3. Asante sana, nashukuru sana. Maneno hayo ya kiswahili yalizungumzwa na Bw. Bogani C. Majora, Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) aliyeshikana mkono na Balozi Tuvako Manogi, wakati Msajili huyo alipofika siku ya jumanne, katika Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa na kufanya mazungumzo ambapo pamoja na mambo mengine ameishukuru Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa Mahakama hiyo ambayo inaelekea ukiongoni mwa utekelezaji wa majukumu yake ya msingi. Pamoja na kwamba ICTR inamaliza shughuli zake, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipatia Tanzania dhamana ya ujenzi wa kituo kitakachosimamia umaliziaji wa kesi za masalia pamoja na uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu zote muhimu za ICTR majengo ya kituo hicho yatajendwa katika eneo la LakiLaki jijini Arusha wa kwanza kushoto ni msaidizi wa Msajili na wa mwisho kulia ni Bi. Tully Mwaipopo Afisa wa Uwakilishi wa Kudumu.
Na Mwandishi Maalum
Ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mfuko wa Umoja wa Mataifa unaohudumiwa Watoto ( UNICEF) umefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayolenga katika utoaji huduma endelevu kwa watoto .
Kauli hiyo imetolewa siku ya jumanne na Bibi. Anna Maembe, Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto , anayeiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Mwaka wa Bodi tendaji ya UNICEF unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa
Katika siku ya kwanza ya Mkutano huu viongozi mbalimbali, akiwamo Malkia Sophia wa Uhispania, Mke wa Rais wa Bukina Faso, Bibi Chantal Compaore Mawaziri, Makatibu Wakuu na Mabalozi walipata fursa ya kuchangia mawazo kuhusu mafanikio na changamoto mbalimbali zinazomkabili mtoto na nafasi ya UNICEF.
Pamoja na kwamba mkutano huu wa mwaka wa UNICEF unahusu zaidi kujadili taarifa za utendaji kazi wa Mfuko mafanikio na changamoto zake. Rais wa Bodi ambaye ni Mwakilishi wa Jamhuri ya Kenya katika Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Secretariet yake, aliandaa mkutano maalum ambapo washiriki wakiwamo wa kutoka Umoja wa Afrika ( AU) walipata fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu kuhusu Maendeleo endelevu katika Afrika, mkazo ukiwa kwa mtoto.
Ni katika mkutano huo maalum, ambapo Katibu Mkuu Maembe alipopewa fursa ya kuzungumza kuhusu Tanzania alisema. Tanzania imefanya mengi katika kumuendeleza mtoto kiafya, kielimu na utetezi wa haki zake za msingi.
Hata hivyo akaeleza kwamba juhudi hizo za serikali zimekuwa zikichangiwa na UNICEF na wadau wengine wa maendeleo, huku akisisitiza kwamba serikali imekuwa na ushirikiano mzuri na mfuko huo kiasi cha kujivunia.
Akaitaja baadhi ya miradi ambayo Serikali inatekeleza kwa ushirikiana na UNICEF na wadau wengine kuwa ni pamoja na huduma za utoaji vyakula vyenye virutubishe ili kukabiliana na tatizo kubwa la utapia mlo, utoaji wa madini joto, vitamini, chanjo mbalimbali zikiwamo za kuzuia ugonjwa wa homa ya mapafu na kuharisha.
Aidha akasema misaada ya kiufudi na kifedha inayotolewa na Mfuko huo ulifanikisha kufanyika kwa utafiti kuhusu vitendo vya kikatili dhidi ya watoto. Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuwa kuna vitendo vingi vya kikatili wanavyofanyiwa watoto, kiasi cha serikali kufungua vituo kwaajili ya kuwahudumua watoto dhidi ya udhalilishaji na ukatili na ambavyo vimefunguliwa karibu katika wilaya zote.
Katibu Mkuu akasema kuanzishwa kwa vituo hivyo kumeifanya serikali kuongeza bajeti katika eneo hilo. Aidha pamoja na utekelezaji wa miradi hiyo, akaongeza kwamba serikali pia imejitahidi sana katika eneo la upunguzaji wa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na fursa ya elimu kwa watoto wa jinsia zote.
Katika eneo hilo la elimu Katibu Mkuu amesema changamoto kubwa ni mimba za utotoni na ndoa za umri mdogo, maeneno ambayo yamekuwa tatizo kubwa kwa wanafunzi wa kike na hivyo kushindwa kuendelea na masomo yao.
Akahitimisha kwa kuitaka UNICEF kuendelea kushirikiana na Serikali hususani katika kipindi hiki cha kumalizia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) na baada ya 2015 wakati ajenda mpya za Maendeleo Endelevu zitakapoanza kutekelezwa.
Rais wa UNICEF Balozi Kamaku, akijumuisha majadilianyo hayo ambapo baadhi ya wazungumzaji waligusia pia suala la kutekwa kwa wasichana zaidi ya 200 na kundi la Boko Haramu huko Nigeria, na kutoa wito wa kutaka waachiwe huru. alisema, malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 lazima yajielekeze katika kuhakikisha kwamba changamoto zinazomkabili mtoto hususani katika Afrika, kama vile magonjwa, utapia mlo, ukosefu wa chakula na mengineyo yanamalizwa na kuwa historia.
Na kusisitiza kwamba haoni sababu ni kwa nini Afrika isiondokane na changamoto hizo na kwamba UNICEF inapashwa kuwa mstari wa mbele katika kuzipigania na kuzisemea changamoto hizo.
No comments:
Post a Comment