwa nje ya kituo cha polisi Jumatatu
usiku, binti huyo aliliambia gazeti hili
kwamba mara ya kwanza alibakwa mchana
Mei 23 na kwamba mtuhumiwa alirudia
kitendo hicho Jumapili Mei 25 usiku ndani
ya gari katika eneo la Tabata, ambako
anadai alifanyiwa kitendo hicho mara mbili.
Hata hivyo, Mbasha alihoji: "Hivi kweli hata
kama mimi ni mbakaji, kweli nimbake
mtoto wa kumlea mwenyewe mara tatu,
yaani Ijumaa halafu nirudie tena Jumapili?
Hata kama ni kusingiziwa basi tuhuma hizi
zimezidi."
"Huyu binti nimekaa naye miaka mingi na
sijawahi kumfanyia hivyo. Hapo nyumbani
kwangu wamekaa mabinti wengi,
wakiwamo shemeji zangu wadogo zake na
Flora na sikuwahi hata kuwagusa, leo hii
kwa nini wananifanyia hivi?"
Mgogoro wa familia
Mbasha alidai kwamba chanzo cha
kusingiziwa kwake ni mgogoro baina yake
na mkewe Flora, ambao umesababisha
mgawanyiko mkubwa ambao umefanya
achukiwe na familia nzima ya mkewe.
"Yako mambo mengi tu ambayo yanahusu
familia, kwa hiyo ilifika mahali mimi na Flora
tukawa hatuishi kwa amani na hata hili
jambo limetokea wakati tukiwa na
mgogoro huo. Hivyo Flora na ndugu zake
waliamua kumlisha binti huyo maneno ili
mimi nifungwe," alisema Mbasha.
Hata hivyo, Flora hakutaka kuingia kwa
undani katika suala hilo, akisisitiza kuwa
Mbasha bado ni mumewe na kwamba
yaliyotokea awali alishamsamehe, lakini
akamtaka ajitokeze kutoa maelezo polisi.
"Mimi nilishamwambia kwamba hata kama
alifanya au hakufanya, nilishamsamehe
kutoka ndani ya moyo wangu maana yeye
ni mume wangu wa ndoa na Mungu wangu
ni shahidi, lakini kuna suala la kisheria polisi
ambalo mimi siwezi kuliingilia," alisema
Flora ambaye alitamba na wimbo wa injili
wa "Tanzania" ambao ulimfanya aalikwe
katika shughuli mbalimba za kitaifa.
"Tatizo linakuwa kubwa kwa sababu yeye
mwenyewe haonekani na taarifa ni
kwamba amekimbia," alidai Flora. "Sasa
kama kweli hajafanya kitendo hicho, kwa
nini anajificha? Ajitokeze… aende polisi na
huko ndiko akatoe maelezo yake.
Kuzungumza na vyombo vya habari
haisaidii kabisa."
Mwimbaji huyo, ambaye ni mjukuuu wa
muhibiri maarufu wa Injili, Askofu Moses
Kulola alisema yeye hana uwezo wa
kuingilia kesi hiyo kwani hakuhusika kwa
namna yoyote ile kupeleka suala hilo polisi
kwa sababu hakuwapo wakati likitokea na
kwamba linasimamiwa na familia.
"Inawezekana anatamani nikafute kesi
polisi, mimi sina uwezo huo kwa sababu ni
suala la kisheria na tuhuma zenyewe ni za
kijinai. Pili familia yenye mtoto ndiyo
inafuatilia kesi hiyo, lakini hilo halifuti
msamaha wangu kwake," alisisitiza.
Kauli ya Flora kwamba ameshamsamehe
mumewe inafanana na ya Mbasha ambaye
pia alisema kwamba kama kuna jambo
ambalo mkewe alimkosea, hana tatizo na
kwamba alishamsamehe.
"Flora ni mke wangu, mke wa ujana
wangu, ninampenda asilimia 100 na yeye
analifahamu hilo, lakini sijui ni kitu gani
kimemkuta? Sijui ni nini kimeingilia ndoa
yetu?" alisema Mbasha.
Alisema ameshampigia simu mkewe mara
nne akitaka waonane ili wazungumze,
lakini hakuonyesha utayari, kauli ambayo
Flora aliikanusha akisema: "Hajanitafuta
maana tangu Jumatatu hapatikani kwenye
simu."
Mwenendo wa upelelezi
Wakati hayo yakiendelea, maendeleon ya
kesi hiyo yanasuasua baada ya faili
kutokupelekwa Kituo cha Polisi Buguruni
kutoka Tabata kwa ajili ya hatua zaidi.
Baadhi ya wanafamilia wa mtoto
anayedaiwa kubakwa walisema jalada hilo
lingefikishwa Buguruni Jumatano jioni,
lakini kutokana na ofisa anayeshughulikia
kesi hiyo kuwa na udhuru, ilishindikana.
Mjomba wa Flora ambaye amepewa jukumu
la kusimamia kesi hiyo, alisema wamekuwa
wakifuatilia Kituo cha Polisi cha Tabata
tangu tukio hilo liliporipotiwa, lakini
wakaelezwa kuwa kesi hiyo itahamishiwa
Buguruni.
"Tuliambiwa lile faili lazima lihamie kituo
cha Buguruni. Nilifika hapa nikaonana na
kamanda wa polisi wa wilaya ambaye
ametupokea vizuri na kuonyesha moyo wa
kutusaidia," alisema.
Kamanda wa polisi wa Ilala, Marietha
Minangi alisema bado wanaendelea na
uchunguzi wa kesi hiyo na kwamba
hafahamu taarifa kuwa faili hilo
linacheleweshwa kuhamishiwa Buguruni.
"Tunaendelea kuchunguza, ila siyajui hayo
masuala ya faili yanayotoka kinywani
mwako. Lakini nimepata taarifa kuwa bado
wanachunguza," alisema Minangi.
Mwanzoni mwa wiki jana, Kamanda
Minangi alisema kuwa maofisa wake
walikuwa wanaendelea kumsaka
mtuhumiwa na kwamba walienda mpaka
nyumbani kwake, lakini hawakumkuta.
"Nimefuatilia ni kweli hiyo kesi
imefunguliwa na maofisa wangu
wameniambia walienda nyumbani kwake
na hawakumkuta mtu. Waliniambia walikaa
pale kwa takribani dakika 20 na ile nyumba
ina fence (uzio) na geti waligonga kengele,
lakini hakuna mtu aliyekuja kufungua.
"Na baadaye waliwauliza majirani, nao
wakasema hawafahamu mtu huyo alipo.
Inaonekana ametoweka, lakini sisi kama
wasimamizi wa sheria tunaendelea
kumtafuta mpaka tutakapomkamata,"
alisema Minangi.
Ustawi wa Jamii
Kesi hiyo pia inafuatiliwa kwa karibu na
Idara ya Ustawi wa Jamii ya Manispaa ya
Ilala kujua usalama na matibabu ya binti
huyo. Ofisa ustawi wa jamii
anayeshughulikia ulinzi na usalama kwa
mtoto wa manispaa hiyo, Fransica Makoye
alisema kuwa wanalishughulikia suala hilo
kama mengine katika kutafuta haki na
usalama wa mtoto na wala hawahusishi na
umaarufu wa wahusika.
"Sisi tunafuatilia kama alipata tiba sahihi
mara baada ya tukio la kubakwa na
kufahamu mahali ambako anakaa kwa ajili
ya usalama wa huyo mtoto. Tumeiona PF3
haionyeshi kama alipata matibabu, lakini
tutawajulisha zaidi kinachojiri kwa kuwa
tutaenda Hospitali ya Amana kwa maelezo
zaidi," alisema Makoye.
Credit:BossNgassa
No comments:
Post a Comment