TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTENDAJI WA SHIRIKA LA USAFIRI DAR ES SALAAM (UDA) KATIKA KUTOA HUDUMA YA USAFIRI WA UMMA
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekuwa ikifuatilia utendaji wa watoa huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam na kubaini kuwa baadhi ya mabasi yanayomilikiwa na Shirika la Usafiri Dar es Salaam yamekuwa yakikiuka Masharti ya Leseni ya Usafirishaji Abiria.
Ukiukwaji wa masharti ya leseni umebainika zaidi katika kutoza nauli zaidi ya zile zilizoridhiwa na SUMATRA, mabasi kutokuonyesha njia zinakotoa huduma, kukatisha njia (ruti) na madereva
kutokuvaa sare pamoja na kutoa lugha chafu kwa abiria.
Kutokana na hali hiyo Mamlaka ya SUMATRA ilitoa maelekezo kwa Menejimenti ya UDA kwa nia ya kuwataka kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Usafirishaji.
Baadhi ya maelekezo ambayo Mamlaka ya SUMATRA imeyatoa kwa UDA ili kuboresha huduma zao ni pamoja na kuajiri wataalamu wa usafirishaji wa kuendesha Shirika kupaka rangi inayoonyesha njia anayotoa huduma, kubandika vibao vinavyoonyesha njia anayotoa huduma na kutoza nauli zilizoridhiwa na SUMATRA.
Ieleweke kuwa UDA wanapaswa kufuata Sheria na Taratibu zote zinazopaswa kufuata na mtoa huduma ya usafiri hapa nchini.
Watumiaji wa huduma za usafiri pamoja na wananchi kwa ujumla wanahamasishwa kutoa taarifa kwa SUMATRA au Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani pale wanapoona watoa huduma yakiwemo mabasi ya UDA wanakiuka masharti ya leseni au kutoa huduma zisizoridhisha. Wananchi wanaweza kuwasiliana na Mamlaka zilizotajwa hapo juu kwa kupiga simu kwa kutumia namba za bure ambazo ni 0800110019 na 0800110020 ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Ni matumaini ya Mamlaka kuwa tukishirikiana, huduma za usafiri zinaweza kuwa bora na salama.
Imetolewa na:
Ofisi ya Mawasiliano kwa Umma
SUMATRA
1 comment:
Haleluyah!
ahimidiwe MUNGU Mwenyezi atuteteaye, hakika "sijawahi ona Mwenye haki ameachwa!!"
Post a Comment