Mshambuliaji wa Lille ya
Ufaransa , Mkenya Divorc Origi ambaye ni mzaliwa wa Ubelgiji ni miongoni
mwa wachezaji wa timu ya taifa ambayo imeondoka Jumanne kuelekea Brazil
kwa mashindano ya kombe la dunia kuanzia Alhamisi wiki hii.
Origi, mwanae Mike Okoth, mchezaji wa zamani wa
timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars atakua mchezaji wa kwanza wa
Afrika Mashariki kuiwakilisha Ubelgiji, na yuko pamoja na wachezaji
nyota kama vile Vincent Kompany wa Manchester City na Eden Hazard wa
Chelsea. Akizungumza na BBC kwa njia ya
simu akiwa Ubelgiji Origi anasema:'' Algeria ni timu yenye wachezaji wazuri kwa hivyo hatuwezi kuidharau. Tutacheza mchezo wetu wa kawaida lakini nina matumaini makubwa tutashinda.’’ Anasema Urusi na Korea pia si timu hafifu hasa Warusi. Lengo lake kubwa ni Ubelgiji kufuzu kwa raundi ya pili kisha kutoka hapo anasema mambo yatakuwa sawa kabisa.
Kuhusu mbona ameamua kuiwakilisha Ubelgiji na sio taifa la babake Kenya, Origi anasema alitilia maanani mambo mengi kama vile usimamizi mzuri wa kandanda nchini humo, mizizi yake ya kandanda iliyoko huko, marafiki, ushauri wa babake pamoja na Ubelgiji kufuzu kwa kombe la dunia kwani haijulikani ni mwaka upi Kenya itafuzu kwa kombe la dunia.
Namuuliza Okoth kama kuna siku Harambee Stars itafuzu kwa kombe la dunia? ''Itakua vigumu sana kwao kufuzu kwa kombe la dunia kama usimamizi ni duni bado,’’ anasema Okoth, na kuongezea:''Tena wanahitaji wawe wakicheza na timu mashuhuri duniani mara kwa mara. Sio kwamba ni vigumu kufuzu lakini lazima pia serikali nayo ikubali kutumia fedha kulipia mechi kubwa za kimataifa na tuwe na msingi mzuri wa kandanda kuanzia mashinani.’’
Origi, mwenye umri wa miaka 19, anasema amefurahia sana kuchaguliwa kuiwakilisha Ubelgiji kwenye kombe la dunia, na vile vile kuwa na mshambuliaji mahiri Romelu Lukaku wa Chelsea ambaye msimu uliopita alichezea Everton kwa mkopo.
Mara ya mwisho Ubelgiji kushiriki kombe la dunia ni mwaka wa 2002 ambapo kocha wao wa sasa Marc Wilmots alikuwa mchezaji wa mwisho kuifungia Ubelgiji kwenye kombe la dunia hadi sasa. Wilmots ana imani na Origi ambaye amechukua nafasi ya Christian Benteke wa Aston Villa anayeuguza jeraha.
Urusi ndio tisho kubwa kwa Ubelgiji kumaliza katika nafasi ya kwanza kundi H, na ina motisha wa kufanya vyema kwani wao ndio wataanda kombe la dunia mwaka wa 2018. Isitoshe Urusi inafunzwa na kocha anayeaminika kulipwa mashahara wa juu zaidi duniani Fabio Capello ambaye anaweka kibindoni dola millioni 6.5 kwa mwaka. Matokeo mazuri zaidi kwa Urusi kwenye kombe la dunia ni mwaka wa 1966 walipomaliza wa nne.
BBC
No comments:
Post a Comment